WANANCHI SHINYANGA,SIMIYU WAMETAKIWA KUJITOKEZA KUPATA ELIMU YA KISHERIA MAADHIMISHO WIKI YA SHERIA

WANANCHI SHINYANGA,SIMIYU WAMETAKIWA KUJITOKEZA KUPATA ELIMU YA KISHERIA MAADHIMISHO WIKI YA SHERIA

Migogoro ya Ardhi, Mauaji kinara ufunguaji Mashauri Mahakama Kuu

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

JAJI Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga Frank Mahimbali, amewataka wananchi wa Shinyanga na Mkoa wa Simiyu, wajitokeze kwa wingi kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria, ili kupata elimu ya kisheria bure na kutatuliwa migogoro yao kwa mujibu wa sheria.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga kiutawala ina hudumia Mikoa miwili ya Shinyanga na Simiyu.

Jaji Mahimbali akizungumza leo Januari 22, 2024 na Waandishi wa habari katika kuelekea kwenye Maadhimisho ya wiki ya sheria nchini, ambayo mkoani Shinyanga yata adhimishwa kwenye Viwanja vya Zimamoto kuanzia Januari 24 hadi 30.
Amesema kwenye Maadhimisho kutakuwa na utoaji wa elimu ya kisheria bure, na hivyo kuwasihi wananchi wa Shinyanga pamoja na Simiyu, wajitokeze kwa wingi kupewa elimu hiyo ambayo itawasaidia kupata haki zao kwa mujibu wa sheria.

“Kila ifikapo Decemba 15 hadi Januari 31 Mahakama hua ipo Rikizo, na kipindi hicho hua tunatumia kujitathimini na kubaini changamoto na kuzitatua, pamoja na kuadhimisha wiki ya sheria na kuanza mwaka mpya wa Kimahakama ambapo hua tuna uanza mwanzoni mwa mwezi Februari,”amesema Jaji Mahimbali.
“Tunawaomba wananchi katika Maadhimisho haya ya wiki ya Sheria wajitokeze kwa wingi kuja kupata elimu ya Sheria bure katika Viwanja vya Zimamoto pale Nguzo Nane, kutakuwa na utoaji wa elimu juu ya masuala ya Mirathi, Ndoa na Talaka, Makosa ya Jinai na Migogoro ya ardhi,”ameongeza.

Aidha, amesema pia watakuwa na wadau kutoka Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), ambao ni wadau Muhimu katika upatikanaji wa vitambulisho hivyo, ambavyo kwa sasa ndiyo vinatumika katika ufunguaji wa Mashauri Mahakamani, pamoja na Rita kwa ajili ya kusajili vizazi ili kuwapatia utambuzi wao.
Amesema kwa upande wa Mkoa wa Simiyu wananchi wataipata elimu hiyo ya kisheria katika Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mahakama ya wilaya Itilima, Busega, Meatu, Maswa, ambapo pia watatembelea Magereza na baadhi ya Shule.

Katika hatua nyingine Jaji Mahimbali, amesema Mahakama hiyo mwaka jana imepata mafanikio makubwa kwa kusikiliza mashauri yote na hakuna shauri ambalo limeachwa.

“Usikilizaji wa Mashauri mwaka jana tumeweza kufanya vizuri kwa kusikiliza Mashauri yote na hakuna mrudikano, ambapo kwa Mahakama Kuu Majaji wanapaswa kusikiliza Mashauri 220 kwa mwaka, lakini wengi walivuka lengo na kusikiliza mashauri zaidi ya 220 na wengine wamesikiliza mashauri hadi 360,”amesema Jaji Mahimbali.

Amesema pia wamejiwekea lengo la kusikiliza Mashauri, kwamba kwa Mahakama Kuu umri kusikiliza Mashauri usizidi miaka miwili, Mahakama za Wilaya na Mkazi muda ni mwaka mmoja, Mahakama za Mwanzo ni miezi sita, na Mashauri mengi yamesikilizwa na hakuna mrundikano.
Pia amesema kwa upande wa Mahakama Kuu, Mashauri ambayo yanaongoza kufunguliwa ni Migogoro ya Ardhi ikifuatiwa na Mauaji ambayo yanatokana na imani za kishirikina.

Kauli Mbiu ya Maadhimisho ya wiki ya Sheria mwaka huu inasema” Umuhimu wa dhana ya haki kwa ustawi wa Taifa, nafasi ya Mahakama na wadau katika kuboresha mfumo wa haki jinai.”

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464