RC MNDEME AGEUKA MBOGO KAYA 142 HAZINA VYOO WANAJISAIDIA VICHAKANI, SITA WAFARIKI KWA KIPINDUPINDU SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amemwagiza Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, pamoja na Watendaji wote wa Serikali, kufanya msako na kuwapiga faini wananchi katika Kata ya Idukilo wilayani humo ambao bado hawajajenga vyoo, na wataogoma kulipa faini wafikishwe Mahakamani.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme.
Kata hiyo ya Idukilo wilayani Kishapu ambayo ndiyo imekumbwa na Ugonjwa wa Kipindupindu kwa kiwango kikubwa, imebainika kwamba Kaya 142 hazina vyoo na wananchi wake hujisaidia vichakani, na ndiyo chanzo cha kuenea kwa Ugonjwa huo.
Mndeme amebainisha hayo leo Januari 23, 2024 wakati alipofanya ziara katika Kata hiyo ya Idukilo, akiwa ameambatana na Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu, kuzungumza na wananchi katika kukabiliana na Ugonjwa huo wa Kipindupindu.
Mganga Mkuu wa Serikali Prof; Tumaini Nagu.
Amesema ni Aibu Kaya 142 katika Kata hiyo ya Idukilo kutokuwa na vyoo, na wananchi kujisaidia vichakani na ndiyo chanzo cha ugonjwa huo wa kipindupindu kushindwa kuondoka kwenye Kata hiyo, nakumuagiza Mkuu wa wilaya ya Kishapu na watendaji wote kufanya msako pamoja na kuwapiga faini watu wote ambao hawana vyoo.
“Mkuu wa wilaya na watendaji wote wa Serikali kumbe ilitolewa siku wananchi hawa katika Kaya hizi 142 wawe wameshajenga vyoo na leo ndiyo ilikuwa siku ya mwisho, hivyo hakuna kuongeza siku ya kujenga vyoo na msako huu uanze mara moja wasiona vyoo piga faini ambao hawana peleka Mahakamani ugonjwa huu siyo wa kuchekeana,”amesema Mndeme.
“Wananchi wanapojisaidia vichakani hasa katika msimu huu wa mvua kinyesi hurudi kwenye vyanzo vya maji, na maji hayo ndiyo wanayatumia na kusababisha ugonjwa kuendelea kuwepo, hapa tu Idukilo wanawake 80 wameathirika na ugonjwa huu wa Kipindupindu na wanaume ni 59,”ameongeza.
Aidha, ametaja takwimu za ugonjwa wa kipindupindu kwa Mkoa mzima wa Shinyanga kwamba mpaka watu 139 wanaugua ugonjwa huo, 398 wamekutana na watu wenye kipindupindu huku vifo vikiwa watu 6.
Naye Mtendaji wa Kata ya Idukilo Marrysiana Robert, amesema awali walishapitisha sheria ndogo na kutoa maagizo kwamba kwa wananchi wote ambao hawana vyoo hadi kufikia leo Januari 23, 2024 wawe wameshajenga vyoo na ambao bado watapigwa faini ya Sh.50,000 na ambao hawatatoa watafikishwa Mahakamani.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Serikali Prof, Tumaini Nagu, amewataka wananchi kuzingatia suala la usafi wa mazingira muda wote pamoja na kunawa mikono kwa majisafi na salama na sabuni wakati wa kula vyakula pamoja na kuacha kufua nguo za wagonjwa kwenye vyanzo vya maji.
Amewataka pia wananchi pale wanapomuona Mgonjwa anatatizo ka kutapika na kuhara wamuwahishe kwenye huduma za Afya ili apate matibabu na kuacha kukaa nao nyumbani hali ambayo ni hatari kuweza kupoteza maisha, huku akitolea mfano kwa wagonjwa ambao walifariki Kahama kwamba Wanne walifia nyumbani na Mmoja kuchelewa kufikishwa hospitalini.
Amesema Serikali imeshatoa vifaa tiba na kinga kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo, pamoja na dawa za kutibu maji kwa kuua wadudu wenye vimelea vya Kipindupindu zenye thamani ya Sh.milioni 7.