Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha pikipiki zilizoibiwa
Na Suzy Butondo Shinyanga Press Club Blog
Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga limekamata watuhumiwa 76 ambao walifanya matukio mbalimbali yakiwemo ya wizi na limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya wizi ikiwemo bunduki moja aina ya Shortgaun Pump Action yenye namba za usajili MV.95738V ambayo iliibiwa huko katika kijiji cha Mondo Wilaya ya Kishapu Mkoani hapa.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoani Shinyanga ACP Janeth Magomi akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo januari 24,2024 ambapo amesema katika doria na misako iliyofanyika kati ya Disemba 21,2023 hadi Januari 23,2024 jeshi hilo limefanikiwa kukamata vifaa mbalimbali vya wizi.
Magomi amesema licha ya kukamata Bunduki jeshi hilo limefanikiwa kukamata simu mbili, mafuta ya dizeli lita 100 pikipiki nane, betri tatu za gari, kompyuta mpakato (Laptop) mbili EMS Foot massager moja, Radio moja na spika moja.
"Vitu vingine vilivyokamatwa ni vipande 120 vya nondo, mifuko minne ya unga wa ngano mafuta ya kula lita 15, vipande nane vya bomba vipande tisa vya vyuma (angle line) mashine mbili za kusukuma maji, extension cable moja, Grander moja, sigara pakiti 30, pombe ya moshi lita 150, Mirungi bunda 94, boksi tano za vifaa tiba aina ya gloves,"amesema Magomi.
Magomi amevitaja vitu vingine vilivyokamatwa ni gorol 125 za kusaga mawe, mtambo mmoja wa kutengeneza pombe ya moshi, sufuria moja bhangi kilo mbili na kete moja pamoja na vifaa mbalimbali vya kupiga ramli chonganishi, pamoja na watuhumiwa 76 ambao walikamatwa katika vituo mbalimbali.
Kamanda Magomi amesema kwa upande wa mahakamani jumla ya kesi 11 zimepata mafanikio ambapo kesi mbili za kubaka, washtakiwa wawili walihukumiwa miaka 30 jela kesi moja ya wizi wa mifugo, washtakiwa wawili washtakiwa wawili walihukumiwa miaka miwili jela, kesi moja ya kujeruhi mshitakiwa mmoja alihukumiwa mwaka mmoja kifungo cha nje, kesi moja ya wizi mshitakiwa alihukumiwa miezi tisa jela.
Amesema kesi zingine za mahakamani ni shambulio la kudhuru mwili kesi tatu washtakiwa watatu ambao walihukumiwa miezi mitatu jela, shambulio la kawaida kesi mbili washitakiwa wawili walihukumiwa kwenda jela miezi mitatu hadi sita na kuingia kwa jinai kesi moja mshitakiwa alihukumiwa kwenda jela miaka mitatu.
"Katika makosa ya barabarani tumefanikiwa kukamata jumla ya makosa 4846 ambapo makosa 4844 watuhumiwa waliajibishwa kwa kutoa faini za papo kwa papo na makosa mawili yaliyohusisha ajali kwa kukiuka utaratibu,kanuni na sheria za usalama barabarani yalifikishwa mahakamani na washtakiwa kulipa faini za mahakamani na kuonywa kutorudia makosa,"amesema Magomi.
Hata hivyo jeshi la polisi Mkoa wa Shinyanga linawashukuru wananchi kwa kuendelea kutoa ushirikiano katika kupambana na uhalifu na wahalifu kwa kutoa taarifa, sambamba na hilo linawataka madereva na watembea kwa miguu kutii na kuheshimu alama, michoro na sheria za usalama barabarani wakati wote wanapokuwa barabarani.
Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga akionyesha bunduki moja aina ya Shortgaun Pump Action yenye namba za usajili MV.95738V ambayo iliibiwa huko katika kijiji cha Mondo Wilaya ya Kishapu Mkoani hapa.
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha kompyuta iliyoibiwa
Kamanda wa jeshi la polisi Mkoani Shinyanga Janeth Magomi akionyesha Bange zilizokamatwa wakati jeshi hilo likiendelea na doria
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464