TAKUKURU kuchunguza upigaji Milioni 25/- Kituo cha Afya Bulige
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Ruwashwa (TAKUKURU) Mkoa wa Shinyanga, imeanzisha uchunguzi wa kutoonekana Vifaa vya Ujenzi katika Kituo cha Afya Bulige Halmashauri ya Msalala, ambavyo tayari vimeshalipiwa Sh.milioni 25,lakini havipo eneo la mradi wala kwenye kumbukumbu ya Vitabu vya Stoo.
Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy, amebainisha hayo leo Februari 7,2024 wakati akitoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Amesema Taasisi hiyo ilifanya ufuatiliaji wa Miradi ya Maendeleo ukiwamo Ujenzi wa Kituo cha Afya Bulige Halmashauri ya Msalala, na kubaini kuna vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh.milioni 25 yakiwemo Madirisha ya Alluminium, kwamba vimeshalipiwa lakini vifaa hivyo havijafikishwa kwenye eneo la mradi na havipo kwenye kumbukumbu ya Vitabu vya Stoo.
“Hatua ambayo imechukuliwa kwenye ujenzi wa Kituo hiki cha Afya Bulige, Uchunguzi umeanzishwa,”amesema Kessy.
Aidha, amesema pia walifanya uchambuzi wa Mfumo kuhusiana na Stakabadhi za EFD kwa Wazabuni wanaofanya biashara na Halmashauri, na kubaini kumekuwepo na utolewaji wa Risiti za EFD ambazo ni za Kughushi.
Aidha, amesema katika uchambuzi huo wa Mifumo, wamebaini pia kuwepo kwa EFD zenye utambulisho wa TIN namba ya Mfanya biashara tofauti na anayetoa huduma au bidhaa.
“Tumeshauri elimu kwa wananchi itolewe dhidi ya Matumizi Sahihi ya Risiti za EFD, na kuanzishwa kwa uchunguzi wa Risiti hizi za Kughushi,”amesema Kessy.
Amesema walifanya uchambuzi pia wa Mfumo wa Matumizi ya Fedha za TASAF, na kubainika kuna madai ya wasimamizi wa miradi na mafundi ambayo hayajalipwa, na kwamba wamemtaka Mratibu wa TASAF Mkoa wa Shinyanga, kufanya Mawasiliano na Makao Mkuu ili madai hayo yalipwe.
Ameeleza kwamba pia wamefanya uchambuzi wa mfumo kuhusiana na utoaji wa huduma za Ardhi kupitia Mabaraza ya Ardhi na kubaini wananchi kutolipa Kodi ya Pango la Ardhi na Nyumba baada ya kufanyiwa umilikishwaji.
Katika hatua nyingine amesema katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka wa fedha 2023/2024 walifanya ufuatiliaji wa miradi ya SEQUIP (Mpango wa Uboreshaji wa elimu ya Sekondari) ili kuona kama miradi inatekelezwa kwa wakati na katika ubora na viwango vinavyotakiwa.
“Kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Mkoa wa Shinyanga ulipokea shingi Bilioni 5.2 (5,283,343,372/=), fedha hizi zilikuwa ni kwa ajili ya ujenzi wa miradi 13 ambayo ni shule mpya sita za sekondari, ujenzi wa nyumba sita 2 in 1 za walimu na ujenzi wa shule ya wasichana ya mkoa”,amesema Kessy.
Amesema pia wamefanya ufuatiliaji wa miradi 10 ya SEQUIP yenye thamani ya Shilingi 4,063,343,372/= na kujiridisha kuwa mbali na uwepo wa changamoto zinazorekebishika, miradi hiyo imetekelezwa kwa ufanisi na ubora unaotakiwa na miradi hiyo kama shule na nyumba za walimu imeshaanza kutumika.
Katika hatua nyingine amesema kwa kipindi cha kuanzia Septemba hadi Disemba mwaka jana, kwamba walipokea taarifa zinazohusu Rushwa kisekta ambapo Ujenzi walipokea Taarifa Mbili, Maji Moja, Elimu Mbili, Kilimo Moja, Nishati Moja, Mahakama Moja, Polisi Moja, Afya Moja na Ardhi Moja.
Ametaja Mikakati ya utendaji kazi kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Marchi mwaka huu, kwamba wataendelea kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili iendane na thamani halisi ya fedha zinazotolewa na Serikali, pamoja na kutoa elimu ya Rushwa kwa wananchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464