RC MNDEME AMEWATAKA WAZAZI KUWAPELEKA WATOTO KUPATA CHANJO YA SURUA NA RUBELLA


RC MNDEME AMEWATAKA WAZAZI KUWAPELEKA WATOTO KUPATA CHANJO YA SURUA NA RUBELLA

Watoto 300,193 wanatarajiwa kupata Chanjo hiyo

Na Marco Maduhu, SHINYANGA

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme, amewataka wazazi mkoani humo kuwapeleka watoto wao wenye umri kuanzia Miezi 9 hadi 59, kwenye Vituo vilivyopangwa ili wakapate Chanjo ya Surua na Rubella ili kuwakinga dhidi ya Magonjwa hayo, ambapo watoto 300,193 wanatarajia kupata Chanjo hiyo.
Mndeme amebainisha hayo leo Februari 14, 2024 wakati akifungua kikao cha Kamati ya huduma za Afya ya Msingi kwa ajili ya Maandalizi ya Kampeni ya Kitaifa ya Chanjo dhidi ya Magonjwa ya Surua na Rubella, Tathimini ya Lishe na Mwenendo wa Ugonjwa wa Kipindupindu.

Amesema Kampeni hiyo ya Chanjo ya Surua na Rubella inaanza kutolewa kesho Februari 15 hadi 18 katika Vituo 236 vya kutolea huduma za Afya, pamoja na Vituo 123 vya muda ambavyo vimeandaliwa kwa ajili ya kutoa huduma hiyo.
“Kampeni hii ina lengo la kuongeza kinga kwa watoto wote wenye umri wa miezi 9 hadi 59 kwa kuwapatia Chanjo hata kama wameshapata Chanjo hizo kwa utaratibu wa kawaida, wanapaswa kupata Chanjo tena sababu hazina Madhara ili kumkinga Mtoto na Magonjwa hayo,”amesema Mndeme.

Katika hatua nyingine akizungumzia upande wa Lishe, amesema Mkoa huo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kupambana na tatizo la Utapiamlo kwa watoto waliochini ya umri wa miaka Mitano, wameweza kupunguza kiwango cha Udumavu kutoka asilimia 32.1 mwaka 2018 hadi asilimia 27.5 mwaka 2022.
Amesema Uzito pungufu wameweza kupunguza kiwango kutoka asilimia 13.3 mwaka 2018 hadi asilimia 8.6 mwaka 2022, Ukondefu kutoka asilimia 4.3 hadi 1.3, na kwamba richa ya mafanikio hayo lakini bado kiwango cha udumavu kipo juu ambapo kinatakiwa kuwa chini ya asilimia 20 ya kiwango cha Kitaifa.

Aidha, amesema kwa upande wa utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Nusu mwaka yani Julai hadi Disemba 2023, kwamba viashiria vyote 14 vimetekelezwa kwa kiwango cha kuridhisha kwa kufikia zaidi ya asilimia 90 kwa kila kiashiria kwa Wastani wa Kimkoa, na fedha zilizopangwa kutumika kwa kipindi husika zimetolewa zaidi ya Sh.1000 kwa kila Mtoto.
“Pamoja na Mafanikio ya utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Juali hadi Disemba 2023 kuna Changamoto zilionekana kwenye utekelezaji wa Mkataba huo, ambazo ni fedha za utekelezaji hazitolewi kwa wakati na hivyo kuathiri shughuli za lishe,

“Kukosekana kwa Vitendanishi vya kupima madini Joto kwenye Chumvi, na kusababisha Halmashauri kutofanya upimaji wa madini Joto kwenye chumvi,”amesema Mndeme.
Aidha, amewataka Wakurugenzi kuhakikisha fedha za Lishe zinatolewa kwa wakati kulingana na mpango kazi, Vitendanishi vya kupima Madini Joto kwenye Chumvi vipatikane, pamoja na elimu kutolewa kwa wazazi ili watoto wapatiwe Lishe sahihi na kupelekwa Kliniki kupata huduma stahiki za Afya.

Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Faustine Mlyutu, ametaja dalili za Magonjwa ya Surua na Rubella kwamba ni homa kali ikiambatana na vipele vidogo na kuenea Mwili mzima, ambapo Madhara yake ni Maskio kutoa Usaha,Vidonda vya Macho na hata kusababisha upofu,Nimonia,Utapiamlo,na kuvimba Ubongo.
Aidha, amezungumzia pia utekelezaji wa Mkataba wa Lishe kwamba kuna ongezeko la fedha zinazotumika kutekeleza Afua za Lishe kutoka Sh. 229,795 mwaka wa fedha (2020/2021), hadi kufikia Sh. 447,844 mwaka wa fedha (2022/2023), na kuonyesha kuimarika kwa utekelezaji wa Afua za Lishe ngazi za Halmashauri.

TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Christina Mndeme akizungumza kwenye kikao hicho.
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof; Siza Tumbo akizungumza kwenye kikao hicho.
Kaimu RMO Mkoa wa Shinyanga Fuastine Mlyutu akizungumza kwenye kikao hicho.
Dk.Mageda Kihulya kutoka TAMISEM akizungumza kwenye kikao hicho.
Viongozi wakiwa Meza Kuu.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao hicho.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Wajumbe wakiendelea na kikao.
Kikao kikiendelea.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464