Darasa la Mfano kwa wanafunzi wa awali shule ya msingi Anderson.
Na Kareny Masasy
PROGRAMU Jumuishi ya Taifa ya Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (MMMAM) imelenga kuwekeza moja kwa moja kwenye maendeleo ya binadamu kwa kukuza malezi jumuishi yenye tija kwa kuhimiza ushiriki wa uchumi ikiwemo sekta ya Elimu.
kupitia program hiyo inaeleza shule binafsi za madhehebu ya dini mwanzoni zilionekana kuongoza kutoa elimu ya darasa la awali nakuwafikia asilimia tano ya watoto wote wenye umri wa miaka minne wengi wao wakiwa maeneo ya mjini.
Shule hizo zilikuja na mipango madhubuti ya kuhakikisha mtoto anafundishwa kupitia zana za ujifunzaji zilizo rahisi madarasa yaliyochorwa picha ndani na nje,mikeka ya kupumzikia ikiwemo bembea kwaajili ya michezo.
Serikali ya Tanzania imekuja na malengo mahususi ya kuhakikisha wanaanza kujenga shule za mfano kwa kuweka dhana na michoro kupitia mradi wa Boost kwenye shule chache kwa kila halmashauri na baadaye kwenye shule zote.
Baadhi ya walimu wanakiri mwanafunzi wa darasa la awali anapoona maneno mafupi na picha zimechorwa hupenda kuangalia na darasa huwa kimya hata wakiwa peke yao hufundishana.
Mwalimu Christina Gabriel ambaye ni Mwalimu anayefundisha darasa la awali shule ya msingi Anderson iliyopo kata ya Majengo manispaa ya Kahama anasema darasa hilo limejengwa mwaka jana (2023) likiwekewa zana zote za ujifunzaji na kuchorwa picha.
“Nilichojifunza kupitia darasa hili watoto wakiona picha wanakuwa na moyo wa kujifunza na kufundishana wao kwa wao kuwa hii ni herufi gani au namba gani”anasema Gabriel.
mwanzoni walikuwa na darasa ambalo lilikuwa halina dhana za ujifunzaji wala michoro ya picha,michezo ya kwenye bembea nakuwafanya watoto wasitamani kuendelea kuwemo darasani au mazingira ya shule mpaka kutumia nguvu.
“Kutokuwa na darasa lenye dhana za ujifunzaji na dhana za michezo humfanya mtoto kwanza kuichoka shule mapema kwa kuona hakuna utofauti na nyumbani lakini sasa hata michoro inawavutia na kubembea”anasema Gabriel.
Wanafunzi wa darasa la awali wamekuwa wakifundishwa mahusiano na kujitambua kwani kila mtoto amelelewa katika mazingira yake wanapofika shuleni wanakuwa kitu kimoja cha kuelewana.
Wanafunzi wa darasa la awali hawatakiwi kuachwa peke yao muda mrefu kila wakati unakuwa nao sababu wanatabia tofauti tofauti utakuta mmoja anamchokoza mwingine.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Anderson Scolastika Leonard anasema darasa la awali limejengwa la mfano kupitia mradi wa fedha za Boost lina vyumba viwili vya madarasa.
“Kupitia mradi huo kumejengwa matundu manne ya vyoo na dhana za ujifunza zilizomo ndani ya madarasa hayo na bembea za michezo kwa wanafunzi zilizopo nje ya darasa”anasema Mwalimu Leonard.
Mwalimu Leonard anasema wanafunzi wanaopokelewa kuanza darasa la awali ni wenye umri wa kuanzia miaka minne na mitano ikiwa maoteo kwa mwaka 2024 ilikuwa kuwaandikisha wanafunzi 104 lakini mpaka sasa walioandikishwa ni wanafunzi 131.
Kaimu Ofisa elimu manispaa ya Kahama Sadiki Juma anasema darasa la awali kwa shule ya msingi Anderson limejengwa mwaka mwaka 2023 kwa gharama ya shilingi Millioni 55 ukijumlisha matundu ya vyoo manne na vifaa vyote vinavyohitajika.
Juma anasema kuna shule tatu zilizonjengwa madarasa ya awali ya mfano kupitia mradi wa Boost ambazo ni shule ya msingi mlimani, Majengo na Anderson.
“lengo la serikali kuangalia matokeo ya madarasa hayo na baadaye zijengwe kwenye shule zote za msingi”anasema Juma.
Ofisa elimu mkoa wa Shinyanga Dafrosa Ndalichako anasema uandikishaji wa darasa la kwa mujibu wa matokeo ya sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 matarajio ni kuandikisha wanafunzi 75,079.
Mzazi James Kija mkazi wa kata ya Majengo anasema mtoto wake ana umri wa miaka mitano alipomuandikisha kuanza darasa la awali alikuwa anakataa kurudi nyumbani au wakati mwingine anataka kurudi shuleni jioni.
Magreth Samweli mkazi kata ya Majengo anasema mtoto wake ana umri wa miaka minne amemuanzisha darasa la awali katika shule hiyo akirudi nyumbani anasimulia picha alizoziona na alivyobembea.
Mtaalamu wa Malezi na Makuzi kutoka shirika la Children in Crossfire (CiC) nchini Tanzania Davis Gisuka anasema mtoto akianza kupata elimu ya awali inamjenge uwezo wa kuanza kufahamu kuandika na kusoma na michezo mbalimbali ikiwemo nyimbo.
Kwa mujibu wa toleo la kitabu cha Programu Jumuishi ya Taifa ya Makuzi,Malezi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ( PJT-MMMAM) inaeleza Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye elimu ya awali kuifanya kuwa ya lazima.
Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho ni elimu ya awali katika elimu ya msingi kwa kuzitaka shule zote za msingi kuwa na darasa la elimu ya awali.
Wanafunzi wa darasa la awali wakiwa na mwalimu wao wakifurahia mchezo wa bembea.
Darasa la mfano kupitia mradi wa Boost
Wanafunzi wakiwa darasani