HOSPITALI YA WILAYA YA SHINYANGA YAKABIDHIWA GARI LA WAGONJWA
Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Salum, amekabidhi gari la kubebea wagonjwa katika Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga ambalo limetolewa na Serikali kupitia Wizara ya Afya.
Gari hilo limekabidhiwa hivi karibuni katika hafla fupi iliyofanyika katika Hospital ya Wilaya ya Shinyanga.
Akikabidhi gari hilo, Mhe. Ahmed, ametoa shukrani za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake katika kutatua changamoto mbalimbali za wananchi hasa katika sekta ya afya hususani kwa wazee, wanawake na watoto.
‘’ Leo tumepata gari hili zuri na la kisasa ili litatue changamoto ya usafiri hususani kwa akina mama wajawazito. Naomba nimshukuru sana Rais wetu, Dkt. Samia Suluhu Hassan, yeye kama mama amefanya jambo hili karibia nchi nzima. Kwa miaka yake hii michache amefanya makubwa sana katika miradi mbalimbali ukiwemo huu wa afya. Mimi binafsi nimekuwa Mbunge kutoka 2005 sijawahi kupata fedha nyingi za miradi kama hizi ambazo anatoa katika awamu yake kama Rais wa nchi ya Tanzania’’
Aidha, Mhe. Ahmed, amewashukuru watumishi wote wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga kwa kujitolea kwao katika kutoa huduma bora kwa wananchi kwa sababu wao ni sehemu kubwa sana katika kuifanya sekta ya afya isaidie maisha ya wananchi. Vile vile, amewaomba wazidi kufanya kazi kwa juhudi maana Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo kwa ajili yao na watanzania wote.
Awali, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga, Dkt. Tom John Mtitu, amemshukuru Mbunge huyo na kusema kuwa gari hilo litatatua changamoto ya usafiri kwa wagonjwa wanaopata rufaa katika vituo vya afya na Hospital ya Wilaya. Pia amewaomba watumishi wenzake kutunza mali na vifaa vinavyotolewa katika kuwawezesha kutimiza majukumu yao wanapokuwa wanatoa huduma za kiafya kwa wagonjwa.
Kwa upande wao wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Bi. Agnes Masanja Dogani na Bi. Jesca Charles Salawa, wakazi wa Kata ya Iselamagazi wametoa shukrani zao za dhati kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwaletea gari la kubebea wagonjwa. Hii inaonyesha anavyojali afya za kinamama pamoja na watoto hasa kinamama wajawazito ambao hukumbwa na changamoto za kiusafiri wanapokuwa katika hali ya kujifungua.
Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Salum akimkabidhi ufunguo
wa gari la kubebea wagonjwa Dereva wa hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Enock Mshama
Muonekano wa gari la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa leo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga Dkt. Tom John Mtitu akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhigari la wagonjwa.
Mkuu wa Divisheni ya Huduma za Afya , Ustawi wa Jamii na Lishe Dr. Nuru Yunge akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa.
Diwani wa Kata ya Iselamagazi, Mhe Isack Sengerema akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa.
Picha ya pamoja ya Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Ally Salum na baadhi ya Watumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Shinyanga.
Picha ya Pamoja ya Mbunge wa Jimbo la Solwa, Mhe. Ahmed Ally Salum na baadhi ya wananchi waliohudhuria hafla ya kukabidhi gari la wagonjwa.