SHIRIKA LA BINTI MSAFI LATOA MSAADA WA TAULO ZA KIKE SHULE YA SEKONDARI LYASIKIKA

 

Shirika lisilo la kiserikali  la Binti Msafi Foundation, lenye makao makuu yake Wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro, limetoa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi 185 wa Shule ya Sekondari Lyasikika iliyopo katika kata Kata ya Machame Mashariki wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro.

Hafla fupi ya kukabidhi taulo hizo za kike iliyofanyika leo Februari 1,2024 imeenda sanjari na zoezi la kuotesha miti kwa ajili ya Kutunza na kuboresha mazingira shuleni hapo.

Akizungumza katika shule hiyo, Mkurugenzi wa Shirika la Binti Msafi Foundation bi Irene Lema amesema kuwa, ni utamaduni wa Shirika hilo kusaidia wanafunzi wa kike katika wilaya hiyo ya Hai, kutokana na wanafunzi wengi kushindwa kujistiri wakati wa masomo na kipindi cha mitihani.

Mbali na kutoa taulo za kike, Shirika pia linatoa elimu ya hedhi kwa wanafunzi hao, ili kuweza kujitunza na kuwa maridadi na salama kwa kipindi  chote cha hedhi. 

Irene amesema Shirika hilo litaendelea kutoa msaada kwenye maeneo mengine katika Shule za Wilaya ya Hai,  na kusaidia katika kampeni ya utunzaji wa mazingira ili kuirejesha Kilimajaro ya zamani yenye uoto wa asili mzuri kwa kuongeza jitihada za upandaji wa miti kwa kila taasisi binafsi na za umma.

Ametoa wito kwa Watanzania kuona umuhimu wa kusaidia watoto wa kike waweze kusoma na kuhitimu vyema masomo yao wakiwa na tabasamu  pamoja na kusoma katika mazingira mazuri na kutunza mazingira hayo. 

Naye Mhandisi Pamela Massay, aliyeambatana na Mkurugenzi wa Shirika hilo ametoa rai ya utunzaji wa mazingira katika Mkoa wa Kilimanjaro na Tanzania kwa ujumla ili kukabiliana na  mabadiliko ya tabia nchi.




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464