Na Eleuteri MangiUtekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi (LTIP)katika Halmashauri ya Mji Nzega katika mkoa wa Tabora umetekelezwa kwa asilimia 55 na kutarajiwa kukamilika Juni 30,2024 .
Akimkaribisha Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Mhe. Japhet Hasunga na ujumbe wake wakati wa ziara ya Kamati hiyo wilayani Nzega tarehe 27 Machi 2024, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Geophrey Pinda amesema utekelezaji wa Mradi wa Uboreshaji Usalama wa Milki za Ardhi katika mji wa Nzega unatekelezwa katika mitaa 14 iliyopo Kata za Nzega Mashariki, Nzega Magharibi, Nzega ndogo, Kitangiri na Uchama.
Amebainisha kuwa, katika kata ya Nzega Mjini Mashariki mradi unatekelezwa Mitaa ya Maporomoko, Uwanja wa Ndege, Msoma, Mwaisela, Nyasa pamoja na Kitongo. Aidha, Kata ya Nzega Mjini Magharibi mradi unatekelezwa katika mitaa ya Ipilili, Mbugani, Ushirika na Utemini.