UTAFITI WABAINI WATANZANIA WANAUNGA MKONO MIKAKATI YA KUPUNGUZA UZALISHAJI WA GESI YA METHANE KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA

UTAFITI WABAINI WATANZANIA WANAUNGA MKONO MIKAKATI YA KUPUNGUZA UZALISHAJI WA GESI YA METHANE KUKABILIANA NA MABADILIKO YA HALI YA HEWA
    Na Mwandishi Wetu

WATANZANIA wameonekana kuunga mkono kwa kiasi kikubwa mipango inayolenga kupunguza uzalishaji wa gesi ya methane na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Global Methane Hub Shirika la kibinadamu linalojitolea kupunguza uzalishaji wa methane duniani.

Utafiti huo, ambao ulijumuisha nchi 17 katika mabara sita, umetoa ufahamu wa jinsi jamii inavyoiona hali ya mazingira na njia za kisheria za kurekebisha hali hiyo. Matokeo ya utafiti huo yanaonesha kwamba asilimia 83 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sera zinazolenga kupunguza uzalishaji hatari wa methane, na kati yao, asilimia 49 wanatoa uungaji mkono mkubwa, kiwango ambacho ni cha juu zaidi kuliko nchi nyingine zilizofanyiwa utafiti.

Zaidi ya hayo, asilimia 87 ya Watanzania wanaamini kwamba shughuli za binadamu ndio sababu kuu ya mabadiliko ya hali ya hewa, ikionesha ufahamu mkubwa wa umuhimu wa kuchukua hatua za kupunguza athari hizo. Utafiti huo pia unaonesha kwamba asilimia 88 ya washiriki kutoka Tanzania wanapendelea sheria zinazolenga kupunguza upotevu wa chakula na utupaji sahihi wa taka za kikaboni, ambazo ni moja ya vyanzo vikuu vya uzalishaji wa methane.

Kwa mujibu wa Marcelo Mena, Mkurugenzi Mtendaji wa Global Methane Hub, “kupunguza uzalishaji wa methane ni njia ya haraka zaidi ya kupunguza ongezeko la joto duniani na kudhibiti athari za mabadiliko ya hali ya hewa.”

Utafiti pia unaonesha kwamba wale wanaoathiriwa zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa ndio wanaotoa uungaji mkono mkubwa kwa jitihada za kupunguza methane.

Utafiti huo unathibitisha pia kwamba uungaji mkono wa mikakati ya kupunguza gesi ya methane umebaki imara licha ya tofauti katika ufahamu wa awali wa gesi hiyo katika nchi zilizofanyiwa utafiti. Hata hivyo, wasiwasi mkubwa pia umeelekezwa kwa suala la ubora wa maji, ambapo asilimia 76 ya washiriki kutoka Tanzania wameripoti wasiwasi mkubwa kuhusu hilo.

Natalie Lupiani, ambaye ni Makamu wa Rais wa kampuni ya BSG, anasisitiza kwamba data hizi ni ishara nzuri kwamba watu wanaunga mkono serikali zao katika kuchukua hatua za kuwalinda dhidi ya ongezeko la joto duniani. Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi tatu zilizoathiriwa zaidi, pamoja na Brazil na Kenya, huku karibu nusu ya washiriki wakiripoti athari kali katika maisha yao ya kila siku.

Mwenyekiti wa Jopo la Kitaalam la Sayansi la Hali ya Hewa na Hewa Safi (The Climate and Clean Air Coalition Scientific Advisory Panel), Drew Shindell, amesisitiza umuhimu wa kupunguza uzalishaji wa methane mara moja ili kuzuia jamii dhidi ya athari mbaya za uchafuzi wa hewa na mabadiliko ya hali ya hewa.

Ripoti inaonesha kuwa kupungua kwa kiasi kikubwa katika ongezeko la joto kunaweza kutokea kupitia juhudi za kupunguza methane kwa asilimia 45, ambayo itasaidia kuleta mustakabali bora na kufikia malengo ya kimataifa ya hali ya hewa.

Utafiti huo pia unaonesha kwamba watu duniani kote wanaona serikali za kitaifa, biashara, na watu binafsi kuwa wajibu wa uharibifu wa mazingira, lakini kuna imani kubwa kwamba biashara kubwa na serikali zinaweza kuleta mabadiliko muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Utafiti huu uliwafikia watu katika nchi 17 kote ulimwenguni kwenye mabara sita, ukikusanya data kutoka kwa watu wazima 12,976, takriban 750 kutoka kila nchi.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464