Viongozi wa Kijiji cha Mwamagunguli wakiwa katika Boma la Zahanati
RIPOTI MAALUMU; UJENZI ZAHANATI YA MWAMAGUNGULI PASUA KICHWA MIAKA 14 IMESHINDWA KUKAMILIKA
Wananchi wadai kuchoshwa na ahadi za uongo za viongozi
Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Kukosekana kwa huduma za Afya maeneo ya Vijijini imekuwa tatizo kwa wanawake wa maeneo hayo kukosa elimu ya Afya ya uzazi na uzazi wa mpango, pamoja na kuendelea kujifungua majumbani na wengine njiani wakifuata huduma za afya umbali mrefu.
Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007 inasema kwamba,Serikali itashirikisha wananchi katika kuimarisha huduma za Afya katika ngazi zote, na kila Kata inapaswa kuwa na Kituo cha Afya, na Zahanati kwa kila Kijiji.
Sera hiyo inasema, wananchi watashiriki kuanzisha ujenzi wa boma hadi kufika hatua ya Renta, ndipo Serikali itamalizia ujenzi huo na kuanza kutolewa huduma kwa wananchi.
WANANCHI.
Wananchi wa Kijiji cha Mwamagunguli Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga, hali hiyo imekuwa tofauti kwao ambapo walianzisha ujenzi wa Zahanati mwaka 2010 kwa nguvu zao na sasa ipo hatua ya Renta, lakini imefikisha miaka 14 bado haijamaliziwa kujengwa na Serikali.
Wanawake katika Kijiji hicho cha Mwamagunguli, wanapaza kilio kwa Serikali kuikamilisha Zahanati hiyo, ili wapate huduma za kujifungua karibu, pamoja na kupata huduma zingine za elimu ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango.
Ester Shija mkazi wa Kijiji cha Mwamagunguli, anasema kutokamilika kwa ujenzi wa Zahanati Kijijini humo, wanawake wamekuwa wakipata shida ya huduma za afya sababu wao ndiyo wahitaji wakubwa hasa huduma za uzazi.
Amesema huduma za afya ambazo wanawake wamekuwa wakizipata kijijini humo, ni kutoka Hospitali ya Kolandoto ambayo ipo chini ya Kanisa la AICT, na kwamba baadhi ya huduma za uzazi hua hawazipati ikiwamo ya uzazi wa mpango kutokana na Sera zao za Kanisa kutotoa huduma hiyo.
“Sisi kuwa na Zahanati yetu hapa Kijijini ni faraja kubwa hasa kwa wanawake, sababu tutapata elimu mbalimbali zinazohusu masuala ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango sababu Hospitali ya Kanisa haina huduma hizi,”anasema Ester.
MHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII.
Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii Ester Emmanuel, anasema kwamba wanawake katika Kijiji hicho kukosa huduma za Afya karibu, baadhi yao hujifungulia njiani na wegine majumbani hali ambayo ni hatari kwa afya ya mama na mtoto.
Anasema kitu ambacho hua anakifanya kwa wanawake kijijini humo, ni kutoa elimu kwamba wanaposikia dalili za uchungu waanze kujiandaa mapema kuwahi kwenye huduma za afya katika hospitali ya Kolandoto kutokana na kuwa mbali nayo, ili asije kujifungulia jiani na kuhatarisha maisha yake na mtoto.
“Wanawake katika kijiji cha Mwamagunguli mara moja moja hua wanajifungulia njiani na wengine majumbani, lakini hua najitahidi kutoa elimu ya kuwahi kwenye huduma za Afya hasa pale wanaposikia dalili za uchungu, sababu hospitali ni sehemu salama ya kujifungua na watakuwa chini ya uangalizi wa wataalamu”anasema Emmanuel.
MGANGA MKUU WA MANISPAA.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk. Elisha Robert anataja takwimu za vifo vya uzazi, kwamba mwaka 2022 vilitokea 16 na mwaka jana 18, huku pia wakikabiliwa na ukamilishaji wa Maboma ya Zahanati 12 ambayo yalianza kujengwa kwa nguvu za wananchi.
RIPOTI YA UTAFITI.
Kwa mujibu wa Ripoti ya utafiti ya Afya ya uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria ya Mwaka 2022, inasema kwamba huduma za uangalizi wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto.
Ripoti hiyo inasema kwamba asilimia 81 ya watoto waliozaliwa hai kipindi cha miaka miwili kabla ya utafiti,walizaliwa katika Vituo vya kutolea huduma za Afya, ikilinganishwa na asilimia 93 ya watoto waliozaliwa wafu, huku asilimia 85 ya watoto walizaliwa chini ya uangalizi wa wataalamu wa Afya wenye ujuzi.
Ripoti hiyo inasema idadi kubwa ya Vifo vya akina Mama na Watoto hutokea katika saa 48 za kwanza baada ya kujifungua, hivyo basi huduma ya uangalizi wa Mama na Mtoto baada ya kujifungua ni muhimu, ili kutibu changamoto yoyote inayoweza kujitokeza na kuokoa Afya yake na Mtoto.
Aidha, Ripoti inasema kutokana na uboreshaji wa huduma za afya nchini Tanzania, imesaidia kupunguza vifo vya uzazi kutoka 530 kwa kila vizazi 100,000 mwaka 2015/2016, na kupungua hadi kufika vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.
MWENYEKITI WA KIJIJI.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamagunguli Makoye Shindayi, anasema mwaka 2010 walihamasisha wananchi kaunzisha ujenzi wa Zahanati ili wapate huduma za afya karibu hasa wanawake wajawazito na watoto.
Anasema wananchi walihamasika na kuanza ujenzi na kufikisha hatua ya Renta na kuiachia Serikali kumalizia ujenzi huo ili Zahanati iaanze kutoa huduma za Matibabu, lakini hadi sasa imefikisha miaka 14 bado ipo vile vile kwenye Renta.
“Kwenye Zahanati hii wamekuwa wakija viongozi mbalimbali na kutao Ahadi zao za kuikamilisha na kisha kuondoka kimoja na hatujui nini kinaendelea na kutuachia lawama sisi kwa wananchi kwamba tumekula pesa za Zahanati,”anasema Shindayi.
Amewaomba viongozi wa Serikali na Kisiasa, kwamba kama hawana uhakika na ahadi zao juu ya kuikamlisha Zahanati hiyo ni vyema wakae kimya, kuliko kuwa danganya wananchi kama watoto wadogo, na kubainisha kwamba ipo siku wananchi watawachoka na kuwaponda mawe.
“Zahanati hii imekuwa kama maonyesho wamekuwa wakija viongozi mbalimbali akiwamo wana siasa na viongozi wa Serikali, na kuahidi kuikamilisha lakini hakuna kitu, sasa niwambia tu kwamba wananchi wameshawachoka na ahadi zao za uongo,”anaongeza Shindayi.
MWENYEKITI CCM.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mwamagunguli Zephania Ngeleja,a anasema kwamba kusuasua kwa Zahanati hiyo na ahadi hewa za viongozi, inakwenda kuwapa shida kwenye chaguzi zijazo ukiwamo wa mwaka huu wa Serikali za Mitaa na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.
Anasema wananchi wa Kijiji hicho wameanza kukosa imani na Chama Cha Mapinduzi (CCM)sababu viongozi wote kwenye kijiji hicho ni kutoka CCM, na hata viongozi ambao hufika kwenye Zahanati hiyo na kutoa ahadi hewa wanatoka CCM hivyo katika chaguzi zijazo kazi ipo.
“Sisi kwenye Kijiji hiki na Kata nzima hatujawahi kutawaliwa na upinzani miaka yote, lakini kwa changuzi hizi zijazo kazi tunayo hii Zahanati inaweza kutuadhibu naiomba Serikali yangu sikivu chini ya Rais Samia waikamilishe kuijenga ili Chama kiwe Salama,”anaseme Ngeleja.
DIWANI.
Diwani wa Kata ya Kolandoto Mussa Andrew, anasema kwamba Zahanati hiyo mwaka huu ipo tayari kwenye mpango wa ukamilisha, na kuwaomba wananchi wawe wavumilivu.
MKURUGENZI.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze,anasema kwamba mwaka wa fedha 2022/2023 Zahanati hiyo ilitengewa fedha Sh.milioni 60 kutoka mapato ya ndani, lakini hazikupelekwa tena kuikamilisha na fedha hizo kuelekezwa kwenye miradi mingine ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa masoko.
Anasema lakini kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kuu imetoa kiasi cha fedha Sh.milioni 50 ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo ya Mwamagunguli, na kwamba wanacho subili ni mfumo kufunguka na ukishafunguka wanaanza mara moja ujenzi.
“Fedha hizo Sh.milioni 5o kutoka Serikali kuu haziwezi kuikamilisha Zahanati hiyo na kuanza kutoa huduma,tutakacho kifanya kama Halmashauri ni kuitengea tena fungu kutoka Mapato ya ndani ili kamilike na kuanza kuhudumia wananchi,”anasema Kagunze.
KATIBU MKUU WIZARA YA AFYA.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk.Grace Magembe akiwa ziara mkoani Shinyanga Februari 23 mwaka huu, alitoa Maagizo kwa Waganga Wakuu kwamba fedha za miradi ya ujenzi ya Afya ikiwamo ujenzi wa Zahanati wazisimamie na kukamilisha jenzi hizo kwa wakati na kutoa huduma kwa wananchi.
“Haiwezekani Zahanati inajengwa miaka nenda rudi haikamiliki tu, hii siyo sawa Waganga Wakuu ambao mtashindwa kusimamia fedha za ujenzi wa miradi ya Afya tutawachukulia hatua,” anasema Magembe.
Dk.Magembe amewasihi pia wanawake wapende kujifungulia watoto kwenye huduma za kiafya maeneo ambayo ni salama na kupunguza vifo vya Mama na Mtoto vitokanavyo na uzazi.