Viongozi wakikagua uandikishaji wa darasa la Awali
Na Kareny Masasy
MANISPAA ya Shinyanga imeanza msako nyumba kwa nyumba na kwenye vituo vya kulea watoto (daycare centre) kwa watoto ambapo hawajaandikishwa darasa la awali wamefikia umri wa miaka mitano.
Manispaa hiyo mpaka sasa mwezi Marchi uandikishaji umefikia asilimia 85 huku lengo likiwa asilimia 100.
Wakazi wa manispaa ya Shinyanga akiwemo Gidion Juma anasema mtoto wake ana umri wa miaka mitano ameona ampeleke kituo cha kulea watoto kwani shule iko mbali hofu iliyopo kupotea hakuna wa kumfuata.
Pia Rahel Moses anasema ameamua kumpeleka kituo cha kulea watoto sababu yupo mtu wa kushinda naye na analipa pesa kidogo akiwa shuleni atatoka saa nne nyumbani atakuwa pekeyake.
Naye Dolnad Kiula anasema wapo wazazi kwa makusudi hawawapeleki watoto kuanza shule bila sababu za msingi suala la msako kila nyumba ni zuri na watakao bainika wachukuliwe hatua.
“Jamani naona kama viongozi wanahangaika na wazazi kwani wanaokaidi iwepo sheria ndogo kuwa adhibu ili watoto wapate haki yao ya elimu”anasema Kiula.
Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la Invest Children Societies (ICS) mkoa wa Shinyanga Sabrina Majikata anasema umuhimu wa darasa la awali ni kumuandaa mtoto katika ujifunzaji wa maendeleo katika ukuaji wake na kituo cha kulelea watoto ni kucheza kwa kadri ya umri wa mtoto kuanzia miaka miwili hadi minne.
“Mtoto anapozaliwa tu ubongo wake unakuwa umefikia asilimia 25 katika ukuaji wake na anapofikisha umri wa miaka mitano unakuwa kwa asilimia 92 hivyo darasani anaendelea kujifunza zaidi vitu mbalimbali kupitia nyimbo na michezo”anasema Majikata.
Majikata anasema mtoto anatakiwa kuanzishwa darasa la awali akiwa na umri wa miaka mitano na akifikisha umri wa miaka sita aanze darasa la kwanza lakini mzazi analazimisha huko kwenye vituo aanze pia kufundishwa kusoma na kuandika.
“Mzazi unaposhindwa kumpeleka mtoto shule umri unaotakiwa tayari umeanza kumnyima haki yake ya elimu ambayo anatakiwa kuipata akiwa mdogo”anasema Majikata..
Mwenyekiti wa kamati ya shule ya msingi Mwenge Alex Malya anasema shule hiyo inaongoza kuwa na wanafunzi wengi wa darasa la awali changamoto iliyopo ni walimu wa kuwafundisha na madarasa ya kuwaweka ni machache.
“Darasa moja linawanafunzi zaidi ya wanafunzi 100 na Mwalimu ni mmoja hivyo bado kunachangamoto ya uangalizi wa watoto ingawa walimu wamekuwa wakijitahidi kwenye hilo”anasema Malya.
Malya anasema sababu ya wingi wa watoto kwenye shule hiyo iko mjini na kila mzazi anataka kuleta hapa ingawa kata wanazoishi kuna shule mikakati iliyopo mwakani malengo yaliyoweka yatakuwa hayo hayo hawatazidisha watoto.
Sera ya elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inaeleza darasa la awali kuwa Mwalimu mmoja na wanafunzi 25 tu.Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwenge Hemed Hussein anasema Mwitikio wa darasa la awali kwa shule hiyo umekuwa mzuri sababu maoteo kwa mwaka huu yalikuwa wanafunzi 130 na mwezi Januari idadi hiyo ilikuwa imetimia.
“Wazazi waliendelea kuleta watoto wao kutoka maeneo mbalimbali mpaka wamefika wanafunzi 287 wa darasa la awali na darasa moja lina wanafunzi zaidi ya 100”anasema Hussein.
Kaimu ofisa elimu manispaa ya Shinyanga Grace Kuzanza anasema shule ya mwenge wazazi wengi wamekuwa ndiyo kimbilio lao na shule zingine zina wanafunzi wachache.
Kuzanza anasema bado mwitikio wa wazazi katika uandikishaji wa darasa la awali ni mdogo ikiwa Maoteo ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali kwa mwaka 2024 ni wanafunzi 5947 wasichana 3000 na wavulana 2,947
Kuzanza anasema kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi March 2024 wanafunzi walioandikishwa ni 5059 wavulana ni 2457 na wasichana ni 2602 wakiwemo walemavu wasichana watatu na wavulana wanne sawa na asilimia 85 .
“Bado baadhi ya wazazi hawapeleki watoto wao kuanza darasa la awali hata kama umri unaruhusu kuanza anasubiri kumuanzishia moja kwa moja darasa la kwanza”anasema Kuzanza.
Kuzanza anasema uandikishaji wa darasa la awali kwa mwaka jana ulifikia asilimia 105 kwa kufikia mwezi March lakini kwa mwaka huu umefikia asilimia 85 zoezi linalofanyika kuwasaka watoto wote kwenye vituo vya kulea watoto wenye umri wa miaka mitano ili waanze darasa la awali.
Kwa Mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka ya Mwaka 2008 ni kuhakikisha mtoto anaandikishwa shule na kufuatilia maendeleo yao kwa kuwapatia mahitaji yote ya shule.
Katika Programu Jumuishi ya Taifa ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto PJT-MMMAM inaeleza Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye elimu ya awali kuifanya kuwa ya lazima.
Katika sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na maboresho yake ya mwaka 2016 kuwa elimu bila malipo na kujumuisha elimu ya msingi kuzita shule zote kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto wenye umri wa miaka mitano.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464