Na Mwandishi Wetu, Kondoa
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) Imewajengea uwezo wadau mbalimbali kutoka kwenye mashirika, asasi na vikundi vya kijamii kuhusu namna ya kuongeza Ushiriki wa Wanawake ngazi za uongozi na maamuzi Halmashauri ya Wilaya Kondoa Mkoani Dodoma.
Mafunzo haya yanatolewa katika Halmashauri za Wilaya ya Kondoa,Morogoro na Mtwara, kama sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa ‘Mwanamke Ongoza-She Leads’ unaotekelezwa na TGNP kwa ufadhili wa Agakhan Foundation na Ubalozi wa Canada unaolenga kuwezesha wanawake viongozi walioko madarakani kutekeleza majukumu yao vizuri ya kiuongozi na kuongeza ushiriki zaidi wa wanawake kwenye nafasi za uongozi na maamuzi.
Mafunzo hayo yamewanufaisha jumla ya washiriki 30 ambao ni viongozi wa vikundi vya Bodaboda, Dini, vikundi vya kijamii, asasi za kiraia, watu maarufu wenye ushawishi, ambao baada ya mafunzo hayo wataenda kutoa elimu kwenye vikundi vyao na kushawishi wanawake kushiriki kikamilifu kwenye nafasi za maamu.
Mwezeshaji mwenza kutoka TGNP, Ester Wiliam alisema kwamba warsha hiyo inalenga kuongeza uelewa wa dhana za jinsia na uongozi,ubainishaji wa fursa zilizopo katika mifumo ya vyama na kwenye jamii ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi za maamuzi,
Ameongeza kwamba washiriki hao, wamejengewa uwezo kubainisha na kuchambua mifumo kandamizi inayomzuia mwanamke kushiriki katika nafasi za uongozi na ngazi za maamuzi.
“Mafunzo haya yanaenda kuongeza nguvu kwenye Tapo, kwasababu hawa tuliowajengea uwezo wanatoka kwenye makundi mengi, taasisi ndogondogo zinazofanya kazi katika kata ya Haubi, ambapo wakienda kupeleka ujumbe tutakuwa tumewafikia watu wengi sana” alisema Esther