UONGOZI WA SERIKALI KITONGOJI CHA KANGOI, WAWAPELEKA WATOTO SHULE, WALIOZUIWA NA WAZAZI.
Ni alfajiri moja tulivu ya ya mwezi huu wa Machi 2024, shule ya msingi Kanyigo, iliyoko kata ya Kanyigo, wilayani Missenyi, mkoani Kagera, inapokea wageni wawili wa ghafla ambao hawakutarajiwa.
Robert Kolugendo, mwenyekiti wa kitongoji Kangoi, katika kijiji cha Bugombe iliko shule hiyo anawaongoza wageni hao katika ofisi ya mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Wageni hao wawili si wengine bali watoto ambao umri wao umefika kwenda shule lakini hawajasajiliwa kwa kuwa wazazi hawakuwa tayari kuwaandikisha.
Watoto hao mmoja wa kike umri miaka 9, na mdogo wake wa kiume, umri miaka 7 (majina yao yanahifadhiwa), wanaonesha tabasamu lenye matumaini ya kupenda shule, ingawa ndoto zao zingezimwa kabisa kama uongozi wa kitongoji usingechukua hatua ya nguvu kuwalazimisha wazazi watoto hao wapelekwe shule.
Uwezekano wa kisa hiki kutokea maeneo mengine ya Tanzania ni mkubwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutokuwepo elimu ya kutosha kuhusu haki za watoto miongoni mwa wazazi na wanajamii kwa jumla.
Wazazi wa watoto hao, Mawazo Jacob Mgenyi (35) ambaye ni mzaliwa wa wilaya ya Ngara mkoani Kagera, na mkewe Sesilia Monica James (30) mzaliwa wa wilaya ya Geita na mkoa wa Geita, walifika kata ya Kanyigo miaka mitano iliyopita, wakiwa wanahamia hapa na pale wakifanya shughuli za vibarua, na wamehamia kitongojini hapo mwanzoni mwa mwaka huu.
Familia hiyo inao watoto wanne wanaofuatana kwa karibu, ba wale wadogo wawili wa mwisho, wanastahili kuwa wanahudhuria kliniki kwa kigezo cha umri wao, lakini bado hawapelekwi, na uongozi wa kitongoji umeanza kuchukua hatua.stahiki pia.
Majirani wamshauri mama mzazi, ageuka mbogo;
baba haonekani
Baadhi ya majirani wa familia hiyo inayoishi kwenye nyumba
waliyoomba kujihifadhi, wamemweleza mwandishi wa habari hii, jinsi kwa nyakati
tofauti walivyomshauri mama wa watoto hao, kuwaandikisha shule, na pia
kuwapeleka hao watoto wadogo kupata huduma za afya, lakini kila mara wamekuwa
akiwajia juu kwa maneno makali makali kuwa waache kujishughulisha na mambo ya
watoto wake.
Baadhi ya majirani hao, Kasimu Kalyomunda na Fauzia
Mohamed wameelezea kusikitishwa na kauli za mama na kusema kuwa Watoto
hawapati malezi bora kwani kutowafanyiwa usafi wa mwili,
kumesababisha kushambuliwa sana na wadudu funza.
Majirani wameeleza pia kuwa baba wa watoto hao huwa
haonekani mara kwa mara hivyo mzazi pekee ambaye yuko karibu na watoto ni
mama yao na ndio maana wakachukua jukumu la kumkabili mama huyo kumueleza
jukumu la malezi bora ya watoto japo kuwa wanaelewa kuwa Watoto wanahitaji
malezi ya wazazi wote .
"Kwa siku kama nne hivi nilimtafuta baba mzazi wa watoto hao bila kumpata ili nimpe ushauri kuhusu watoto kutokwenda shule, nikamgeukia mama watoto, katika hali ya kushangaza na kuonesha kukata tamaa, alinikasirikia akisema hayo hayamhusu", amesema jirani Kasimu Kalyomunda.
Naye Fauzia Mohamed ambaye ni jirani yao anasema, "Nmemshauri mara kadhaa huyu mama kuwapeleka watoto kliniki, na pia usafi wa mwli wa watoto, lakini akisema ana msongo wa mawazo kutokana na mumewe kutomsaidia katika malezi na matunzo ya familia".
Mama watoto aeleza yanayomsibu,
Wakihojiwa na uongozi wa kitongoji, kwa nini watoto
hawapelekwi shule wala kliniki, na kudhoofika kwa watoto, Sesilia alijitetea
kuwa yeye daima yuko kwenye kibarua cha kuhemea chakula na fedha ya kujikimu,
hivyo asingeweza kukabiliana na michango ya shule, na anaogopa kuwapeleka watoto
kliniki kwani hawana nguo nzuri, maana baba yao amekalia ulevi tu.
Baba wa Watoto
hao, Mawazo, alipoulizwa amekiri udhaifu wa kulewa na
kutoitunza familia yake na ameahidi kubadilika ili kuleta ustawi
katika familia yake.
"Ukweli nilikuwa nimekengeukia mno, pombe zilinitawala kupita kiasi, ila kiukweli kuona nasakwa na uongozi kama digidigi imenifedhehesha sana, Nikajiuliza mara mbilimbili, hivi kwa nini nakuwa hivi. Nimeamua kubadilika na nitajitahidi kuhakikisha naitunza familia na watoto nawatimizia mahitaji yao".
Mwalimu mkuu awapokea watoto hao, aipongeza jamii kwa kuguswa
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Kanyigo, Edwin Mugomba, amekiri kuwapokea na kuwasajili watoto wawili wa miaka 9 na7, ingawa muda wa usajili umekwishapita na huyo mmoja yuko mbele kwa miaka miwili.
Amewashukuru wanajamii walioguswa na watoto hao hadi kuweka msukumo wa kuletwa shuleni.
Kwa mujibu wa kifungu cha 35 (1) cha Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, ilivyofanyiwa marekebisho, kila mtoto anayefikisha miaka saba na hazidi
miaka 13 ni lazima aandikishwe darasa la kwanza.
Hata hivyo Maboresho ya mtaala mpya katika Sera ya elimu, kuanzia
mwaka 2027 mtoto darasa la awali akiwa na miaka 5 ( kama ilivyo sasa) na
darasa la kwanza miaka sita badala ya saba ya sasa.
Lakini bado watoto wengi nchini Tanzania, kama walivyo hao wanaozungumziwa hapo juu bado hawako shuleni kutokana na umaskini, miundombinu , kutelekezwa na wazazii nk
Pamoja na uwekezaji mkubwa wa serikali na wadau wa mendeleo katika sekta ya elimu, serikali inajitahidi kupunguza tatizo hili kadri inavyowezekana ili walengwa wafaidike na kuleta tija kwa taifa miaka ya baadaye.
Miongoni mwa hatua chanya zinazochukuliwa na serikali kwa
kushirikiana na wadau, ni kuweka sheria na miongozo inayosimamiwa
na kutekelezwa, kama vile Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na
Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJTMMMAM) iliyozinduliwa mwaka 2021/22
ikitarajiwa kukamilika mwaka 2025/26.
Utekelezaji PJT-MMMAM unawaleta pamoja wadau wote wa elimu,
afya, lishe, ulinzi na malezi yenye kuitikia mahitaji ya mtoto, ili kuhakikisha
watoto wote kuanzia miaka 0 hadi 8 wanakua kwa utimilifu wao ili waweze
kutimiza ndoto zao. Kipengele vipengele vikuu vitano vinayo leta ukuaji
timilifu kwa Watoto. Na kupitia PJT-MMMAM jamii kwa ujumla inawajibika kwenye
ulezi wa watoto na wanajamii wa Kanyigo wameonyesha mfano bora.
Baadhi ya watoto kutokana na sababu mbalimbali kutokana na kutowajibika,mifarakano katika ndoa, umaskini, miundombinu , kutelekezwa na wazazi nk hukosa fursa ya kuandikishwa shule kujumuika na wenzo kama hawa, shule ya msingi mojawapo wilayani Missenyi (picha kwa hisani ya mdau wa maendeleo ya elimu