Na Baraka Messa, Songwe.
UKOSEFU
wa zana za kufundishia katika elimu ya madarasa ya awali na darasa la
kwanza katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kumelisukuma shirika lisilo
la kiserikali la Save the Children kutoa mafunzo kwa walimu 47
wanaofundisha elimu ya awali ili kuongeza maarifa ufundushaji.
Akiongea
na mwandishi wa BLOG mratibu wa mradi jumuishi kutoka shirika la Save the
Children John Tobongo amesema lengo kubwa la mafunzo hayo kwa walimu ni
kuboresha msingi wa watoto wa elimu ya awali ili kujifunza vizuri kwa
vitendo kupitia vitu mbalimbali vinavyowazunguka.
Alisema
wameanza na shule 47 ambazo zimetoa mwalimu mmoja mmoja wa elimu ya
awali kila shule kupata mafunzo hayo , ambayo wanaamini yataboresha
ujifunzaji wa watoto kupitia kuona na kugusa zana wanazofundishiwa.
"
Tumeanzisha mafunzo haya baada ya kubaini kuwa kuna upungufu wa zana za
kufundishia katika madarasa ya elimu ya awali, walimu kukosa ujuzi wa
kutengeneza zana za kufundishia,
Lakini pia
tumebaini kuwa mtoto anajifunza vizuri zaidi pindi mwalimu anapokuwa na
nyenzo za kutosha za kufundishia ambazo hupatikana kulingana na
Mazingira yanayowazunguka" alisema Tobongo.
Mwezeshaji
wa mafunzo ya kutengeneza zana na namna ya kutuzitumia Adelina Kamara
alisema watoto wa elimu ya awali katika ujifunzaji wao huhitaji darasa
linalongea , ambalo husheheni zana mbalimbali za kujifunzia.
Kuhusu
namna ya kutengeneza zana alisema wamewafundisha walimu kutumia vitu
vinavyo wazunguka kama vile, makopo, vijiti, magunzi ya mahindi , mawe
na maboksi mbalimbali ambavyo hutumia gharama ndogo.
"Mfano
rangi ya shilingi 200 au 500 pekee unaweza kutengeneza zana nyingi
ambazo zitakuwa na rangi mbalimbali mbazo huwavutia watoto wakati wa
kujifunza " alisema Adelina.
Alitaja
faida ya zana za kufundishia kuwa ni ;pamoja na uhusiano wa mwalimu na
mwanafunzi kuongezeka, mwanafunzi kujifunza muda wote hata kama mwalimu
hayupo darasani na ujasiri na kujiamini huongezeka kwa watoto.
Mwalimu
wa elimu ya awali kutoka shule ya Msingi Oswe Judith Kamwela alisema
wamejifunza namna ya kutengeneza zana kwa gharama ndogo tofauti na awali
ambapo walikuwa wanashindwa kutengeneza kwa kuhofia gharama za vifaa
vya kutengenezea zana.
Aliongeza
kuwa pia amejifunza namna ya kutengeneza zana kwa kutumia rangi
mbalimbali zinazopendezesha darasa ambazo ni rafiki kwa watoto
kujifunza.
Kwa
upande wake Mratibu wa shule za Msingi na elimu ya awali mkoa wa Songwe
Mtinga Maleya alisema toka serikali kupitia sera ya elimu ya mwaka 2014
kuanzishwa madarasa ya awali yenye miundo mbinu mizuri katika shule zote
za Msingi kumepunguza changamoto za watoto kutokujua kusoma na
kuandika kwa kiasi kikubwa.
Alisema
walimu waliopata mafunzo ya namna ya kutengeneza zana za kufundishia
watakuwa mabalozi kwa walimu wengine katika shule zao.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464