WANANCHI WAFUNGA BARABARA BAADA YA MTOTO KUGONGWA NA GARI GEITA



 Usalama wa  watoto katika kuvuka barabara mkoani Geita.

SALUM Maige,Geita

Moja ya changamoto zinazowakabili wanafunzi wa darasa la awali,la kwanza na la pili wakati wa kwenda shule ni ajali za barabarani kutokana na umri wao mdogo wa kutotambua ni wakati gani sahihi wa kuvuka barabara kwenda upande wa pili.

Hali hiyo imesababisha baadhi yao kupoteza maisha,kujeruhiwa na wengine kupata ulemavu wa kudumu katika kipindi ambacho wanatafuta elimu kwa manufaa ya maisha yao ya baadae,familia na taifa kwa ujumla.

Ajali hizo,zimesababisha wakazi wa mtaa wa Nyantorotoro A mjini Geita kufunga barabara kuu ya kutoka Geita mjini kuelekea Katoro ili kushinikiza serikali kuweka tuta na alama za barabarani katika eneo hilo baada ya mtoto wa darasa la kwanza kugongwa na gari wakati akivuka barabara hiyo.

Mtoto huyo(jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka saba aligongwa gari ambalo ni lori la mchanga wakati akivuka barabara hiyo akitokea shule ya msingi Tumaini kuelekea nyumbani kwao.


Tukio la mtoto huyo kugongwa limetokea machi 25, mwaka huu majira ya saa tano asubuhi na kwamba wakati akivuka barabara aligongwa na lori la mchanga na kusababishiwa majeraha, ambapo alikimbizwa na kulazwa katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Geita.

Baada ya tukio hilo kutokea wananchi waliamua kuzuia magari kwa muda ikiwa ni hatua ya kuishinikiza serikali kuweka alama na tuta kwenye barabara hiyo ili kuepusha ajali ambazo zimekuwa zikitokea mara kwa mara.

Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo wamesema, katika kipindi cha kuanzia januari hadi machi watoto watatu wamepoteza maisha kwa kugongwa na gari wakati wakivuka barabara kutoka ama kwenda shule ya msingi Tumaini.

“Watu wamekuwa na hasila kwa sababu kila mwezi watoto wanagongwa hapa, haiwezekani watoto wetu kuendelea kupoteza maisha kwa sababu tu ya kugongwa na gari,tunaomba serikali iweke tuta au alama za barabarani” ,anasema Pendo Julias.

Kufuati eneo hilo kuwa janga kwa watoto kugongwa mara kwa mara, mmoja wa wakazi hao Juma Athuman yeye amewaachisha shule watoto wake wawili baada ya mwanae mmoja kufariki siku chache zilizopita kwa kugongwa na gari katika eneo hilo wakati akivuka barabara hiyo kwenda nyumbani.

“Nilikuwa na watoto watatu mmoja aligongwa hapahapa, hawa wawili nimekataa wanangu wasisome kabisa, niliumia sana ,hivyo serikali inatakiwa kusikia kilio chetu sisi wananchi ,tunapoteza watoto kila wakati, mimi sisomeshi tena watoto” anasema Athuman.

Akizungumza kwa masikitiko mkazi mwingine Semen Meleka ameiomba serikali kutofumbia macho tatizo hilo ambalo limekuwa kero kwa wananchi kuendelea kupoteza watoto wao katika kipindi ambacho wanatafuta elimu.

“Watuwekee zebra hapa ,ikiwezekana wawe wana kuja kusimama hapa maaskari ili kuvusha watoto wetu haiwezekani kuwa tunazika kila wakati watoto ni jambo ambalo sisi wazazi linatuumiza sana” anasema Semeni.

Meneja wa wakala wa barabara mkoa wa Geita, mhandisi Ezra Magogo amefika eneo la tukio na kuwasihi wananchi hao kufungua barabara hiyo na kwamba serikali inafanyia kazi maombi yao ya kuweka alama za barabarani na tuta.

“Poleni sana wananchi wa Nyantorotoro kwa ajali hii iliyotokea leo, maombi yenu nimeyachukua na niwaahidi eneo hili tutaweka alama za barabarani likiwemo tuta ili kusitokee ajali tena ambazo zinagharimu maisha ya watoto wetu

“Hivyo nawaomba tuache vyombo vya usafiri viendelee na safari wakati serikali ikifanya jitihada za kutimiza maombi yenu,niwaahidi jambo hili tutalifanya kwa haraka zaidi, hivyo tuondokeni barabarani ,nawaomba sana ndugu zangu wananchi” alisema mhandisi Magogo.

Baada ya kauli hiyo wananchi walifungua barabara hiyo na kuruhusu vyombo vya moto kuendelea na safari.

Aidha,akithibitisha kumpokea majeruhi huyo mganga mfawidhi wa hospitali hiyo Dkt.Thomas Mafulu amesema,mtoto huyo alifikishwa hospitalini hapo akiwa na hali mbaya baada ya kupata majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Ameumia zaidi kichwani ambako kuna michubuko, mikono na miguu, lakini toka ameanza kupata huduma za kitabibu hali yake inaendelea vizuri,kwa sababu wakati analetwa alikuwa hawezi hata kuongea alikuwa hana fahamu kabisa,tunaendelea kumhudumia” anasema Dkt.Mafulu.

Musa Edward mkazi wa mtaa huo amesema, wananchi wa eneo hilo wamelazimika kuchangishana fedha kwa ajili ya kujenga shule mpya ili kuwanusuru watoto wao na ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.

“Hadi sasa michango inaendelea wananchi tunaedelea kuchangia tunapenda tuwe na shule yetu ili watoto wa eneo hili wasivuke kwenda ng’ambo ya pili kutafuta elimu,na mwitikio wa wananchi kuchangia ni mkubwa mno” anasema Edward.

Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) ni kwamba watu 1,031 wamefariki dunia na watu 646 wamejeruhiwa kutokana na matukio 1,933 ya ajali za barabarani katika kipindi cha kuanzia januari hadi disemba 2020 nchini Tanzania.

Mkoani Geita katika  kipindi kama hicho cha januari hadi disemba, 2020 matukio ya ajali za barabarani ni 71 yaliyosababisha vifo 54 na majeruhi 12.

Akizungumzia kuthibiti ajali za barabarani, kamanda wa polisi mkoa wa Geita Safia Jongo amesema, jeshi la polisi limefanikiwa kudhibiti ajali kwa kukamata makosa 8,124 ya usalama barabarani, ambapo baadhi ya madereva walitozwa faini na wane kufikishwa mahakamani.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464