WATANZANIA WAHIMIZWA KUTEMBELEA VIVUTIO VYA UTALII KUELEKEA KILELE CHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI

 


Na  John I. Bera

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imewataka Watanzania ikiwemo Wanawake  kusherekea kilele cha Siku ya Wanawake Duniani kwa kutembelea Vivutio vya Utalii vilivyopo nchini.

Kauli hiyo imetolewa leo Alhamisi Machi 7, 2024  na  Afisa Utalii, Maria Nyamsekela akiwa  katika Maonesho ya Wiki ya  Wanawake  yanayofanyika kwa muda wa siku tano kuanzia leo  kwenye Viwanja vya Mashujaa Jijini Dodoma.

Amesema Maadhimisho hayo yatumike kwa  Watanzania  ikiwemo Wanawake kwa kutembelea Vivutio vya Utaliii nchini ili waweze kujionea jinsi Tanzania ilivyobarikiwa kuwa na vivutio vya kila aina mathalan wanyamapori, fukwe, misitu, utamaduni na milima huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni njia mojawapo ya kuchangia uchumi wa nchi na kukuza Utalii wa ndani.  

Ameongeza kuwa, Tanzania imejaliwa kuwa na maeneo mengi yenye Vivutio vya Utalii huku akitaja maeneo kama Hifadhi  ya Eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa  Serengeti, Hifadhi ya Nyuki  Agondi, Pori la Akiba Mkungunero kuwa ni mfano wa maeneo machache  mazuri ambayo Watanzania ikiwemo wanawake wanaweza kwenda kufanya Utalii wa ndani.

“Tanzania ni nchi iliyojaliwa vivutio mblalimbali, Tuna Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, Hifadhi ya Taifa  Serengeti,  Hifadhi ya Nyuki Agondi, Pori la Akiba Mkungunero na maeneo mengi ya Malikale, Tunachotakiwa kufanya Siku hii ya Kilele cha Siku ya Wanawake ni kwenda kutembelea Vivutio vyetu kwa wingi na hapo tutakuwa tumechangia uchumi wa nchi yetu.’’ amesema Nyamsekela.

Sambamba na hayo, amewataka Watanzania wote kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii lilipo katika maonesho hayo ili waweze kupata maelezo ya namna ya kufika kwenye maeneo mbalimbali ya Vivutio hivyo vya Utalii

“Nitoe rai kwa Watanzania wote ikiwemo wakazi wa Dodoma kutembelea Banda letu la Wizara ya Maliasili na Utalii ili waweze kujionea Vivutio mbalimbali vya Utalii vilivyopo na pia waweze kupata maelezo ya namna gani ya kufika kwenye vivutio vyetu vya utalii hapa nchini’’ ,amesema

Naye, Juma Salim akitembelea Banda la Wizara katika maonesho hayo, ameipongeza Wizara kwa kuendelea kutumia njia mbalimbali ikiwemo Maonesho mbalimbali nchini kutangaza Utalii wa ndani

Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake  Duniani hufanyika kila mwaka  Machi 8 ambapo kwa mwaka huu Kifaita yatafanyika Jijini Dodoma  katika Wilaya ya Chamwino  yakiwa na kauli mbiu  isemayo ‘’ Wekeza kwa Wanawake  kuharakisha  Maendeleo ya Taifa na Ustawi kwa Jamii’’

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464