TANROADS SHINYANGA YAFANYA MALIPO YA MAPUNJO YA FIDIA KWA WANANCHI WALIOPISHA UJENZI WA UWANJA WA NDEGE SHINYANGA.
Na. Paul Kasembo, SHY RS.
MENEJA TANROADS Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Joel Mwambungu ameongoza timu ya wataalam kufanya malipo ya mapunjo wa fidia kwa wananchi wa eneo la Ibadakuli waliopisha utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Uwanja wa Ndege Shinyanga huku akiwaomba kuendelea kuwa wazalendo wa kulinda mali na uwanja huu wa ndege ambao kimsingi ni mali yao.
Malipo haya kwa wananchi yaliyofanyika kwa njia ya Hundi yamefanyika katika Ofisi ya Kata ya Ibadakuli hapa Manispaa ya Shinyanga huku yakishuhudiwa na viongozi mbalimbali akiwemo Eng. Eugene Soka aliyemuwakilisha Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Prof. Siza Tumbo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Shinyanga Ndg. Leo Komber, uongozi wa Serikali ya Tarafa, Kata na Mtaa huku wananchi wakionesha furaha zaidi kuwa na hatma ya jambo lililochukua muda kiasi katika uhitimishaji ambalo leo limefikia mwisho wake.
"Ndugu zangu wananchi wa Ibadakuli, kwa dhati kabisa na kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TANROADS Mhandisi Mohamed Besta ninamshukuru sana Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha malipo haya ya mapunjo ya fidia kwenu ili kupisha ujenzi wa uwanja wa ndege Shinyanga ambao kimsingi ni maendeleo na mali yenu wananchi," amesema Mha. Joel.
"Pamoja na shukrani kwenu kwa uvumilivu wenu mkubwa wakati mkisubiria malipo haya ya mapunjo, niwaombe muendelee kuwa walinzi wa miundombinu yote ya uwanja huu wa ndege na mali zote kwakuwa vyote hivi ni mali yenu hivyo ni wajibu wetu sote kuwa sehemu ya umiliki na ulinzi," amesisitiza Mha. Joel.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Ibadakuli Mhe.Msabila Malale amemshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha uhai mpaka kufikia leo, amemshukuru pia Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha kufikia mwisho wa kero kubwa ya wananchi wa Ibadakuli huku akiwapongeza TANROADS Mkoa wa Shinyanga kwa utekelezaji wa tukio hili kwa wananchi wake huku akiwasihi kwenda kutumia fedha hizo katika kujiletea maendeleo yao.