Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa kiasi cha Sh.Milioni 444 kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi 97 waliotoa maeneo yao kupisha Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga.
Mradi unaofadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Ufaransa(AFD) kwa Ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wananchi hao wanatoka katika vijiji sita vikiwemo Mwagala, Kolandoto na Ihapa vilivyopo Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, pamoja na vijiji vya Kituli, Didia na Mwamakalanga vya Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.
wananchi hao wameanza kusaini majedwali ya uthamini ili fedha zao ziweze kuingizwa katika akaunti zao za benki.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Afisa Mazingira kutoka Wizara ya Maji Moses Mgalla, amesema ulipaji wa fidia umefuata taratibu zote za kisheria ikiwemo ushirikishwaji wa wancnhi kuanzia hatua ya kwanza ya kutoa elimu.
kuanisha maeneo, kufanya udhamini na uhakiki na hatimaye kulipa fidia. MbaIi na ushirikishwaji wa wananchi amesema pia viongozi wa Serikali ngazi za Mkoa, Wilaya, Halmashauri na Serikali za Mitaa walishirikishwa katika hatua zote.
Kafula Ngaiwa, mkazi wa Kijiji cha Ihapa na miongoni mwa wanufaika wa fidia, ameishukuru Serikali kwa kuwafidia kwa wakati bila kuchelewesha malipo na kuwapeleka mradi katika kijiji chao.
Aidha ameomba Mamlaka izingatie wananchi wa kijiji hicho waweze kunufaika na ujenzi wa mradi huo kwa kuwapa vijana ajira.
Naye Paul Sitta mkazi wa Matanda Manispaa ya Shinyanga na mnufaika wa fidia hiyo, amesema ameridhika na fidia iliyotolewa na kwamba anabariki mradi huo kutekelezwa katika maeneo waliyoyaachia.
“Naishukuru Serikali kwa kuweza kutukamilishia zoezi la kulipa fidia ya ardhi iliyochukuliwa kwaajili ya matumizi ya Serikali na taratibu zote zimefuatwa na wananchi hawajapuuzwa kwani watu wa SHUWASA na wizarani wameweza kuelekeza vizuri na wananchi wameelewa,” amesema Sitta.
Mradi wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga, unagharimu kiasi cha Euro Milioni 76 sawa na takribani Sh Bilioni 200 na unahusisha ujenzi wa mtandao wa majisafi, ujenzi wa mitambo minne ya kuchakata tope kinyesi,
ukarabati wa mtambo wa kutibu majisafi na kuijengea uwezo Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA)
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464