Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Kassim Majaliwa ameipongeza Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa namna inavyodhibiti biashara ya dawa za kulevya nchini.
Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo Aprili 9, 2024 wakati wa hafla ya Futari aliyoiandaa kwa ajili ya watumishi wa ofisi yake na taasisi zake, Mlimwa jijini Dodoma.
"Upande wa Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya tunaye hapa, Bwana Lyimo alishaanza kazi, amefanya kazi nzuri sana.
Ameendesha operesheni,amekamata madawa, zaidi ya madawa tuliyowahi kuyakusanya miaka yote, ameenda shambani, mpaka kule Arusha akavuna cha Arusha chote (bangi) hongera sana", amesema Waziri Mkuu Majaliwa.
Ameongeza kuwa, mpaka sasa Mamlaka ya Kudhibiti imepanua wigo wake kiutendaji hadi kufikia ngazi ya kanda ambapo tayari watumishi wako katika kanda hizo kutekeleza majukumu yao.
Amesema; "Lakini pia amefanya maboresho kwenye sekta yake, tulipotoka tulikuwa tunaboresha, lakini Kamishna Jenerali ameboresha zaidi kwamba ofisi yake haiishi makao makuu ya nchi tu, ameshusha kwenye kanda na tayari wakurugenzi wameshaenda kwenye kanda".
Aidha waziri mkuu amesisitiza kuwa utekelezaji wa shughuli za Mamlaka utafanikiwa sana kwa sababu kamishna jenerali Lyimo ameshusha watu ambao watasimamia operesheni zote, mipango yote ya kudhibiti na kukamata wazalishaji, wasafirishaji, watumiaji na wafanyabiashara.