MKOA WA GEITA WAZIDI KUZIKABILI CHANGAMOTO ZINAZOHATARISHA USALAMA WA WATOTO WADOGO



Mmoja wa watoa huduma akimsaidia Mjamzito.
Na Salum Maige,Geita
 
MOJA ya changamoto ama sababu inayohatarisha usalama wa watoto wadogo kabla,mara ama baada tu ya kuzaliwa ni ukosefu ama uduni wa huduma za afya kwa mama pamoja na mtoto,uduni wa miundombinu hususani katika maeneo ya pembezoni mwa nchini.

 Katika kuhakikisha usalama wa mtoto kabla na baada ya kuzaliwa,serikali ya Tanzania imekuwa ikiongeza bajeti kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha huduma za Afya mijini na vijijini ikiwa na lengo la kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto kabla na baada ya kuzaliwa.

 Mkoa wa Geita unatekeleza mpango wa kuimarisha vituo vyake vya Afya ili kukabiliana na hatari ya vifo vya watoto kabla na baada ya kuzaliwa kwa kuviimarisha baadhi ya vituo vya afya vinavyotumiwa na wakazi wa eneo hilo ili kupounguza vifo vya watoto vinavyosababishwa na huduma dhaifu za Afya au ukosekanaji kabisa wa huduma za Afya.

 Moja ya uwekezaji kwenye sekta ya Afya Mkoani Geita ni maboresho ya kituo cha Afya cha Nyankumbu kilichopo halmashauri ya mji wa Geita ambacho maboresho yake yamehamasish awanawake wajawazito wengi kuacha kujifungulia nyumbani na hivyo kuongeza usalama wa mtoto wakati na kabla baadaya kuzaliwa.

 Uwekezaji huo wa serikali ni moja ya mikakati yake ya kuhakikisha inapunguza vifo vya watoto ambapo kwa mujibu wa wizaraya afya kati ya mwaka 2010 na 2015 kiwango cha vifo vya watoto wachanga vimepungua kutoka 40 hadi 25 kwa vizazi hai 1,000.

 Kwa mujibu wa taarifa za kituo hicho kwa mwaka huu wa 2024 akina mama wajawazito wapatao 280 hadi 300 hujifungua kila  mwezi kwenye katika kituo hicho idadi hiyo imeongezeka kutoka wajawazito 245 waliokuwa wanajifungua kila mwezi kwa mwaka wa 2023 baada ya serikali kufanya ukarabati na kujenga wa jengo jipya la wodi ya wazazi.

 Kituo hicho kinahudumia zaidi ya wakazi 21,152 kutoka kwenye mitaa saba na vijiji vine vilivyopo kwenye kata za Nyanguku,Mtakuja,Kalangalala na Buhalahala.

 Maeneo yaliyoboreshwa ni pamoja na kukamilika kwa ujenzi wa wodi mpya ya wazazi yenye vitanda vya kisasa,jengo la upasuaji na vifaa vyake,na jengo jipya la kliniki ya mama na mtoto.

 Wakizungumza na mwandishi wa blogi hii,baadhi ya wazazi wanasema zamani kabla ya maboresho hayo walikuwa wanalala kitanda kimoja watu wawili na watoto wao lakini kwasasa kila mzazi anatumia kitanda chake.

 Mmoja wa wazazi hao Irene Mashauri mkazi wa m taa wa Nyantorotoro B mjini Geita amesema,  kabla ya kuwepo kwa wodi hiyo baadhi ya akina mama walikuwa na mwitikio mdogo wa kufika katika kituo hicho kujifungua kutokana na mazingira kutokuwa mazuri.

 “Wazazi wengi walikuwa wanajifungulia nyumbani,au wengine njiani wakati wakitafuta huduma mbali mfano kwenda hospitali ya mji wa Geita au hospitali ya rufaa ya mkoa ambako ni mbali,lakini kwa sasa hivi tuna shukuru huduma ni nzuri sana”anasema Irene.

 Naye Salome Deus mkazi wa kijiji cha Nyanguku anasema, tangu amefika akiwa anajisikia uchungu hadi kujifungua amepata huduma nzuri kutoka kwa watoa huduma huku akifurahishwa na vitanda vya kisasa vilivyowekwa katika wodi hiyo.

 “Nishauri tu wanawake wenzangu waache tabia ya kujifungulia nyumbani kwani ikitokea ukatokwa na damu nyingi ni kuhatarisha uhai wako na uhai wa mtoto,wafike hospitali hasa kituo cha Nyankumbu ambacho kwa sasa kimeboreshwa”, anasema Salome.

 Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Bombambili Samson Lushinge amesema, kupitia mikutano ya hadhara huwa wanatoa elimu ya kuhamasisha akina mama kwenda kujifungua hospitali.

 “Tunao pia watoa huduma ngazi ya jamii wawili kweye mtaa wetu ambao huhakikisha kila mama mjamzito anahudhuria kliniki na kwenda kujifungulia kwenye kituo cha afya ili kupunguza vifo vya mama na mtoto”, anasema Lushinge.

Mjumbe wa mkutano mkuu taifa chama cha mapinduzi CCM Kilosubi Magambo amewashauri akina mama kuacha tabia ya kujifungulia nyumbani au kwa waganga wa kienyeji hali ambayo inahatarisha uhai wa maisha yao pamoja na kichanga kilichoko tumboni.

 “Huduma kwa kweli ni nzuri sana hata wagonjwa na wazazi wana kili kwamba upatikanaji wa huduma uko vizuri,sasa basi sisi kama viongozi wa chama tunaomba sana jamii ibadilike itumie kituo hiki kupata huduma za afya,zikiwemoza upasuaji na kujifungua”, anasema Magambo.

 Mganga mfawidhi wa kituo hicho Dkt.Irene Temba amesema, kukamilika kwa jengo la wodi ya wazazi na upasuaji kumesaidia kuboresha huduma kwa jamii na kupunguza idadi ya wajawazito kujifungulia nyumbani.

Dkt.Temba anasema, zamani idadi ya wajawazito kujifungulia nyumbani kwa mwezi ilikuwa inafika hadi 80,lakini baadaya maboresho hayo pamoja uhamasishaji wa majengo mapya wanawake wengi wanafika kujifungua na hivyo idadi imepungua kutoka wanawake 80 hadi  4 kwa mwezi wanaojingulia nyumbani.

 Pia  kiongozi huyo anasema, wajawazito wanaolazwa kila mwezi ni 1,054  akina mama wanaojifungua ni 280 hadi 300 kila mwezi huku kwa kipindi kama hicho watoto chini ya umri wa miaka mitano 3,255 hulazwa katika kituo hicho.

 Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa ya programu jumuishi ya taifa ya malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) iliyozinduliwa disemba 2021 inaonyesha kuongezeka kwa uwiano wa vifo vya akina mama wajawazito kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 ikilinganishwa na vifo 454 kwa mwaka 2010 kwa kila vizazi hai 100,000

 

 

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464