MSHITAKIWA KESI YA MAUAJI YA MTOTO WA MWEZI MMOJA AKUTWA NA KESI YA KUJIBU




Na Salum Maige,Geita

Mahakama kuu Kanda ya Geita imemkuta na kesi ya kujibu mshitakiwa Shemas Juma mkazi wa kijiji na kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe mkoani humo anayeshitakiwa kwa kosa la kumuua mwanae Anna mwenye umri wa mwezi mmoja kwa madai ya kwamba mtoto huyo alizaliwa akiwa hajafanana naye.

 Akisomewa hati ya mashitaka ya awali na kupokelewa na Jaji mfawidhi wa mahakama kuu kanda ya Geita Mh.Kelvin Mhina,mshitakiwa huyo anakabiliwa na kosa la kuua mwanae kwa makusudi kinyume na kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2022.

 Kesi hiyo Na.53 ya mwaka 2022 ilianza kusikilizwa aprili 15 na 16 ,mwaka huu kwa upande wa mashahidi wa jamhuri kutoa ushahidi wao wakiongozwa na mawakili wa serikali Godfrey Odopoy na Kabula Benjamini.

 Mashahidi wote wanane wamekamilisha kutoa ushahidi wao katika kesi hiyo pamoja na kukabidhi vielelezo viwili kikiwemo cha uchunguzi wa daktari na maelezo ya upande wa ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai.

 Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Oktoba 19,2021 huko katika kata ya Masumbwe wilayani Mbogwe mkoani Geita kwa kuumua mwanae kwa kumnyonga kisha mwili wake kuutupa ndani ya shimo la maji.

 Akitoa ushahidi wake Casmiry Lubango ambae ni daktari kituo cha afya Masumbwe aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu ameieleza Mahakama kuwa mtoto Anna Shemas alikufa kwa kukosa hewa kotokana na kunyongwa na kubanwa pumzi.

 Akiongozwa na Wakili wa upande wa Jamhuri Godfrey Adopoy shahidi huyo amesema, mwili wa mtoto huyo mchanga ulikutwa kwenye shimo la maji ukiwa unatoa harufu na tayari ulikua umevimba.

 “Mwili ulikutwa kwenye shimo lililojaa maji ukiwa umeshaharibika unatoa harufu na ulikuwa umevimba, haukua na jeraha na viungo vyote vilikuwepo na baada ya kumfanyia uchunguzi mwili ulipelekwa Mochwari kutokana na kukosa ndugu na baada ya siku 14 ulizikwa”amesema Dkt.Lubango.

 Baaada ya kutoa ushahidi huo,shahidi huyo alikabidhi taarifa ya uchunguzi wa mwili kama kielelezo jambo lililoridhiwa na mahakama hiyo na kupokelewa kama ikiwa ni kielelezo namba moja kwa upande wa mashtaka.

 Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo Gaudencia Aloyce(57) mkazi wa mtaa wa Lugito wilayani Mbogwe ameieleza mahakama kuwa oktoba 19 saa mbili asubuhi akitoka kwenye jumuiya alifuatwa na dada mmoja aitwae Anna akimueleza kuna mtoto kwenye shimo la maji lililopo karibu na ofisi za chadema.

 Ameongeza kuwa alipofika kwenye shimo alikuwa mwili wa mtoto huyo ukielea juu ya maji na ndipo alilazimika kutoa taarifa kwenye uongozi na polisi ambao walifika na kuuchukua mwili huo.

 Shahidi wa tatu Monika Kisusi akiongozwa na wakili wa Jamhuri Kabula Benjamin ameieleza mahakama kuwa ogasti 2021 wakiwa nyumbani aliitwa na Shemas Anold Juma ambaye ni mtuhumiwa na kumuomba amsindikize mkewe  kwenda hospitali kwa kuwa anaumwa uchungu.

 Baada ya kufika kituo cha afya Masumbwe mke wa Shemas aitwae Kulwa alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida na hivyo kufanyiwa upasuaji na kupata mtoto wa kike lakini kidonda kilibaki kikitoa usaha na baada ya wiki moja alirudi nyumbani.

 Bila kutaja tarehe amedai siku moja mtoto alikua akilia sana usiku ndipo Shemas(baba wa mtoto) alidai anampeleka hospitali kwa kuwa kitovu kinatoa usaha na baadae alirudi akidai mtoto amepelekwa Bugando kwa kutumia gari la wagonjwa.

 “Kwa kuwa yule mtoto alikua mdogo sana tulimuuliza amemwacha vipi wakati ananyonya akadai mama yake mzazi ameenda nae na kesho yake asubuhi alimchukua mkewe akidai wanaenda kumfuata mtoto hospitali na hawakurudi tena”.

 Alidai baada ya siku chache mshitakiwa alirudi nyumbani kuchukua vyombo vyake na akidai amehamia Kahama mkoani Shinyanga.

 Shahidi namba 8 katika kesi hiyo askari Na.H8250 Koplo Alex kutoka Ofisi ya upelelezi wa makosa ya jinai wilaya ya Mbogwe ameieleza mahakama hiyo kuwa mshitakiwa alifanya mauaji hayo baada ya madai mtoto kuzaliwa akiwa hajafanana naye.

 Koplo Alex ameleeza kuwa,  yeye ndiye aliyemuhoji mshitakiwa ambapo katika mahojiano hayo alikiri kufanya mauaji hayo na kuwasilisha maelezo ya onyo ya mshitakiwa katika mahakama hiyo ikiwa ni kielelezi kwa upande wa mashitka.

Imelezwa kuwa wakati mama mzazi wa mtoto huyo alipoelekea Hospitali mshitakiwa alimchukua mtoto huyo na kuondoa naye kwa madai anampeleka hospitali na alipofika njiani akiwa na bodaboda alisimama kisha kumziba mdomo na pua kisha kumtupa kwenye shimo la maji huku akimziba mdomo na pua.

Hata hivyo aliporejea nyumbani na kuulizwa na mkewe mama wa mtoto huyo Kulwa James mshitakiwa alidai kwamba mtoto amepelekwa Hospital ya Bugando na bibi yake.

Shahidi namba 5 ambaye ni mama mzazi wa mtoto huyo ameieleza mahakama hiyo kuwa, alipomkosa mtoto huyo alianza kulia na majirani kukusanyika,ndipo ilibidi wasafiri mumewe ambaye ni mshitakiwa kwenda Bugando Jijini Mwanza.

Walipofika Mwanza kumuona mtoto mwanaume huyo hakumpeleka Bugando hospital na badala yake waliishi nyumba ya kulala wageni kwa siku tatu na baadaye alimweleza mkewe kwamba mtoto amepelekwa hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaamu.

Hata hivyo wakiwa safarini kurejea nyumbani Masumbwe mshitakiwa alimweleza mkewe wasiende nyumbani kwao kwa kuwa majirani ndiyo waliomloga mtoto huyo na hata yeye mama mzazi akirejea katika nyumba hiyo kidonda chache cha upasuaji hakitapona.

Baada ya miezi miwili mshitakiwa alienda Kahama Shinyanga na siku chache Mama wa mtoto huyo alienda kwa mjomba wa mshitakiwa na alipofika alipewa pole ya msiba kitendo ambacho kilimshitua na alipohoji alielezwa kwamba muwewe ambaye ni mshitakiwa kwa sasa alipiga simu na kuwaeleza kuwa mtoto huyo amefariki.

Baada ya kufunga ushahidi upande wa jamhuri mahakama hiyo imebaini kuwa mshitakiwa ana kesi ya kujibu na alipotakiwa kujitetea amedai kuwa yeye hajawai kuoa wala kuwa na mtoto na kwamba yeye alikamatwa kama mhamiaji haramu akiwa mnadani na kufikishwa mahakamani na kusomewa shitaka la mauaji

Hata hivyo mahakama hiyo mbele ya jaji mfawidhi wa mahakama hiyo Mh.Mhina imefunga kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili upande wa jamhuri na upande wa mshitakiwa na kuahirisha kesi hiyo hadi Mei 30,2024 mahakama hiyo  itakapoketi tena kwa ajili ya kutoa hukumu.

 

 




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464