MWITIKIO WA WANANCHI VITUO VYA AFYA KWAPUNGUZA VIFO VYA MAMA NA MTOTO SONGWE


 Baadhi ya akina mama wakiwa na watoto wao kituo cha afya kupata huduma za chanjo

 Na Baraka Messa, Songwe.

MWITIKIO Mkubwa wa wananchi kutumia vituo vya afya hasa akina mama wajawazito na watoto mkoani Songwe kumepunguza vifo vya watoto wachanga na akina mama wakati wa kujifungua.

Hayo yamebainishwa na mganganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Boniface Kasululu alipofanya mahojiano na mwandishi wa blog hii  baada ya kufanya kikao cha mikakati kuzuia vifo vya mama na mtoto hivi karibun.

Amesema  miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kubwa ya akina mama wajawazito kuhudhuria klinik na kujifungulia kwa wakunga wa jadi , jambo lililokuwa linapelekea vifo vya Mama wakati wa kujifungua pamoja na watoto.

" Baada ya kuongezeka vituo vya afya pamoja na elimu kwa wananchi katika mkoa wa Songwe, vifo vya mama na mtoto vimepungua kwa kiasi kikubwa ,

Mwaka 2022 vifo 38 vilitokea kwa upande wa akina mama wajawazito wakati wa kujifungua, Lakini mwaka 2023 vifo 33 vilitokea " alisema Dkt Kasululu.

Kwa upande wa vifo vya watoto wachanga kabla ya kuzaliwa na baada ya kuzaliwa alisema vimepungua kutoka kutoka vifo 320 mwaka 2022 na kufikia vifo 196 kwa mwaka 2023.

Amezitaja  sababu zilizopelekea kupungua vifo vya mama na mtoto kuwa ni pamoja na Jamii kubadilika baada ya elimu na kuanza kutumia vituo vya afya na hospital wakati wa kujifungua, kuwahi kliniki baada ya kupata ujauzito, kuongezeka vituo vya afya pamoja na hospitali za Wilaya pamoja na kuimalika kwa miundo mbinu ikiwa ni pamoja na magari ya kubebea wagonjwa.

Mratibu msaidizi wa huduma za uzazi kutoka nyanda za juu kusini Aida Chaula amesema kupitia vikao hivyo vya kujadili sababu za vifo vya mama na mtoto kumekuwa na mafanikio hasa hasa kwa vituo vya afya ambavyo having uwezo vimekuwa vikijengewa uwezo kwa kutembelewa na kujengewa uwezo na madaktari bingwa wa wanawake na watoto.

 Mganga Mkuu Wilaya ya Songwe Calvin Mwasha amesema kupitia vikao hivyo taifa limepunguza vifo vya mama wajawazoto kutoka vifo 556 kwa vizazi hai 100,000  mwaka 2015 mpaka vifo 104 kwa mwaka 2023 kwa vizazi hai 100,000 

Program Jumuishi ya ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto (MMMAM) imezingatia mpango wa tatu wa Maendeleo 2021/2022 -202/2026 wenye kuhakikisha unapunguza vifo vya watoto wakati wa kuzaliwa na baada ya kuzaliwa.

Pia  Programu  hiyo imejikita kuwekeza katika ukuaji wa binadamu katika miaka ya awali tangu ujauzito kujenga misingi imara kwa Mtoto kuwa mtu mzima mwenye afya anayewajibika na mwenye tija kwa Taifa.

Baadhi ya wananchi wamesema vifo vingi vya mama na mtoto vilikuwa vikisababishwa kutokana vituo vya afya na hospital kuwa mbali Hivyo baadhi ya akina mama kulazimika kujifungulia njia na wengine kwa wakunga wa jadi.

Suzan Kalinga ambaye ni mama wa watoto watatu alisema yeye alijifungulia nyumbani watoto wawili kutokana na hospital kuwa mbali , Lakini baada ya Serikali kusogeza huduma za vituo vya afya mtoto wake wa mwisho ambaye ana miaka miwili alijifungulia kituo cha afya na kupata huduma nzuri.

 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464