Na Kareny Masasy
MTOTO mwenye umri wa miaka mitatu kutoka kijiji cha Igalamya kata ya Usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga amezaliwa akiwa na tatizo la ulemavu wa vioungo pamoja na kichwa kikubwa hali ambayo mzazi wake anasimulia.
Mtoto huyo anajisogeza kwa kutumia makalio kwa kurudi kinyumekinyume hawezi kunyanyuka na kutembea, anajisadia hapohapo bila kujijua na kichwa ni kikubwa.
Samson Saramba baba wa mtoto huyo anasema alizaliwa katika Zahanati ya kijiji cha Usule mwaka 2021 na tatizo walilibaini wauguzi baada ya kuona eneo la mgongoni kuna kitu kama kovu jeusi.
Saramba anasema hakujua kama mke wake wakati wa ujauzito alikuwa anakunywa Folik Acid baada ya mtoto kutimiza mwezi mmoja waliona kovu linakuwa nundu wakamrudisha Zahanati wauguzi wakampatia rufaa ya kwenda kituo cha afya Tinde.
“Tulienda Tinde nao wakatupa rufaa ya kwenda moja kwa moja hospitali ya rufaa Bugando ambapo alifanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo nakushonwa lakini kichwa kiliendelea kuwa kikubwa na miguu haina nguvu.
Saramba anasema Daktari wa Bugando aliwaruhusu nakuwaambia waende warundi kliniki kwa uangalizi lakini wameshindwa kutokana na kukosa nauli ya kumrudisha nakuamua kumuacha hivyo hivyo.
Martha Kashindye (70) ambaye ni bibi wa mtoto huyo amekuwa akimlea anasema amekuwa akishinda naye nyumbani muda wote wazazi wake baba na mama wanamuacha nakwenda shambani wakati mwingine mjini kutafuta chakula walipewa namba ya kupiga kwa daktari hawafanyi hivyo.
Mwenyekiti wa kijiji cha Igalamya Felster Bundala anasema mtoto kweli anashinda na bibi yake nyumbani wazazi wake wanakuwa wamekwenda kwenye majukumu ya utafutaji.
“Kaya hiyo inaonekana maisha duni wameshindwa kumrudisha mtoto kwenye kliniki Bugando sababu ya kukosa fedha na mtoto anateseka hata uangalizi wa wazazi haupo”anasema Bundala.
Mtendaji wa kata ya Usule Shimba Masesa anasema kuna vijiji saba na wapo wahudumu ngazi ya jamii kila kijiji na kila kitongoji ambao wamekuwa wakifanya kazi ya kutoa elimu ya lishe kwa wajawazito na mama wanao nyonyesha.
Masesa anasema tatizo la mtoto huyu ni kubwa hawezi kujihudumia ,hawawezi kumuacha na bibi huyu hawezi kuondoka lazima amuangalie anavyoonekana mtoto huyo anaongea vizuri umri ukifika ataanzishwa shule.
“Sasa hivi ninaona hawana mpango wa kumpeleka sehemu yoyote kinyesi kinatoka hovyo bila utaratibu inachotakiwa uangalizi wa hali ya juu na kurudishwa kwa wataalamu na familia haina kitu chochote ”anasema Masesa.
“Tunajitahidi kutoa elimu kwenye jamii kwa kushirikiana na wahudumu ngazi ya jamii kuanzia kwenye vitongozji kwa kuwasaka wajawazito kuwapa elimu ya umuhimu wa lishe”anaongeza Masesa.
Ofisa lishe mkoa wa Shinyanga Yusuph Hamis anasema wapo baadhi ya wajawazito kuwa na tabia ya kufuata mtindo wa maisha wa ulaji wa kutofuata makundi matano ya vyakula ambayo ndiyo kichocheo cha kuongeza madini ya Folic acid mwilini.
Ofisa habari na mawasiliano kutoka shirika la Child Help Tanzania Milton Byemerwa anasema madini ya foliki acidi ni madini yatokanayo kwenye vyakula vitokanavyo na wanyama kama vile Maziwa, mayai,nyama na samaki na vyakula vya mbogamboga na matunda.
Byemerwa anasema mama akikosa madini hayo mwilini anao uwezekano mkubwa wa kuzaa mtoto mwenye ulemavu wa mgongo wazi na kichwa kikubwa.
Byemerwa anasema kila mzazi anatamani kuzaa mtoto akiwa na afya njema lakini tatizo linakuja mama anapokuwa mjamzito anakosa madini ya foliki acidi.
Byemerwa anasema upatikanaji wa vyakula hivyo ni rahisi siyo gharama mama anatakiwa ale kipindi chote cha ujauzito na njia nyingine anashauriwa ameze vidonge vyenye madini ya foliki acid miezi mitatu kabla ya kupata ujauzito.
“Madhara yatokanayo na ukosefu wa viini lishe mwilini kwa mjamzito anapobahatika kupata mtoto ndipo linajitokeza tatizo la mgongo wazi, hutokea kwenye paji la uso,utosini, uti wa mgongo, na kichwa kikubwa”anasema Byemerwa.
Byemerwa anasema ubongo wa mtoto na mishiba ya fahamu inatengenezwa ndani ya wiki tatu tangu kutungwa kwa mimba na mama akiwa hana madini ya kutosha mwilini changamoto hujitokeza kwa mtoto anayezaliwa ikiwemo ulemavu.
Byemerwa anasema wanachokifanya sasa hivi kwa watoto wanaozaliwa ulemavu huo ni kuwatafutia tiba na kuwaunganisha na madaktari bingwa pamoja na chama cha wazazi wenye watoto wa aina hiyo.
Hapa Tanzania kwa mujibu wa Waziri wa afya Ummy Mwalimu mwaka jana amesema watoto zaidi ya 6000 kila mwaka wanazaliwa na tatizo la ulemavu wa aina hiyo.
“Hapa duniani vizazi hai 1000 ikiwa wastani watoto watatu mpaka wanne wanazaliwa na mgongo wazi na kichwa kikubwa changamoto kubwa ni ukosefu wa lishe kwa mama kabla ya kupata ujauzito”anasema waziri Ummy.
Ofisa lishe kutoka taasisi ya chakula na lishe nchini (TFNC) Doris Katana anasema Uongezaji virutubishi maana yake ni kiwango cha kuongeza vitamin au virutubishi kwenye vyakula vya kawaida vinavyopatikana kwenye jamii.
Katana anasema virutubishi hivyo ni madini chuma, vitamin A, Madini joto lengo kuzuia pale tatizo linapotokea mfano watu wamekuwa wakitumia mtindo wa maisha kwenye vyakula vingi ambavyo havina madini.
“Madini ya foliki acidi ni muhimu kwa mama mwenye umri wa kuzaa akiwa na upungufu wa madini hayo hitilafu inatokea na ndipo anampata mtoto mwenye ulemavu huo”Katana .
Katana anasema ili mama aweze kukaa vizuri hali ya mwili wake wa kujiandaa kupata mtoto anahitaji madini na ale matunda,mbogamboga, jamii ya mikunde mayai kwa wingi nakushauriwa kutumia vidonge vya foliki asidi.
Katika kukabiliana na tatizo la udumavu nchini waziri mkuu Kassimu Majaliwa amesema serikali inatarajia kutenga bajeti kwaajili ya ununuzi na usambazaji wa mashine maalum za kuchanganya virutubisho kwenye vyakula.
Waziri mkuu Kassimu Majaliwa akikabidhi mashine zilizotengenezwa nchini na shirika la Gain ambapo zitakuwa na kazi ya kuchanganya virutubishi vya vitamin B,Foliki Acid sambamba na madini chuma na Zinki kwenye mahindi wakati wa kusaga.
“Mbinu hiyo itasaidia wanawake kuepuka na changamoto ya ukosefu wa madini mbalimbali ambayo yanasababisha mtoto kuzaliwa akiwa na matatizo”anasema Majaliwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464