Mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt Omar Sukari
Salum Maige, Geita.
SERIKALI mkoani Geita kupitia idara ya afya imewataka wananchi wa mkoa huo hususani mjini Geita kuchukua tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu kwa kuzingatia usafi,kutumia vyoo na maji safi na salama yaliyocheshwa.
Tahadhari hiyo imetolewa na mganga mkuu wa mkoa wa Geita Dkt.Omar Sukari kwenye uzinduzi wa utoaji chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi, hafla iliyofanyika katika shule ya msingi Mwatulole halmashauri ya mji wa Geita.
Dkt. Sukari amesema, kuna wagonjwa wamebainika kuugua kipindupindu katika mji wa Geita na baadhi yao wamelazwa na wengine wameruhusiwa, hivyo wananchi wanatakiwa kuchukua tahadhari ili usiene zaidi katika jamii.
Kauli hiyo imekuja ikiwa ni siku chache baada ya watoto wawili wa familia moja Kelvin Marco(11) na Monderic Marco(3) kufariki dunia kwa tatizo la kuhara na kutapika huko katika mtaa wa Uwanja kata ya Nyankumbu mjini Geia.
Mama wa familia hiyo pamoja na mtoto wa umri wa mwaka mmoja walilazwa katika hospitali ya halmashauri ya mji wa Geita baada ya kufikishwa hapo wakiwa na hali mbaya wakitapika na kuhara mfululizo.
“Nichukue nafasi hii kusema, Geita tuna kipindupindu, kuna familia imetibiwa , wapo waliolazwa wanaendelea na matibabu na wengine tumewaruhusu leo, niwaombe mchukue tahadhari kwa kuchemsha maji, kutumia vyoo siku zote, kukabiliana na magonjwa ya mlipuko kikiwemo kipindupindu”, anasema Dkt.Sukari.
Taarifa zisizo rasmi zinaeleza kuwa mpa watu 11 akiwemo mama na watoto wawili wameugua ugonjwa huo na kulazwa na kati yao watano wameruhusiwa aprili 23 mwaka huu kutoka, huku wengine wakiendelea kupatiwa matibabu.
Dkt.Sukari amesema, watoto wawili waliofariki kwa kuhara na kutapika miili yao ilizikwa na watu wa idara ya afya ikiwa ni kuchukua tahadhali ili ugonjwa huo usilete madhara ziadi kwa ndugu,jamaa na wananchi wa mtaa huo.
Mmoja wa familia ambayo imekumbwa na ugonjwa huo wa kuhara na kutapika, Ester Charles amesema, mmoja wa watoto hao alitoka shule na kula wali na maharage kisha kwenda kucheza lakini saa moja jioni alijisikia vibaya na kwenda kulala.
Ester anasema, ilipofika saa 10 usiku alianza kutapika na kumpa huduma ya kwanza kwa kumpatia kidonge cha flagyl na panado lakini aliendelea kutapika na kuharisha ambapo kila wakati alikuwa akiomba msaada wa kujisaidia.
“Muda mfupi na mdogo wake naye akaanza kutapika na kuharisha, wakalegea ilipofika saa 12 asubuhi mdogo wao mwingine naye akaanza kuharisha,tukawabeba tukawapeleka hospitali binafsi wakaongezewa maji na vipimo wakasema ni homa ya matumbo na maralia,wakatupatia dawa lakini walizidi kuhara na kutapika tukarudi nyumbani” , alisema Ester.
Aliongeza kwa kusema kuwa, “Ndiyo tukarudi tukamkuta mama na huyo mdogo hali zao ni mbaya tukaamua kuwapeleka hospitali wakalazwa, bahati mbaya mmoja alifariki wakati tukijiandaa kwenda hospitali mmoja alifariki akiwa anapatiwa matibabu”
Hivi karibuni mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Uwanja Enos Chelehani akizungumzia tukio hilo alisema, hali ya wanafamilia hao kuanza kuhara na kutapika iliwakuta usiku wa aprili 18 na aliyeanza kuonyesha hali hiyo ni mama wa familia hiyo jina linahifadhiwa.
“Baada ya kufika kwenye hiyo familia taarifa zinasema kuwa, mama ndiye aliyeanza kuhara,ambapo akiwa amelala usiku na mumewe alinyanyuka kwenda chooni ,lakini baadaye mwanaume alimfuatilia na kumkuta amelala na akiwa ameishiwa nguvu baada ya kuharisha”, alisema mwenyekiti huyo.
Hata hivyo,mwenyekiti huyo alisema ,toka hali hiyo ijitokeze katika familia hiyo hakuna mwananchi mwingine aliyekubwa na tatizo la kuhara na kutapika katika mtaa huo.
Mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela amesema, siku mbili zilizopita tatizo la ugonjwa wa kuhara na kutapika limeikumba familia moja mjini Geita na akawataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo hatari unoweza kusababisha madhara.
“Ni ugonjwa
unaosababisha vifo kwa haraka , kwa kuwa unapoteza maji mengi ,asilimia 70 ya
mwili wa binadamu umebebwa na maji, unapotapika na kuhara uwezo wa kuhimili ni
mdogo, ugonjwa upo , unaweza kuwa kipindupindu au ugonjwa mwingine, lakini
hatuna budi kuchukua tahadhari”, ame
sema Shigela.
Ameongeza, tahadhari hiyo itasaidia wananchi na serikali kutotumia gharama kubwa kwa matibabu na kuwataka wananchi kuzingatia maelekezo ya watalaamu wa afya ili kujilindi dhidi ya maambukizi ya ugnjwa huo hatari.
Mwisho.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464