BARAZA LA MADIWANI KISHAPU,WANANCHI WATAHADHARISHWA UGONJWA WA KIPINDUPINDU BAADA YA KUIBUKA UPYA WILAYANI HUMO 29 WANASA
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kishapu William Jijimya.
WANANCHI wilayani Kishapu, wametahadharishwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya ugonjwa wa Kipindupindu,ambao umeelezwa kuibuka upya wilayani humo,huku watu 29 wakibainika kuwa na ugonjwa huo na hakuna Kifo.
Hayo yamebainishwa leo Mei 9,2024 Kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani wilayani Kishapu cha Robo tatu ya mwaka 2023/2024.
Kaimu Mkurugenzi Halmashauri ya Kishapu Sabinus Chakula.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Dk. Joseph Bahati,amebainisha hayo kwenye Baraza hilo la Madiwani wakati akiwasilisha Taarifa ya Lishe na hali ya ugonjwa wa Kipindupindu wilayani humo baada ya kuibuka upya.
Amesema awali Ugonjwa wa Kipindupindu uliibuka Mkoani Shinyangakuanzia Januari hadi Februari mwaka huu na ukadhibitiwa na kuisha kabisa, lakini ugonjwa huo umeibuka upya tena wilayani Kishapu.
Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kishapu Dk. Joseph Bahati.
" Ndani ya Siku hizi tatu kumeibuka upya tena upya Ugonjwa wa Kipindupindu wilayani Kishapu, na upo katika Kata tatu ambazo ni Mwataga,Mwamashele na Mwakipoya"amesema Dk.Bahati.
"Wagonjwa ambao wamebainika wanakipindupindu kwenye Kata hizo ni 29 lakini hakuna Kifo, na wanaendelea kupata Matibabu kwenye Kambi yetu na taarifa mpya ambazo nimepewa Wagonjwa waliobaki ni 16 na hali zao ni nzuri,"ameongeza.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana.
Aidha,ametoa tahadhari kwa wananchi wilayani Kishapu, kwamba wafuate taratibu za kiafya ikiwamo kufanya usafi wa Mazingira, kuchemsha Maji, kutibu Maji na dawa,kuacha kula hovyo na kujisaidia hovyo, pamoja na kutembea na Maji ya kunywa Mashambani.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Wiliam Jijimya, akizungumza kwenye Baraza hilo, amesema Kipindupindu ni Vita na kina chukua uhai wa watu, na hivyo kuwataka Wananchi wilayani humo kuzingatia Elimu na Masharti ya Watalaamu wa Afya.
Kaimu Katibu Tawala wilaya ya Kishapu Fadhili Mvanga.
Amewataka pia Wataalamu wote wa Afya wilayani humo,kwenda kutoa elimu kwa wananchi juu ya kukabiliana na Ugonjwa huo wa Kipindupindu, na siyo kuishia kwenye kikao cha Baraza la Madiwani.
Mwakilishi wa Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Ibrahimu Makana ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi sehemu ya Menejiment,Ufuatiliaji na Ukaguzi, akizungumza kwenye Baraza hilo amesisitiza suala la wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya Kipindupindu ikiwamo kufanya usafi wa Mazingira,kufukia Madimbwi ya Maji.
Baadhi ya wananchi wa Kishapu wakiwa kwenye Baraza la Madiwani.
Katika hatua nyingine Makana, amewataka Watumishi wanaokusanya fedha za Mapato wawe wanapeleka fedha hizo Benki kwa wakati na siyo kukaanazo, hali ambayi ni ukiukaji wa Sheria, kanuni na miongozi ya ukusanyaji mapato ambapo wanapaswa kuweka fedha hizo Benki ndani ya Saa 24.
“Hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu jumla ya fedha za Mapato ambazo zimekusanywa kwenye Halmashauri hii ya Kishapu kiasi cha Sh.milioni 15.3 zipo mikononi mwa wakusanyaji Mapato na hazijapelekwa benki,”amesema Makana.
Ameiagiza Ofisi ya Mkurugenzi wilaya hiyo wawe wanaziwesha Timu za ukusanyaji Mapato, pamoja na kuwabadilisha mara kwa mara wasikae muda mrefu, huku akisisitiza pia kuongeza kasi kwenye ukusanyaji wa mapato katika mazao ya Mpunga,Pamba na Kunde, ili kuongeza Mapato ya Halmashauri ambayo kwa sasa yamefikia asilimia 64.
Kaimu Katibu Tawala Wilaya ya Kishapu Fadhili Mvanga, naye amesisitiza suala la ukusanyaji mapato, huku akiwataka wanaokusanya Mapato wawe waadilifu pamoja na kufuata Sheria za ukusanyaji mapato na kuibua vyanzo vipya ya mapato.
Katika Baraza hilo la Madiwani wilayani Kishapu ziliwasilishwa taarifa za Kamati mbalimbali zikiwamo za Fedha,Uchumi, Ujenzi na Mazingira, huduma za Jamii,Smack na Lishe, pamoja kutolewa Semina ya Maadili kutoka Secretaliety ya Maadili Kanda ya Magharibi Tabora.
Kikao cha Braza la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464