RC MACHA ARIDHISHWA UTUNZAJI WA MAZINGIRA UNAOTEKELEZWA KWENYE CHANZO CHA MAJI - IHELELE.

RC MACHA ARIDHISHWA  UTUNZAJI WA MAZINGIRA UNAOTEKELEZWA KWENYE CHANZO CHA MAJI - IHELELE.


Na. Paul Kasembo, Ihelele Misungwi.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi Kahama Shinyanga KASHWASA kwa namna inavyotekeleza utunzaji wa Usafi na Mazingira katika chanzo chake cha maji kilichopo Ihelele Wilaya ya Misungwi Mkoani Mwanza huku akitoa wito kwa wale wanaodaiwa ankara za maji kulipa kwa wakati ili kuiwezesha Mamlaka kutoa huduma iliyo bora na stahiki kwa wananchi.

RC Macha ametoa pongezi hizo jana alipotembelea na kuona namna ambavyo Mamlaka inavyoendesha Mradi wa Maji kutoka Ziwa Victoria na kuuza maji ya jumla kwa Mamlaka nyingine zinazohusika na usambazaji wa maji kwa wananchi katika maeneo ya mijini na vijijini ambao wamegawanyika katika makundi matatu (3) ambayo ni Mamlaka za Maji Mijini (WSSA), Jumuiya za Wayoa Huduma ya Maji (CBWSO) na Mgodi.

"Nawapongeza sana kwa namna ambavyo mnachapa kazi hii ya kutoa huduma muhimu kwa maisha ya watu, lakini kwa dhati kabisa nawapongeza zaidi kwa utunzaji mkubwa na bora kabisa wa mazingira katika chanzo hiki cha maji Ihelele hongereni sana KASHWASA," amesema RC Macha.

Kwa KASHWASA inazalisha maji kiasi cha lita 80 Milioni kwa siku ambapo baadhi ya miundombinu inaweza kupanuliwa na kuongeza uwezo wa kuzalisha maji hadi kufikia lita 120 milioni kwa siku na kutoshereza mahitaji ya watu zaidi ya 1,900,000 pamoja na mifugo yao kwa Mikoa sita (6) ya Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Tabora, Singida na Geita huku ikitajwa kutoa huduma kwa saa 23.5 kwa siku.

KASHWASA iliiundwa kwa Tangazo la Serikali Na. 45 la mwaka 2007 na inatimiza majukumu yake kwa mujibu wa Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira Na.5 ya mwaka 2019 pamoja na maeneo mengine yaliyoongezwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 359 la mwaka 2023
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464