RC MACHA AWASIHI VIONGOZI WA DINI KUTOA MAFUNDISHO SAHIHI YA NENO LA MUNGU KWA WAUMINI WAO,MAADHIMISHO SIKU YA CCT SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewasihi viongozi kutoka Madhehebu mbalimbali ya kidini mkoani humo kutoa mafundisho sahihi ya Neno la Mungu kwa waumini wao.
Macha amebainisha hayo leo Mei 26,2024 alipokuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Mkoa wa Shinyanga,ambayo inaunganisha Umoja wa Madhehebu ya Kikristo ya Kiprotestanti hapa Nchini.
Akizungumza wakati akitoa hotuba, amewasisitiza viongozi wa Madhehebu mbalimbali ya kidini mkoani humo, kwamba watoe mafundisho sahihi ya Neno la Mungu kwa waumini wao ambayo yatawajenga kiroho,kiimani pamoja na kutenda yaliyo mema.
Amesema sasa hivi kumeibuka tabia ya viongozi wa dini hasa Wahubiri binafsi baadhi yao wamekuwa wakitoa mafundisho ya uongo ambayo hupotosha watu.
"Mafundisho mengine yanakinzana na tamaduni zetu za kiafrika,likiwamo suala la ndoa ya jinsia moja, tuone mafundisho sahihi ya Neno la Mungu siyo kuwaambia watu wainua simu juu eti wakifika nyumbani wanakuta hela zimeingia kwenye simu zao, msilemaze watu waambieni wafanye kazi, na nyie viongozi wa dini kazi yenu ni kubariki kazi zao,"amesema Macha.
"Toeni pia mafundisho ya Neno la Mungu shuleni na hasa vyuoni sababu huko kuna shida kubwa ya Mmomonyoko wa maadili, pamoja na kwenye ndoa ili kuondoa mifarakano,"ameongeza.
Aidha,amewataka pia viongozi wa kidini kujiepusha na Migogoro ndani ya Makanisa,pamoja na kuendelea kuwa na Mahusiano mazuri kati ya dini moja na nyingine na kuishi wa amani na upendo.
Aidha,ameipongeza Jumuiya hiyo ya CCT kwa kuunga Mkono juhudi za Rais Samia katika suala la utunzaji Mazingira pamoja na kuhamasisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia.
Pia,amewasihi viongozi wa dini kuendelea kuliombea Amani Taifa,pamoja na Viongozi hususani Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, pamoja na kuombea uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika mwaka huu,ili uwe wa Amani na hata kupata viongozi wazuri wenye hofu ya Mungu.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya CCT Mkoa wa Shinyanga Askofu Zacharia Bugota, amesema viongozi wa dini wapo pamoja na Serikali katika kuombea Amani, pamoja na kushiriki kwenye Kampeni mbalimbali ikiwamo ya utunzaji Mazingira na Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Katibu wa Jumuiya ya CCT Mkoa wa Shinyanga Mathias Chidama,akisoma Risala,ametaja Malengo na Mikakati kwamba wataendelea kutoa Mafundisho sahihi ya Neno la Mungu,kuhamisha usawa wa kijinsia,kupinga ukatili na ndoa za utotoni.
Mikakati mingine ni kutoa elimu ya uraia, kushiriki kampeni ya utunzaji Mazingira,kupanda Miti na kuhamasisha Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia,na kupinga Ramli chonganishi.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI👇👇
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akizungumza kwenye maadhimisho ya CCT Day.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Julius Mtatiro akizungumza kwenye maadhimisho ya CCT Day.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya CCT Mkoa wa Shinyanga Askofu Zacharia Bugota akizungumza kwenye maadhimisho hayo.
Katibu wa Jumuiya ya CCT Mkoa wa Shinyanga Mathias Chidama akisoma Risala kwenye maadhimisho hayo.
Viongozi wakiwa Meza Kuu.
Maadhimisho ya CCT Mkoa wa Shinyanga yakiendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akiwasili kwenye Maadhimisho ya CCT Mkoani humo akipokelewa na Mwenyekiti wa CCT Mkoa Askofu Zacharia Bugota.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Picha za pamoja zikiendelea kupigwa.