RC MACHA AIPONGEZA MENEJIMENTI YA BUZWAGI
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameipongeza sana Menejimenti ya Mradi wa Ufungaji Mgodi wa Buzwagi kwa namna ambavyo imejipanga katika kutekeleza kazi hii ikiongozwa na Meneja wa Mgodi Bi. Zonnastral Mumbi, Meneja Uhusiano wa Jamii na Miradi Buwagi Ndg. Stanley Joseph pamoja na Ndg.James Maziku ambaye ni Mkurugenzi Uwekezaji na Uwezeshaji kutoka EPZA huku akisema kuwa amridhishwa zaidi na uhalisia wa taarifa yao na namna ya uwasilishaji wao pia.
Pongezi hizo amezitoa jana alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa mradi huu ambao unafuatia kufungwa kwa Mgodi na kuanza maandalizi ya uanzishwaji wa mradi mpya wa Buzwagi Special Economic Zone mradi unaotajwa kuja kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji wa viwanda, wafanyabiashara na ofisi kubwa zaidi za kikanda na kimataifa jambo ambalo litawezesha utoaji wa huduma kwa Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga, Mikoa jirani pamoja na Nchi za Burundi, Rwanda na maeneo mengine ukizingatia kuwa Kahama ni Lango la Kibiashara.
"Naipongeza sana Menejimenti ya Mradi wa Ufungaji Mgodi wa Buzwagi kwa namna ambavyo mmejipanga katika uwasilishaji wa taarifa yenu, utekelezaji wa ufungaji mgodi huu na mikakati yenu katika kuimarisha uhusiano wenu na jamii inayowazunguuka pamoja na Serikali, nawapongeza sana Menejimenti ikiongozwa na Bi. Zonnastral," amesema RC Macha.
"Nimewasikiliza vizuri sana, nimewatazama vema sana nyuso zenu wakati miiwasilisha hakika mnafahamu vema wajibu wenu, na mnaifahamu vizuri kazi iliyopo mbele yenu katika utekelezaji wa mradi huu wa ufungaji, tunataka vijana kama ninyi ambao mnakiishi kile mnachokisema,"amesisitiza RC Macha.
RC Macha amesema, lengo la Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha mradi huu unaokwenda kuanzishwa wa Buzwagi Special Economic Zone unawanufaisha wananchi wote na kuleta tija ya kuwahudumia jamii yote katika nyanja zote, huku akizikumbusha Ofisi za mgodi na Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama kuhakikisha wanashirikiana kwa karibu zaidi katika utekelezaji wa kazi hii ukizingatia inahusisha ardhi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464