KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA MWANZA YAKOSHWA NA MRADI WA MAJI WA BUTIMBA
KAMATI YA SIASA YA CCM MKOA WA MWANZA YAKOSHWA NA MRADI WA MAJI WA
BUTIMBA
Kamati ya Siasa ya Halmashauri
Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Mwanza imeridhishwa na ukamilishwaji wa
mradi wa maji wa Butimba na ufanisi wake.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mwanza,
Michael Lushinge (Smart) amedhihirisha hayo Mei 27, 2024 wakati wa ziara ya
Kamati ya kukagua miradi ya maendeleo Wilayani Nyamagana.
"Tumefarijika kwa mradi huu wa maji. Mradi ni mzuri, umekamilika na
unatoa huduma. Kwa niaba ya Kamati tumeridhika," amesema Lushinge.
Lushinge ameielekeza MWAUWASA
kuhakikisha inaharakisha mpango wake wa usambazaji maji ili mradi ulete matokeo
yanayokusudiwa sambamba na kuhakikisha usimamizi wa karibu unakuwepo ili mradi
uwe endelevu.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa
Kamati, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza
(MWAUWASA), Neli Msuya amesema pamoja na kukamilika kwa mradi wa Butimba na
kuanza kutoa maji, hatua inayofuatia ni ya kuboresha mfumo wa usambazaji maji kwa
kuongeza mtandao wa bomba na kujenga matenki makubwa ya kuhifadhia maji.
"Ili kuhakikisha maji kutoka katika mtambo wa Butimba yanapatikana
kwa uwiano sahihi, Serikali kupitia MWAUWASA itatekeleza mradi wa ujenzi wa
vituo viwili vya kusukuma maji na matenki makubwa matano," amefafanua Neli.
Neli ameainisha maeneo
yatakayojengwa matenki kuwa ni Buhongwa (lita milioni 10), Fumagila (milioni
10), Nyamazobe (milioni 5), Kisesa (milioni 5) na Usagara (milioni 1).
"Tunamshukuru Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuipa Sekta
ya Maji kipaumbele cha kipekee," amesema Neli. Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Neli, mradi wa Maji Butimba ulianza kutekelezwa Februari 1, 2021 na ulikamilika
Oktoba 31, 2023 na unatarajiwa kukabidhiwa rasmi kwa MWAUWASA Oktoba mwaka huu.