Na Stella Homolwa,Shinyanga Press Club Blog
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha ameipongeza Mamlaka ya majisafi na usafi wa Mazingira (KASHWASA) kutokana na kutekeleza mradi huo kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni pamoja na kupata hati safi ya ukaguzi kutoka kwa Mdhibiti na mkaguzi Mkuu wa hesabu za serikali(CAG).
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo katika Kijiji cha
Ihelele Wilayani Misungwi Mkoa wa Mwanza,Mkuu wa Mkoa amesema kazi kubwa
imefanyika ya kutunza mazingira na kuhakikisha maji yanakuwa katika ubora wa
kimataifa.
Amesema mradi huo tangu ulipoanzishwa mwaka 2009 Mamlaka hiyo
kila ikifanyiwa ukaguzi imekuwa ikikidhi vigezo na kupatiwa hati safi jambo
ambalo linapaswa kuigwa na taasisi zingine katika kusimamia miradi yao.
“Nimeona namna ambavyo maji yanaanza kusafishwa kutoka Ziwa
Victoria hadi kufikia hatua ya kuwa safi na kusambazwa kwa wateja na hatua kubwa
mnastahili pongezi,mambo kama haya wananchi wetu wanatakiwa
wajue,Madiwani,wabunge na kamati za watumia maji vijijini ili kujua gharama”amesema
Macha
Amesema wakati mwingine gharama za maji zinapokuwa juu
inatokana na mchakato mzima unaotumika kutibu maji hayo, hadi kufikia hatua ya
kupelekwa kwenye tenki kuu ili kusambazwa kwa wateja.
Mkuu wa Mkoa akizungumzia changamoto ya madeni katika taasisi
hiyo amesema licha ya kutoa huduma lakini bado ina zidai Mamlaka za maji ambazo
zinauziwa maji na Kashwasa zaidi ya Sh bilioni 14 zikiwemo jumuiya za watumia
maji ngazi ya jamii.
Changamoto ambayo imekuwa ikikwamisha Mamlaka ya Majisafi na usafi wa Mazingira
Kahama Shinyanga (Kashwasa)kushindwa kulipa deni la umeme la Tanesco zaidi ya
Shilingi bilioni nne na kusababisha kusuasua.
Amesema Kuendesha
mitambo ya maji ina gharama kubwa ambapo kwa mwezi umeme pekee unagharimu Sh650
milioni,ambapo ametoa wito kwa mamlaka zote zinazodaiwa kulipa madeni yake
pamoja na wananchi kulipa bili zao kwa wakati.
Mkurugenzi wa Kashwasa
Mhandisi Patrick Nzamba,amesema Kituo hicho kinauwezo wa kusafisha na kuchakata maji lita milioni 80 kwa siku na kwamba
wamefikia Mikoa ya Mwanza,Tabora,Singida,Simiyu,Geita na Shinyanga.
Amesema kwa sasa wanatoa huduma ya maji kwa watu milioni 1.9 katika
Mikoa hiyo,ambapo wana makundi matatu
zikiwemo Mamlaka za maji nane,watoa huduma za maji ngazi za jamii 95 na kundi
la jingine ni migodi.