TANZANIA: MTIBWA SUGAR YASHUKA DARAJA BAADA YA MIONGO MITATU

 

 Mtibwa Sugar yashuka daraja baada ya miongo mitatu


,

Mabingwa wa zamani wa soka wa Tanzania Bara, Mtibwa Sugar wameshuka daraja kutoka Ligi Kuu ya nchi hiyo, baada ya miaka 29 tangu walipopanda daraja mwaka 1995.

Mabingwa hao mara mbili wa 1999 na 2000 wameshuka daraja rasmi baada ya kukubali kichapo cha magoli 3-2 mbele ya timu ya Mashujaa ya Kigoma katika pambano lililofanyika dimba la Lake Tanganyika.

Kwa kichapo hicho Mtibwa wamebaki na alama 21 huku ukibakia mchezo mmoja kabla ya kukamilisha msimu, hivyo hata wakishinda watakuwa na alama 24 ambazo tayari zimevukwa na timu nyingine 15 za ligi hiyo ya timu 16.

Timu mbili za mwishoni mwa msimamo zinashuka daraja moja kwa moja wakati timu mbili za nafasi ya 13 na 14 zitacheza mtoano na timu za Championship kupigania kubaki ligi kuu.

Ligi Kuu ya Tanzania Bara itakamilika mwisho mwa juma lijalo na tayari mabingwa Yanga walionyakua taji la tatu mfululizo wamekabidhiwa kombe la ubingwa Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa katika jiji kuu la kibiashara la Dar es Salaam.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464