KUNI, MKAA VINAVYOWEKA KITANZINI AFYA, UCHUMI WA WANAWAKE NA MISITU

 KUNI, MKAA VINAVYOWEKA KITANZINI AFYA, UCHUMI WA WANAWAKE NA MISITU


 Na Ibrahim Rojala,Mwakitolyo-Shinyanga

Nilianza kuugua kifua,kikawa kinabana,nguvu zinaisha mwilini,baadae mwenzangu akanipeleka hospitali Kahama, nilipofikishwa Kahama wakasema nendeni Bukumbi,nikatibiwa lakini kitu cha kwanza alichoniambia daktari alisema punguza matumizi ya mkaa kwasababu unaonekana umetumia mkaa muda mrefu,damu imekuwa nyepesi na mapafu yanaonekana yana vumbi”.

Ndiyo alivyoeleza Mariam Matwiga (45) Mkazi wa Kijiji cha Mwakitolyo kata ya Mwakitolyo halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani Shinyanga ambaye ili kumudu mahitaji ya familia yake ya watoto sita aliamua kujikita katika biashara ya vitumbua na maandazi aliyoifanya kwa muda mrefu.

Ili kufanikisha biashara yake hiyo,Mariam alilazimika kujenga urafiki wa karibu kati yake na kuni na mkaa ili kuendeleza mapambano dhidi ya umasikini na lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa familia yake,lakini baada ya urafiki huo kudumu kwa kipindi cha miaka tisa mambo yakabadilika na mapambano yakabadilika kutoka kuipambania familia na kugeuka na kuwa dhidi ya madhara ya matumizi ya kuni na mkaa kwenye afya ya Mariam.

 Maumivu ya kifua yaliyoambatana na mwili kuishiwa nguvu vilifuatiwa na utaratibu wa kutafuta suluhu ya tatizo na baada ya kupita katika hospitali kadhaa ndipo majibu yakatoka yakionesha kuwa kinachomsumbua ilikuwa ni matokeo ya matumizi ya kuni na mkaa kwa muda mrefu kabla ya daktari kumshauri kutojihusisha tena na matumizi ya nishati hizo za kupikia.

 Ugonjwa huo licha ya kuyumbisha hali ya kiuchumi ndani ya familia ya mama huyu mjane pia ulipelekea mtoto wake wa kwanza kukatisha masomo akiwa mwaka wa pili chuoni ili aweze kuwasaidia wadogo zake kuendelea na elimu pamoja na kupata mahitaji ya msingi baada ya afya ya mama, ambaye alikuwa tegemeo la familia kutetereka.

 Utafiti wa athari za upatikanaji wa Nishati Endelevu kwa mwaka 2021/2022 uliotolewa Novemba 2023 na Ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) unaonesha kuwa asilimia 67 ya kaya zote Tanzania Bara hutumia kuni kama chanzo chao kikuu cha nishati kwa ajili ya kupikia, huku mkaa ukichukua nafasi ya pili (asilimia 25).

 Aidha Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 unaeleza kwamba,asilimia 7 pekee ya watu nchini Tanzania wanategemea teknolojia safi ya nishati kwa ajili ya kupikia, hii inajumuisha majiko yanayotumia umeme, gesi asilia, nishati ya jua na nishati itokanayo na alcohol/ethanol.

Sehemu kubwa ya watu iliyosalia ambayo ni asilimia 93 wanategemea nishati ngumu ya teknolojia kama vile, makaa ya mawe, mkaa, kuni, majani,magugu taka, mabaki ya mazao ya kilimo na vinyesi vya wanyama, mabaki ya mbao,plastiki na pumba za mbao katika mapishi.

Wakati Mariam katika makala hii akielezea athari za kiafya alizokumbana nazo kutokana na matumizi ya mkaa na kuni katika biashara yake,hali ni tofauti kwa Mwanamke Mariam Doma Msomi, mjasiriamali wa biashara ya chakula(mgahawa) na mkazi wa kata ya Mwakitolyo halmashuari ya wilaya ya Shinyanga ambaye bei za mkaa na kuni kwake zimekuwa changamoto kubwa na kueleza kwamba anafanya biashara ya mgahawa ili tu yeye na familia yake  waweze kujikimu mahitaji ya kila siku akilalamikia kukosa faida.

Mkaa bei ghali,ni shilingi 9000 hadi 10000 kwa debe hususani nyakati hizi ambazo mvua zinanyesha, kwahiyo unajikuta unafanya biashara ambayo haina maslahi,unakuwa upo tu kwaajili ya kupata chakula ili familia yako iweze kuishi,kuni sita ni shilingi 1000,kwa siku natumia kuni za shilingi 5000 na mkaa wa shilingi 7000,yaani unapata faida kidogo na inakuathiri kwasababu unajikuta bado unadaiwa pango la nyumba mahali unapofanyia biashara”Anasema Mariam.

Kuhusiana na uelewa wake juu ya matumizi ya nishati safi za kupikia, Mariam Doma Msomi anasema huwa anaangalia na kusikia kupitia vyombo vya habari lakini hana uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya nishati hizo ambazo anaamini kwamba pengine akijengewa uelewa zinaweza kumkwamua katika biashara yake hiyo aliyoifanya kwa kipindi cha miaka mingi akiitegemea kusomesha watoto, kuendesha maisha ya familia na kueleza kwamba kuna wakati alikwama kufanya biashara hiyo kutokana na ughali wa bei ya kuni na mkaa na kuiomba serikali kutoa elimu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Bi.Mariam Doma Msomi akiwa katika eneo lake la Biashara ya Mgahawa pamoja na nishati za Mkaa na Kuni ambazo huzitumia kila siku kuendesha shughuli zake za uuzaji wa chakula katika kata ya Mwakitolyo Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga.

Wakati wanawake hawa wakihitaji msaada wa serikali na wadau wa maendeleo ili kujengewa uelewa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia,hali ni tofauti kwa mwanamke Daines Martin Masua ambaye licha ya kukiri kuwa na uwezo wa kumudu gharama za  kununua jiko la gesi au mkaa anaeleza kwamba hayuko tayari kununua wala kutumia nishati hizo.

“Mimi toka nimezaliwa nilikuta nyumbani wanapikia kuni,tumeenda na hizo kuni baaadae mapori yakawa yamekata tukanza mkaa mpaka sasa hivi na umri huu nilionao wa miaka 40 natumia mkaa tu,changamoto  kuni zenyewe unapangiwa labda tano,mkaa debe mpaka 12,000 ni kuwa mkaa ni bei,unanunua hata mkaa wa 500 unapikia kusudi upate kula,labda tatizo ni ushamba,mimi gesi siwezi kutiumia kwakweli,hapana siwezi kutumia gesi yaani hamna uwezo wa kununua gesi au hata jiko la umeme ninao lakini siwezi kutumia mimi gesi, kama gesi ningekuwa nimeshanunua au jiko la umeme kabisa”

Maelezo haya yanaonesha wazi kuwa bado uelewa wa matumzi ya nishati safi ya kupikia ni changamoto miongoni mwa wanawake ndani ya jamii na hivyo licha ya wanawake kuendellea kuhatarisha afya zao kutokana na matumizi ya nishati chafu za kupikia pia viya ya mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi kutokana na uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa lengo la kupata kuni na mkaa inaendelea kukabiliwa na ugumu.

Tarehe 8, Mei 2024 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam ilielezwa kwamba takribani hekta 469,000 za misitu hupotea kila mwaka ambapo nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha kutoweka kwa misitu hiyo.

Akizungumza kuhusiana na afya za watumiaji wa nishati hizo chafu kupitia uzinduzi huo,Rais Dkt.Samia alisema nguvu kazi ya Taifa ambao ni Watanzania zaidi ya elfu 33 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na magonjwa ya mfumo wa kupumua ambayo yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uvutaji wa moshi kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Uwepo wa mkakati huo unaotarajiwa kutekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 kati ya mwaka 2024-2034 lengo likiwa ni kuhakikisha asilimia 80 ya watanzania ndani ya kipindi hicho wanafikiwa na kutumia nishati safi ya kupikia.

Ili kufikia malengo ya mkakati huo ni vyema kipengele cha elimu ya umuhimu wa matumizi ya nishati safi na uainishwaji wa madhara ya matumizi ya nishati chafu kwa kupikia,kupunguza bei ya nishati na upatikanaji kwa urahisi wa nishati hii katika maeneo ya vijijini pamoja na ushirikiano na sekta binafsi katika kufikisha nishati hii.

SOURCE:JAMBO FM

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464