Jengo la
Hosptali ya Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga.
Na Kareny Masasy,
UKWELI usio pingika hakuna mwanamke ambaye ana beba ujauzito na ikifikisha miezi tisa anapojifungua akose mtoto kwani matarajio yake ni kupata mtoto mwenye afya njema na kuendelea kuishi.
Baadhi ya wanawake Manispaa ya Kahama Maimuna Deus na Blandina Haule wanasema watoto wanaofariki mara nyingi wazazi wamekuwa wakielezwa amekunywa maji ya tumboni au kashindwa kupumua.
“Mimi nilifiwa na mtoto mchanga hakufikisha siku 28 kwanza hakulia wakati namzaa walimpiga piga mgongoni ili ashtuke na baadaye akalia lakini tulikwenda nyumbani wakawa wananiambia ana ugonjwa wa degedege”anasema Haule.
Mratibu wa afya ya Uzazi Mama na mtoto Manispaa ya Kahama Caroline Malesela anasema kupitia mradi wa Saver bandle of birth Care (SBBC) ulioanza mwaka 2021 mwezi Februari kwa kutoa mafunzo kwa watoa huduma 56 nao wakawa vinara wa kuwafundisha wenzao.
“Mradi pia umeleta vifaa kwaajili ya kujifunza na vifaa vya kumpima mtoto ili kuona mapigo ya moyo kwa mtoto kama yupo hai zamani utaalamu na vifaa hivyo hatukuwa nao na watoto walikuwa wanapoteza maisha” anasema Malesela.
Malesela anasema Manispaa ya Kahama Vituo sita vimepata wahudumu waliopitia mafunzo na kupitia mradi huu wadau hao wameajiri watu wanaofuatilia takwimu za mama wanaojifungua salama pamoja na watoto na waliopoteza maisha pia .
“Takribani kwa siku watoto wanazaliwa kwa hospitali ya manispaa ya Kahama ni 35 hadi 40 na kwa mwezi watoto zaidi ya 1000 na kila mtoto anaweza kuzaliwa na changamoto zake”anasema Malesela.
Watoto wengi wametambulika na kupona ndiyo maana tulikuwa tunaendelea kuona vifo vya watoto wachanga vinazidi ikiwa mwaka 2020 kulikuwa na vifo 382 vya watoto wachanga.
Baada ya mradi kuanza waliona mabadiliko ya kuokoa vifo hivyo mpaka mwezi Desemba 2021 kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 350 na mwaka 2022 kulikuwa na vifo 326 na mwaka 2023 kulikuwa na vifo 281.
Muuguzi kinara kutoka ofisi ya Muuguzi kitengo cha kujifungua Zahara Hassan anaelezea namna wanavyofanya kazi ya kumuokoa mtoto baada ya kuzaliwa kupitia mradi wa kitita cha uzazi salama ambao umesaidia kuokoa vifo vya watoto wachanga kwa asilimia kubwa wilaya nzima ya Kahama.
Hassan anasema baada ya kupata mafunzo amekuwa wakitembea kwenye wodi ya kujifungua kutoa elimu kwa wengine namna ya kumuhudumia mtoto mwenye shida ya kupumua ambapo imekuwa ikitokea kwa baadhi ya watoto na kuokoa maisha yao.
“Tumepewa vifaa maalum na kupata mafunzo ya namna ya kutumika kifaa cha kupima mapigo ya moyo na kifaa cha kuweka tumboni baada ya mtoto kuzaliwa” anasema Hassan.
Hassan anasema kulingana na takwimu za vifo vya watoto wachanga wengi walikuwa wakifariki wakiwa bado tumboni na wengine wenye siku moja hadi 28 kutokana na hali ya kutopumua vizuri na kukosekana utaalamu kwa watoa huduma.
Muuguzi Nyabiseko Kadidi kutoka Kitengo cha uangalizi wa watoto wachanga Manispaa ya Kahama anasema wapo watoto wenye matatizo mbalimbali ambapo wamekuwa wakilazwa kwa siku watoto kumi hadi 15 na ndani ya mwezi takribani watoto 150 hadi 80.
Mkurugenzi wa Afya,ustawi wa jamii na Lishe kutoka ofisi ya Rais Tawala za mikoa na serikali za Mitaa Dk Rashid Mafume anasema zipo jitihada zimefanyika kwenye mradi wa Kitita cha uzazi salama ambacho kimesaidi upatikanaji wa kifaa kinachoitwa Moyo kupima mapigo ya mtoto na kifaa kinachoitwa Nevit kupima tumboni kwa mama.
“Hali ilivyo sasa nchini kumeanza kupungua vifo vya watoto wachanga kutokana na teknolojia iliyotumika ya kuwa na vifaa vya upimaji,matumizi ya takwimu na mafunzo kwa watoa huduma”anasema Dk Mfaume.
Dk Mfaume anasema vifo vya watoto wachanga hali ni mbaya walichobaini wataalamu walikuwa wanahangaika kupata mapigo ya moyo ya mtoto vifaa vilikuwa havipo na walipokuwa wakiona mtoto asipo hema wanamhesabu amefariki lakini sasa watoto wengi wameokolewa.
vifo vya watoto wachanga nchini vimepungua kwa asilimia 25 ni suala la kuwapongeza wadau na wataalamu wanao shauriana kwani wakilenga kuokoa vifo vya mama watakuwa pia wanapunguza vifo vya watoto wachanga na kupanua wigo wa mafunzo wa wauguzi kwenye vituo vyote.
Dk Mfaume anasema Shughuli nyingi zilikuwa zinafanywa na wadau kuhusu kupunguza vifo vya wajawazito nakusahau kuokoa maisha ya watoto wachanga na sasa kupitia mpango huu inawasaidia watoto kuwaangalia wakiwa bado tumboni na mpaka anazaliwa.
Mratibu wa mradi wa kitita cha uzazi Salama (SBBC) mkoa wa Shinyanga Janeth Mpemba unajihusisha na uzazi salama, mama wanaofariki wakati wa kujifungua na vifo vya watoto wachanga na watoto njiti.
“Tulianza mradi huu mwaka 2021 kwa mkoa huu kipindi cha miaka mitatu tulikuwa na malengo matatu kupunguza vifo vya mama kwa asilimia kumi ,watoto wachanga kwa asilimia 50”anasema Mpemba.
Mpemba anasema kipindi cha mradi awamu ya kwanza ilikuwa ni utafiti wakagundua vifo vya watoto wachanga vinachangiwa na watoa huduma kutojiamini na sasa wamewekeza kutoa mafunzo na vifaa ambapo vimepunguza vifo vya watoto wachanga.
Mpemba anasema mkoa wa Shinyanga walianza kwenye vituo sita na kipindi cha pili cha mradi wameongeza vituo nakufikia 28 na wahudumu 56 wamekwisha patiwa mafunzo.
Sera ya afya ya mwaka 2007 imewekeza katika kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji wa huduma za afya bure kwa kina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Uwekezaji wa serikali katika uhai wa mtoto unaonekana dhahiri kwenye kupungua kwa vifo vya watoto kati ya mwaka 2010 hadi 2015 ambapo kiwango cha vifo vya watoto wachanga kuanzia siku 0 hadi 28 vimepungua kutoka vifo 40 hadi vifo 25 kwa kila kizazi hai 1000.
mwisho
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464