Viongozi wa dini,Serikali na wadau wajadili malezi ya watoto.
|
|
Salum
Maige, Geita. MOJA ya
vikwazo katika kukabiliana na ukatili dhidi ya watoto hapa nchini ni uelewa
mdogo kuhusu malezi chanya na mawasiliano duni miongoni mwa wana familia
pamoja na wazazi kutotimiza majukumu yao ya msingi ya malezi.
Changamoto
hizi zimetajwa na baadhi ya wadau wa watoto pamoja na wizara ya maendeleo ya
jamii,jinsia wanawake na makundi maalumu nchini Tanzania waliokutana mkoani
Geita hivi karibuni kujadili namna bora ya malezi ya watoto kuanzia ngazi ya
familia ili kuondokana na mmomonyoko wa maadili katika familia, jamii na
taifa kwa ujumla.
Mwenyekiti
wa baraza la CPCT mkoa wa Geita Mchungaji Joshua William amesema,viongozi wa
dini wanao wajibu wa kuzikumbusha familia kuepukana na migogro ambayo
inachangia kuporomoka maadili.
“Sisi kama
viongozi wa dini tunao wajibu mkubwa sana kusimamia malezi bora ya watoto
kuanzi ngazi ya family, kwani ni kweli maadili yanashuka katika familia na
hii inachangiwa na wazazi au walezi kuacha majukumu yao”, anasema mchungaji
William
Naye
askofu Stephano Saguda wa kanisa la Tanzania Messionary Revival Church(TMRC)
amesema, ni kweli maadili ni mabaya sana kwa sasa katika jamii kutokana na
utandawazi ambapo hata familia ikiwa na malezi bora bado watoto wanapotoka
nje ya familia wanakutana na vikwazo vya malezi duni.
“Yapo
matangazo ya luninga yanachangia pia mmomonyoko wa maadili,unakuta tangazo
linaonyesha mtu akiwa amevaa mtupu,mavazi yasiyokuwa na staha,haya matangazo
yangezuiliwa yanachochea maadili mabaya”,anasema askofu Saguda.
Ameongeza
kuwa, wazazi ni chanzo cha familia kwa maana hiyo wanatakiwa kuwa makini sana
kuwafundisha watoto maadili ya Mungu maana wakifundishwa maadili mazuri hata
wakija kuwa wakubwa wanakuwa viongozi wazuri kuanzia kwenye familia zao hata
taifa kwa ujumla.
Christina
Gamba kutoka kituo cha huduma za kisheria mkoa wa Geita(GELAC)anasema,
malezi sahihi ya kumtengeneza mtoto ni kuanzia umri wa miaka 0-8,
pamoja na wazazi au walezi kuwa majukumu mengi ya uzalishaji mali hawapaswi
kusahau majukumu yao ya malezi kwa watoto.
“Zipo kesi
za watoto zinajitokeza kwa jamii na asilimia kubwa zina,watoto wanakatiliwa
kwa kupewa adhabu kuzidi umri wao,wengine kubwaka, hii inatokana na maadili
kuporomoka kuanzia ngazi ya familia baada tu ya wazazi kushindwa kutimiza
majukumu yao ya malezi bora” anasema Gamba.
Mkuu wa
dawati la jinsia na watoto wilaya ya Geita mkaguzi msaidizi wa polisi
Christina Katana amesema, kuna nafasi kubwa sana kwa wazazi kuleta maadili
mema kwa watoto ,na hivyo wazazi wanapaswa kuchukua nafasi zao za malezi bora
ili kuepukana na uharifu unaotokea katika jamii.
“Dawati la
jinsia na watoto tumekuwa tukitoa elimu kuhamasisha wazazi kuwa na malezi
bora kwa watoto, jamii inatakiwa kujikita kusimamia maadili ili kuwa na
familia bora,na jamii bora ya baadaye”, amesema Katana.
Mratibu wa
mradi wa Mtoto Kwanza kutoka shirika lisilo la kiserikali la NELICO mkoani
Geita Sophia Njete amebainisha kuwa, mradi huo unatekeleza programu jumuishi
ya Taifa ya malezi, makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(PJT-MMMAM) ambapo
moja ya majukumu yake ni kuhimiza wazazi na walezi kuwekeza katika malezi
bora kwa watoto.
Amongeza
kwa kusema kuwa, uwekezaji mzuri wa malezi ya mtoto ni kuanzia umri wa mwaka
0 hadi 8, umri ambao ubongo wa mtoto unakuwa kwa asilimia 90.
“Katika
umri huo tukimuandaa mtoto vizuri eneo hili, kuhakikisha kwamba tunatengeneza
watoto bora itasaidia kuwa na familia bora, jamii bora na taifa lenye watu
sahihi hata wanapokuwa viongozi wa serikali”, amesema Njete.
Wakati
wadau hao wakikutana kujadili namna bora ya kuimarisha malezi,makuzi na
maendeleo ya awali ya mtoto,jamii imekuwa na mtazamo mseto juu ya namna bora
ya kumlinda mtoto mwenye umri wa miaka 0-8.
Katika
mahojiano maalum baadhi ya wakazi wa mkoa wa Geita wamebainisha kuwa, wazazi
wamekuwa mbali na watoto,kushindwa kufuatilia mionendo yao hali inayochangia
ukatili dhidi ya watoto kwa kukosa malezi bora.
Mmoja wa
wakazi mjini Geita,John Kasenda anasema, ukatili kwa jamii umekidhiri hasa
kundi la watoto yakiwemo matukio ya kubakwa,kulawitiwa na kupewa adhabu zenye
kuumiza watoto visa vinavyosababisha vizazi vyenye visasi.
Kwa mujibu
wa wizara ya maendeleo ya jamii, jinsia, wanawake na makundi maalum ni kwamba
katika kipindi cha kuanzia julai,2023 hadi aprili, 2024 wizara hiyo
imeshughulikia mashauri 5,944 sawa na asilimia 41 yanayohusu familia na
matunzo ya watoto na mashauri 3,350 sawa na asilimia 23 yanayohusu watoto
waliozaliwa nje ya ndoa.
Aidha,Katika
taarifa ya waziri wa wizara hiyo Dkt.Doroth Gwajibu katika kipindi hicho
mashauri 3,411 yalifikishwa kwa maafisa ustawi wa jamii ambapo 1,642
yalipatiwa ufumbuzi na 443 yanaendelea kufanywa kazi na mashauri 1,326
yalipewa rufaa.
Mashauri
hayo yalipewa rufaa kwenda kwenye vyombo mbalimbali vya usuluhishi ikiwemo
mahakama mashauri 921 na mabaraza ya kata na jumuiya mashauri 405.
Dhima kuu
ya kongamano hilo ilikuwa ni kuimarisha uwezo wa wazazi au walezi kwenye
malezi chanya ya watoto ambapo serikali imeendelea kufanya jitihada
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuelimisha wazazi au walezi na jamii
kuhusu malezi bora ya watoto sambamba na kuhimiza wajibu wa wazazi au
walezi katika matunzo ya watoto na familia.
Ujumbe wa
viongoziwa dini kwenye kongamano hilo ni kuwaasa wazazi au walezi kuongeza
jitihada za makusudi katika malezi na makuzi bora ya watoto ili kukabiliana
na changamoto za uharifu ukiwemo ukatili unaotokea kwenye familia.
|