WANANCHI WA GEITA WALALAMIKIA LUGHA CHAFU ZINAZOTOLEWA NA WATOA HUDUMA ZA AFYA-
Saluma Maige. 16/05/2025
Wakati serikali ya Tanzania ikiendeleza kampeni na uwekezaji katika mapambano dhidi ya vifo vya mama na mtoto kabla,wakati na baada ya kujifungua,takwimu za kitaifa kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya wizara ya Afya ya mwaka 2024/2025 iliyosomwa jtarehe 14.5.2024 bungeni na mjini Dodoma na waziri wa Afya Ummy Mwalimu zinaonesha kupungua kwa vifo vya akina mama kutoka vifo hai 100,000 mpaka 104.
Haya ni mafanikio katika kampeni hii ambapo kwa mujibu wa takwimu za nyuma zinaonesha kulikuwa na uwiano wa vifo vya akina mama kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mnamo mwaka 2015/16 ikilinganishwa na vifo 454 kwa kila vizazi hai 100,000 mnamo 2018.
Kwa mkoa wa Geita mwelekeo huu unaonekana kuwa chanya kulinganisha na miaka ya nyuma katika uhai wa mtoto, ambapo vifo vya watoto kati ya mwaka 2010 na 2015 ambapo kiwango cha vifo vya watoto wachanga (siku 0 mpaka 28) vimepungua kutoka vifo 40 hadi 25 kwa kila vizazi hai 1,000.
Kiwango cha vifo vya watoto wachanga mwenye umri kati ya siku 28 mpaka miezi 11 imepungua kutoka vifo 99 hadi 43 kwa kila vizazi hai1,000; na kiwango cha vifo vya watoto chini ya miaka 5 (miezi 12-59) vimepungua kutoka vifo 147 hadi 67 kwa kila vizazi hai 1,000.
Moja ya changamoto zinazowakwaza wananchi hasa kundi la akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano katika sekta ya Afya ni lugha chafu zinazotolewa na baadhi ya watoa huduma kwenye vituo vya Afya hali inayo hatarisha uhai wa mama na mtoto.
Wakazi wa kijiji cha Kikumba Itale halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita ni miongozi mwa wananchi wanaokumbana na adha hiyo kutokanana uongozi wa Zahanati ya kijiji hicho kutumia lugha chafu,na wakati mwingine kuomba fedha kwa huduma za mama mjamzito na mtoto chini ya miaka mitano.
Hayo yanajitokeza wakati serikali ya Tanzania kupitia Sera ya Afya ya 2007 kuwekeza katika kuboresha uhai wa mtoto kupitia utoaji wa huduma bure za afya kwa akina mama wajawazito na watoto chini ya miaka mitano.
Wakizungumzia hali hiyo,baadhi ya wananchi wa Kikumba Itale wamesema, mganga mfawidhi wa zahanati hiyo Cecylia Reuben ameendekeza migogoro,kutumia lugha chafu kwa wagonjwa hasa wanapofika kupata huduma wakiwa katika hali mbaya.
Yasinta Petro ni miongoni mwa wananchi walioonja machungu ya hali hiyo baada ya kupeleka mwanae wa mwaka mmoja katika zahanati hiyo akiwa na hali mbaya na kufukuzwa kwa sababu ya kusahau kadi ya kliniki ya mtoto nyumbani.
“Niliulizwa na huyo mganga kwamba, mtoto hadi anakuwa na hali hii ulikuwa wapi na kadi ya kliniki iko wapi ,ondoka nenda ufuate kadi ,kwa kweli niliondoka nikaamua kusafiri hadi Mungaza kutibiwa mwanangu”anasema Yasinta na kuongeza.
“Sasa hivi ugonjwa huwa unakuja na hodi?, badala ya mtoto kumhudumia unaulizwa maswali yasiyokuwa na msingi,tunatukanwa, tunakaripiwa, huduma ni mbovu sana, hatuoni umuhimu wa hii zahanati”
Musimu Maneno mkazi wa kitongoji cha Mwaloni ilipo zahanati hiyo anasema, tangu mganga huyo afike katika kituo hicho huduma za matibabu zimekuwa mbaya.
Anasema, mbali na kutumia lugha chafu baadhi ya akina wajawazito na watoto chini ya miaka mitano hutozwa faini ya shilingi 3,200 ilihali serikali inasema huduma kwao ni bure.
Mkazi mwingine anayefahamika kwa jina la Plakseda John amesema, kuna wakati wanakosa dawa katika zahanati hiyo licha kutakiwa kutoa fedha kiasi cha 3,200 kwa ajili ya matibabu ya watoto.
“Kuna umuhimu gani sasa,unaenda unatozwa fedha, serikali inasema huduma ni bure kwetu sisi wajawazito na watoto chini ya miaka mitano,ukishatoa hela unaambulia panado zingine unaambiwa ukanunue sasa dawa zinazoletwa na serikali zinaenda wapi?”, amehoji Plakseda.
Paulo Mashaka amesema, ili kuondokana na hali hiyo ambayo imekuwepo kwa muda mrefu serikali inapaswa kuingilia kati kufanya mabadadiliko ya uongozi ili kuwanusuru wananchi na adha wanayokumbana nayo.
“Tunaishukuru sana serikali kutujengea zahanati, lakini lugha zinazotolewa si nzuri zinatukatisha tama, maana wakati mwingine wajawazito inapofikia hali ya kujifungua hulazimika kwenda Mungaza na wanapofika huko wamechoka wanajifungua kwa upasuaji”, amesema Mashaka.
Mganga mfawidhi wa zahanati hiyo, Cecylia Reuben alipokutana na mwandishi wa habari hizi amesema ,hana mamlaka ya kuzungumza jambo lolote juu ya malalamiko ya wananchi hao bila kupewa kibali na mkurugenzi wa halmashauri hiyo.
“niliongea na viongozi wangu wa halmashauri, niwashauri muanzie ngazi ya halmashauri mkipata kibali na mimi nikapata kibali nitazungumza nazani tuliweke hivyo, fanyeni hivyo”, amesema Reuben.
Diwani wa kata ya Kigongo amesema,amehusisha jambo hilo na suala la kuelekea kwenye uchaguzi ambapo kuna makundi yanaendekeza chuki ili kuwachafua viongozi walioko madarakani.
“Tutafanya mikutano na wananchi ili kuwauliza wananchi, nimefanya mikutano hapa, hili na wananchi niliwauliza changamoto lakini hakujawahi kuulizwa jambo hili, na wananchi wanasema ni la muda mrefu, niwaombe tu mfuate utaratibu aliouelekeza mganga mfawidhi.
Mganga mkuu wilaya ya Chato Dkt.Elibariki Mollel alipotafutwa kuzungumza jambo hilo hakuweza kupatikana baada ya simu yake kutopatikana.
Usalama na uhai wa watoto kabla,wakati na baada ya kujifungua umekuwa ukiwekwa njia panda kutokana na ubora wa huduma za afya ikiwemo mazingira kati ya watoa huduma na wataalamu wa afya kwenye baadhi ya vituo vya Afya nchini