Na Mutayoba Arbogast, Kagera
NCHINI Tanzania takriban ni asilimia
47 tu ya Watoto wa wako kwenye mwelekeo wa kufikia ukuaji timilifu. Tafsiri ya
taarifa hii iliyotolewa na Idara ya Takwimu ya Taifa inafikirishau maana yake
ni takriban nusu ya Watoto wa nchini mwetu ndoto zao za kuwa madaktari,
wanasiasa, wafanyabiashara mahiri zinaweza zisitimie na hivyo, badala yake kuwa
na ongezeko kubwa la watu wazima tegemezi, vibaka na wasio na tija yoyote
kitaifa.
Leo tunuaangazia kundi ambalo
lina uwezekano mkubwa kuwa miongoni mwa hawa Watoto walio katika asilimia
53 ambao wengi wao wanakosa malezi bora kama yanavyoainishwa kwenye Programu
Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya 2021/22
hadi 2025/26 (PJT-MMMAM). Hili ni kundi ambalo watoto, kwa sababu mbalimbali,
imebidi walelewe nje ya kaya au familia zanye Baba, mama, kaka dada na ndugu
wengine wa karibu kinasaba kwenye familia, kwani hulelewa kwenye vituo maalum
kwa ajili hiyo.
Vituo vya kulelea watoto
yatima hapa nchini vinakumbwa na changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa
raslimali fedha katika kuendesha vituo hivyo na kupelekea kutomudu gharama za
kutoa chakula chenye ubora na lishe ya kutosha kwa Watoto wanaoishi huko.
Aidha, utelekezaji wa watoto wachanga katika mazingira magumu na hatarishi unaofanywa
na mabinti na wanawake, unaongeza idadi ya watoto katika vituo hivyo, hata
kusababisha ugumu katika kukidhi mahitaji ya vituo.
Lishe na ulinzi wa mtoto
miongoni mwa maeneo matano muhimu yanayotajwa kwenye PJT-MMMAM kuhitajika kwa
mtoto ili aweze kukua kufikia utimilifu wake. Maeneo mengine ni afya, elimu na
malezi yenye kuitikia mahitaji na hisia za mtoto.
Mojawapo ya vituo vinavyopitia
changamoto mbalimbali ikiwemo uhaba wa fedha katika kuendesha kituo hicho na
kuweza kuwahudumia watoto kikamilifu, sawa na au kukaribiana na watoto
wanaoishi na familia zao ni kituo cha kulelea watoto yatima kiitwacho UYACHO,
kilichoko kata ya Hamugembe, katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.
Kituo hicho chenye watoto 302
kinakabiliwa na uhaba mkubwa wa fedha kuweza kuwahudumia watoto hao kwa kile
anachoeleza mmiliki na mkurugenzi wa kituo hichò Bi Saada Selemani (90), kuwa
ni kupungua mno kwa misaada ya wafadhili na hivyo kuomba kusaidiwa kupaza sauti
yake kwa serikali na jamii kuwasaidia watoto hao.
Kwa mujibu wa PJT-MMMAM,
baadhi ya watoto wanaopata changamoto za kutengwa, kufiwa na wazazi wao au
kutelekezwa, wako kwenye hatari kubwa sana yana uwezekano kukumbwa na ukosefu
wa usalama, lishe duni na ukosefu wa huduma za afya, utoro shuleni na kukosa
watu wa karibu kuwasikiliza shida zao, hivyo programu hiyo inasisitiza kwamba
mbinu ya kutumia mifumo iliyopo kwa malezi itumike na hususan kufuata
sera na miongozo ya muktadha kama huo.
Mwezi Aprili 2021, waziri mkuu
Kassim Majaliwa, alisema kulikuwa na vituo vya kulelea watoto yatima
visivyopungua 140 nchini, vikiwa na watoto zaidi ya 24,000. Hili ni kundi
kubwa linalohitaji huduma zote stahiki kwa Watoto.
Mmiliki na mkurugenzi wa kituo hicho
cha UYACHO, Bi Saada anakumbusha, "Watoto hawa, wanahitaji
msaada mkubwa wa serikali na jamii, maana wafadhili waliokuwa wanatusaidia
wamefunga misaada yao, wanasema tujitegemee, nami ndio hivyo nimezeeka nguvu
zinapungua kuwahudumia".
Kituo hicho kilianza
kupokea na kuwalea watoto yatima na wale wenye mazingira magumu tangu mwaka
1999, ambapo baadhi ya waliolelewa hapo wamekwisha kujiimarisha kimaisha katika
nafasi mbalimbali za kujitegemea na kulitumikia taifa, huku wengine wakiendelea
na masomo ya elimu ya awali, msingi na sekondari katika shule za
Hamugembe,Nyanshenye, Istikama, Kabwoba nk za mkoani Kagera.
Anasema kwa sasa anao watoto
22 walio chini ya miaka 8 ambao wako madarasa ya awali kwenye shule za msingi.
Akiongea na waandishi habari
waliotembelea kituo hicho hivi karibuni, mkurugenzi huyo amewashukuru sana
viongozi wa mkoa, manispaa ya Bukoba na jamii kwa jumla, kwa awamu tofauti
walivyomshika mkono katika kuhakikisha kituo hicho kinaendelea kuwahudumia
watoto , lakini anaomba jitihada hizo ziwe maradufu kwa kuwa misaada ya
wafadhili imepungua mno.
"Watoto
hawa ndiwo baba na mama wa kesho, kwa hiyo tunatakiwa kuwalea kwa kuwatimizia
mahitaji yao muhimu sawa na watoto wengine, ili wakue kwa utimilifu wao, na hii
inahitaji fedha", anasema
mkurugenzi huyo.
"Niliacha
kazi katika halmashauri ya mji Bukoba, wakati ule nikiwa nina nguvu, ili niweze
kuwahudumia vyema watoto 42 niliokuwa nao wakati ule, huku nikiwa nimepewa na
serikali shamba la kulima mazao mbalimbali kama mihogo na viazi kuwalisha
watoto, sasa hivi nimezeeka sina nguvu hiyo", anasema Bi Saada kwa tabasamu huku uso wake ukiwa na alama
zote za uzee, akikumbuka enzi hizo, miaka ya 2010 wakati mkuu wa mkoa wa Kagera
wa wakati huo, Kanali Fabian Massawe, alipomkabidhi shamba la hekta 20
katika kitongoji cha Katongo, kijiji Mbale,wilayani Missenyi kwa shughuli za
kilimo, ambako sasa pia zinajenga nyumba mbili kuweza kuwajamishia baadhi ya
watoto.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464