RC MACHA AWATAKA WANAFUNZI SHINYANGA KWENDA KUIBUKA KIDEDEA MASHINDANO YA UMITASHUMTA KITAIFA MKOANI TABORA



RC MACHA AWATAKA WANAFUNZI SHINYANGA KWENDA KUIBUKA KIDEDEA MASHINDANO YA UMITASHUMTA KITAIFA MKOANI TABORA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
RC Macha
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha, amewataka wanafunzi mkoani humo ambao wamechaguliwa kwenda kuwa wakilisha Mkoa katika Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa wanafunzi wa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA)ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani Tabora, kwamba wakarudi na ushindi kwa kushika nafasi ya kwanza.

Macha amebainisha hayo leo Juni 4,2024 wakati akifunga Kambi pamoja na kuwaaga Wanafunzi wa Mkoa huo wapatao 120, ambao wamechaguliwa kwenda kuwakilisha Mkoa katika Michezo mbalimbali kwenye Mashindano ya UMITASHUMTA Kitaifa mkoani Tabora,Kambi iliyokuwa katika Chuo cha Ualimu Shinyanga (SHYCOM).
REO Ndalichako

Amesema Mashindano ya Mwaka Jana ya UMITASHUMTA Mkoa huo ulishika nafasi ya Tatu Kitaifa, hivyo kwa mwaka huu kutokana na Maandalizi mazuri walionayo na amejionea baadhi ya Michezo, wanapaswa kurudi na ushindi kwa kushika nafasi ya kwanza.

“Nendeni mkaonyeshe nidhamu ya hali ya juu, Juhudi, kuzingatia maelekezo ya Waalimu wenu, mkatulize akili zenu, mcheze kwa nguvu na kwa bidii, ili mpate ushindi katika Michezo yote na mrudi hapa Shinyanga mkiwa nafasi ya kwanza Kitaifa na kuupatia Mkoa heshima, na sisi tutawapa zawadi,”amesema Macha.
“Nawasihi pia mkiwa huko Tabora msikubali kufanyiwa vitendo viovu, wala kukubali kushikwa katika maeneo yasiyofaa bali mseme “Don’t Touch Me’pamoja na kutoa taarifa kwa walimu juu ya watu ambao wanataka kuwafanyia vitendo hivyo,”ameongeza.

Amewataka Pia Walimu wakawe Wazalendo pamoja na kujenga vipawa vya watoto hao, ikiwa Michezo ni Ajira licha ya kuimarisha Afya.
Katika hatua nyingine amewaagiza Wakurugenzi wote wa Halmashauri mkoani humo, kwamba kila Mmoja avilinde Viwanja vya Michezo Shuleni ili visivamiwe, na kutojenga katika maeneo hayo ya Viwanja, ili kila shule kuwepo na Viwanja vya Michezo.

Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga Dafroza Ndalichako, akisoma taarifa kwa Mkuu wa Mkoa,ametaja idadi ya wanafunzi ambao wamechaguliwa kuwakilisha Mkoa wa Shinyanga kwenye mashindano ya UMITASHUMTA Kitaifa Mkoani Tabora kuwa wapo 120,Walimu wa Michezo 15, Mratibu wa Michezo Mmoja na Daktari wao.
Amesema wanafunzi hao wataondoka kesho kwenda Tabora kwa ajili ya Mashindano hayo ya Kitaifa ya UMITASHUMTA kwa kushiriki Michezo mbalimbali ikiwamo ya Riadha, Mpira wa Kikapu, Pete, Miguu, Mikono, Wavu, Nyimbo za kizazi kipya pamoja na utamaduni wa Ngoma.

Aidha, ametaja Changamoto ambazo walikabiliana nazo katika Mashindano ya UMITASHUMTA kuanzia ngazi za wilaya, kwamba kuna upungufu wa Viwanja vya Michezo, hasa katika Shule za Manispaa, Vifaa vya Michezo pamoja na ufinyu wa Bajeti.
Nao baadhi ya wanafunzi hao akiwamo Grace Boazi kutoka Halmashauri ya Msalala ambaye alishinda ngazi ya Mkoa kwa konyesha kipaji cha kuimba nyimbo za kizazi kipya, wamemuahidi Mkuu huyo wa Mkoa, kwamba watakwenda kufanya vizuri na kurudi na ushindi kwa kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.

Kauli Mbiu katika Mshindano hayo ya UMITASHUMTA mwaka huu inasema “Miaka 50 ya UMITASHUMTA tunajivunia Mafanikio katika Sekta ya Elimu,Michezo na Sanaa, Hima Tanzania shiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024”.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akipiga picha ya pamoja na Wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akipiga picha ya pamoja na Wanafunzi.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha akipiga picha ya pamoja na Walimu wa Michezo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464