WANAUME KAGONGWA WAWEKA AZIMIO LA KUPINGA UKATILI WA KIJINSIA
Salvatory Ntandu,KAHAMA
Wanaume katika Mji mdogo wa Kagongwa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga wameweka azimio la pamoja la kupinga Ukatili wa Kijinsia kwa Wanawake, Watoto na Watu Wenye ulemavu ili kutokomeza vitendo vya ukatiki vinatajwa kuleta athari mbalimbali kwa wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.
Azimio hilo linalenga kutoa elimu ya kuachana na Mila na tamaduni potofu, kwa kushirikisha makundi ya Vijana, Waendesha pikipiki, Wazee wa mabaraza, Waganga wa tiba asili, Viongozi wa kimila na Viongozi wa Dini ambao wana nafasi kubwa ya kukutana na jamii.
Akiongoza kiapo hicho katika kikao cha Pamoja kilichowakutanisha Wanaume na vijana na Maafisa kutoka Idara ya Maendeleo ya Jamiii Manispaa ya Kahama, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia kituo cha Polisi Kagongwa Joseph Kyakalaba amesema Azimio hilo litasaidia kupunguza matukio ya ukatili kwenye jamii.
Amesema endapo Makundi hayo yakiliweka azimio hilo kama ajenda katika vikao wanavyokaa na Wananchi katika maeneo yao itasaidia kuondoa matukio ya ukatili kwa Wanawake, Watoto na Watu wenye ulemavu ambayo hufanyika kwa siri na wanaohusika ni wanaume kwa sehemu kubwa.
Awali akiongoza Majadiliano katika kikao hicho cha Wanaume wa Kata ya Kagongwa Afisa Maendeleo ya jamii Manispaa ya Kahama Abrahaman Nuru, amesema Mila na tamaduni kandamizi zinaongoza kusababisha ukatili wa kijinsia kwa Wanawake,Watoto na Watu wenye ulemavu.
"Viongozi wa dini na Kimila Msifungishe ndoa Watoto wa kike chini ya umri wa miaka 18, Wazazi acheni tamaa za Mali hakikisheni mnawapatia haki zao za Msingi kama vile elimu ili waweze kutimiza ndoto zao na baadae waweze kuwasaidia,"amesema Nuru.
Kwa upande wake Joseph Mbasha kutoka Shirika la HelpAge Tanzania ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa CHAGUO LANGU HAKI YANGU ndani ya shirika, amesema wameamua kukutana na Wanaume katika wa Kagongwa ili kutafuta muafaka wa kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia kwa Wanawake.
"Upo ukatili wa kiuchumi unaotekelezwa na baadhi ya Wanaume, ikiwemo kuwanyima fursa wanawake za kushiriki katika uzalishaji; kutelekeza familia zao hasa baada ya kuvuna mazao na kuhamia mjini hali inayosababisha Wanawake kushindwa kuhudumia familia peke yao, na kusababisha Watoto kukosa chakula na huduma zingine za msingi. Hivyo kupitia kikao hiki naomba muwe mabalozi,"amesema Mbasha.
Nae Mwakilishi wa Waganga wa tiba asili, Jongela Heneriko amesema vitendo vya baadhi ya Wazazi kuwaleta mabinti zao kwaajili ya kuwaogesha dawa za mvuto wa Mapenzi (SAMBA) unachangia kusababisha baadhi yao kujiingiza katika vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo.
"Azimio hili kwetu itakuwa suluhu ya utoaji wa dawa za (SAMBA) Wazazi watakowaleta Watoto hatutawahudumia na badala yake tutatoa taarifa kwa Serikali, ili kuwanusuru watoto wa kike na ukatili huu. Pia, tuwaombe Wazee wa Kagongwa waache kuoa mabinti wadogo,"amesema Heneriko.
Nae Mwenyekiti wa Baraza kuu la Waislam kata ya Kagongwa Sheikh, Mustach Salum amewaomba viongozi wa dini kupitia nyumba za ibada kuweka ajenda za kudumu ya elimu juu ya vitendo vya ukatili wa kijinsia kwa waumini wao kila wanapokutana Bili kutomeza matukio hayo kwenye jamii.
"Sisi tunanafasi kubwa ya kuleta mabaliko kwenye jamii hebu tuibebe ajenda hii Kikamilifu kila Ibada tuongelee hata kwa dakika 10 suala la ukatili wa kijinsia kwa waumini wetu itasaidia kuondoa mitazamo hasi juu ya kundi hili ambalo limeathirika kwa kiasi kikubwa,"amesema Salum.