RC MACHA AKAGUA MIRADI UJENZI WA BARABARA WILAYANI KAHAMA,ATOA MAELEKEZO UANDISHI WA MABANGO


Na. Paul Kasembo. KAHAMA MC.

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha amekagua utekelezaji wa ujenzi wa miradi ya barabara wilayani Kahama huku akitoa maelekezo kwamba Mabango yote yanayotambulisha miradi inayotekelezwa ndani ya Mkoa wa Shinyanga yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili au yawepo mabango mawili, moja lianze kwa kiswahili na la pili liandikwe kwa lugha ya kiingereza iwapo kuna ulazima huo huku akisisitiza kuwa yataje aina ya mradi, gharama za mradi, muda utakaotumika kutekeleza mradi, jina la mwajiri/mlipaji na jina la mkandarasi lengo ni kuwafanya wananchi kujua Serikali yao inavyowaja, kuthamini lugha yao, na kuwezesha wao kuwa sehemu ya umiliki wa mradi husika na kwamba utekelezaji wa maelekezo haya uanzie kwenye ujenzi wa barabara ya Kahama - Kakola km 74.

RC Macha amefanga ziara hiyo jana ya kukagua utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa barabara za katikati ya Mji (CBD), barabara za eneo la Viwanda la Zongomela na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua ya Chalsea - Lyazungu na Shunu - Magobeko zote za hapa Kahama Manispaa unaotekelezwa na Mkandarasi Sichuan Road and Bridge (Group) Corporation Ltd ya Jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya Tzs. Bil 20.864 kwa muda wa miezi 15.




"Nirudie tena kuwaelekeza wataalam wetu kuwa, kwa maslahi mapana ya wananchi wetu na Watanzania kwa ujumla Mabango ya miradi yote ndani ya Mkoa wa Shinyanga yaandikwe kwa lugha ya Kiswahili ili waweze kuelewa nini kinafanyika katika maeneo yao, na pia mabango hayo yaeleze kila kitu ikiwemo gharama za mradi, muda utakaotumika kutekeleza, jina la mlipaji, jina la mkandarasi maana kwa kufanya hivi itasaidia sana kuwa na uelewa wa pamoja na wananchi kujua Serikali yao inawathamini na wao kuwa sehemu ya mradi husika," amesema RC Macha.




Mkandarasi huyu anatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara za katikati ya mji(CBD), Barabara eneo la Viwandani Zongomela na ujenzi wa mifereji ya maji ya mvua mitaa ya Chelsea, Lyazungu na Shunu kwa zaidi ya Tzs. Bil 20 kwa muda wa miezi 15. Ujenzi huu wa barabara wenye urefu wa km 12 unatokana na Programu ya Uboreshaji wa Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC) ambapo Manispaa ya Kahama ni mnufaika umefikia asilimia 22.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464