UMOJA WA WAZEE MASANGA WILAYANI KISHAPU WAZINDULIWA,SERIKALI YAWAHAKIKISHIA WAZEE KUENDELEA KUWAPATIA HUDUMA BORA ZA MATIBABU
DC Mkude akikata utepe kuzindua Ofisi ya Umoja wa Wazee Masanga wilayani Kishapu.
UMOJA wa Wazee Kata ya Masanga wilayani Kishapu, umezinduliwa Rasmi,huku Serikali ikiwahakikishia Wazee kuendelea kuwapatia huduma bora za matibabu bure.
Umoja huo umezinduliwa leo Juni 15,2024 na Mgeni Rasmi Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude, na kushuhudiwa na viongozi mbalimbali wakiwamo Maprofesa na viongozi wa Jumuiya ya Maridhiano ya Amani Mkoa wa Shinyanga.
Mkude akizungumza kwenye uzinduzi wa Umoja wa Wazee Masanga, amempongeza Muasisi wa Umoja huo Profesa Emmanuel Shija ambaye ni Mkurugenzi wa Outreach Care International (OCI) mzaliwa wa Masanga, kwa kukumbuka nyumbani na kuwaunganisha wazee.
Amesema Serikali itakuwa pamoja na Umoja huo wa Wazee Masanga wilayani Kishapu, pamoja na kuendelea kutatua changamoto mbalimbali ambazo zinawakabili Wazee ikiwamo upatikanaji wa matibabu bure kwa Wazee.
Prof; Emmanuel Shija akizungumza kwenye uzinduzi Umoja wa Wazee Masanga Kishapu.
“Leo tumezindua Umoja wa Wazee hapa Masanga wilayani Kishapu, na Serikali tutaendelea kuboresha huduma za Afya kwa wazee ikiwamo upatikanaji wa Matibabu bure,dawa za Magonjwa ya Wazee na utengwaji wa Madirisha,"amesema Mkude.
"Wazee wale ambao bado hamjachukua Vitambulisho vya kupata Matibabu bure nendeni mkachukue ili muendelea kupata matibabu bure ,"ameongeza Mkude.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamis.
Pia amewasihi Wazee wilayani humo, kwamba wajitokeze kwa wingi kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao utafanyika mwaka huu, iliwakachague viongozi makini wenye kuwaletea Maendeleo.
Katika hatua nyingine Mkude, ameipongeza Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga, kwa kuhakikisha Amani inaendelea kutawala mkoani humo, na hata matukio ya mauaji ya reja reja yakiwamo ya Wazee wilayani Kishapu hayapo tena.
Mwekahazina wa Umoja wa Wazee Masanga Elizabeth Jimola akisoma Risala.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania Mkoa wa Shinyanga Sheikh Balilusa Khamis, ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwashirikisha kwa kila jambo, hali ambayo imesaidia Amani ya Mkoa huo kuendelea kutawala pamoja na kukomesha Mauaji ya Wazee yatokanayo na Imani za Kishirikina, na hata Mimba na ndoa za utotoni zimepungua siyo kama ilivyokuwa hapo awali.
Naye Mwekahazina wa Umoja wa Wazee Masanga Elizabeth Jimola, akisoma Risala kwa niaba ya Mwenyekiti wa Umoja huo, amesema ulianzishwa mwaka jana kwa kuasisiwa na Prof; Emmanuel Shija, na sasa wapo wanachama 9, na Marengo yao ni kuanzisha Miradi ya kujikwamua kiuchumi ili waondokane na umaskini.
Elizabeth ambaye pia ni Diwani wa Vitimaalum wilayani Kishapu,ametaja Marengo mengine kuwa ni kuhakikisha vijana wanakuwa na maadili, uzalendo na kulipenda Taifa lao, kulinda na kudumisha Amani ya Nchi,pamoja na kuunga Mkono Juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na kuwaletea Maendeleo wananchi.
Aidha, ameipongeza pia Serikali kwa kuendelea kuwajali Wazee na hata kuwaboreshea huduma za matibabu bure, upatikanaji wa Madawa pamoja na kuwatengea Madirisha yao kwenye huduma za Afya na kupata matibabu bila usumbufu.
Katika hafla hiyo ya uzinduzi wa Umoja wa Wazee Kata ya Masanga, kabla ya hapo walitembelea shule ya Msingi Masanga ambayo alisoma Prof Emmanuel Shija mwaka 19873 na kuhitimu 1980, na kuahidi kuikarabati, pia likafuatiwa na zoezi la utoaji wa Tuzo za Utumishi uliotukuka.
Waliopewa Tuzo hizo ni Dk. John Ndani, Alex Shija, Askofu Amos Ndatulu, Peter Kitang’wa, Sheikh Balilusa Khamis, Victoria Mkumbwa, Osca Rutengo, Elizabeth Jamila, Charles Emmanuel, Mark Leveri, TCRS pamoja na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga, huku akikambatana na utoaji wa Zawadi kwa viongozi mbalimbali akiwamo Mkuu wa wilaya ya Kishapu.
TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA HAPA CHINI👇👇
Zoezi la Utoaji wa Tuzo ya Utumishi uliotukuka likiendelea.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude akipewa Zawadi.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Picha za pamoja zikiendelea kupigwa.
Picha za pamoja zikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464