KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT SAMIA YAWASILI SHINYANGA KUTOA HUDUMA ZA MATIBABU KWA WANANCHI


KAMBI YA MADAKTARI BINGWA WA RAIS DKT SAMIA YAWASILI SHINYANGA KUTOA HUDUMA ZA MATIBABU KWA WANANCHI

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
Mratibu  wa Kambi ya Madaktari Bingwa Dkt. Everine Maziku kutoka Idara ya Afya,Uzazi,Mama na Mtoto Wizara ya Afya.

KAMBI ya Madaktari Bingwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ya kutoa huduma za matibabu ya kibingwa kwa wananchi, imewasili mkoani Shinyanga tayari kwa kutoa huduma kwa wananchi wa Mkoa huo na kuimarisha Afya zao.

Madaktari hao Bingwa wamewasili leo Juni 17,2024 ambao watatoa huduma za kibingwa kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga, katika Halmashauri zote Sita za Mkoa huo kwa muda wa Siku Tano hadi Juni 22.
Muuguzi Mkuu Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga Frola Kajumla.

Mratibu wa Timu hiyo ya Madaktari Bingwa Dkt. Everine Maziku kutoka Idara ya Afya,Uzazi,Mama na Mtoto Wizara ya Afya, amesema Madaktari hao wapo 30, na watawafikia wananchi wote ambao watafika kupatiwa huduma hizo za kibingwa.

Amesema tangu Madaktari hao waanze kutoa huduma hizo za kibingwa, tayari wameshafika katika Mikoa 20 na kutoa huduma za Matibabu kwa wananchi zaidi ya Elfu 50, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma za Afya wapatao 3500.
Mratibu Afya Mama na Mtoto Mkoa wa Shinyanga Halima Hamis.

“Huduma ambazo zitakuwa zikitolewa na Madaktari hawa Bingwa ni Magonjwa ya Wanawake,Watoto, Upasuaji,Mkojo,Ganzi,Usingizi, Macho, Mifupa, Mionzi na Magonjwa ya Ndani,” amesema Dk.Everine.
Muuguzi Mkuu Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga Frola Kajumla, akizungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk.Yudas Ndungile, amemshukuru Rais Samia kwa kufikisha Timu hiyo ya Madaktari Bingwa katika Mkoa huo, na kuwafikia wananchi hadi wa pembezoni kupata huduma za kibingwa na kuimarisha Afya zao.

Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wa Mkoa wa Shinyanga, wajitokeze kwa wingi kwenye Kambi za Madaktari hao Bingwa, ambao wamesambaa kwenye Halmashauri zote ili wapate matibabu ya kibingwa.
Nao baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wamemshukuru Rais Samia, kwa kuendelea kujali wananchi wake kwa kuhakikisha wanaendelea kuwa na Afya Njema, kwamba licha ya kuboresha huduma za Afya nchini, bado ameendelea kuwapelekea na Madaktari Bingwa hadi pembezoni mwa Miji.
Picha ya pamoja ikipigwa.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464