Header Ads Widget

HATIMAYE ZAHANATI YA MWAMAGUNGULI IMEANZA KUJENGWA BAADA YA KUSHINDIKANA MIAKA 14

Hatimaye Zahanati ya Mwamagunguli imeanza kujengwa baada ya kushindikana miaka 14

Na Marco Maduhu,SHINYANGA

UTAWALA bora ni pamoja na uwajibikaji kwa viongozi wa Serikali dhidi ya jamii, na kuwatatulia matatizo yao mbalimbali.
Muonekano wa Zahanati ya Mwamagunguli ikiwa inajengwa.

Hali hiyo imejidhihilisha katika Kijiji cha Mwamagunguli Kata ya Kolandoto Manispaa ya Shinyanga,ambapo Serikali mara baada ya kuona habari kupitia Mtandao huu mwezi Marchi mwaka huu, kwamba Zahanati ya Kijiji hicho imechukua miaka 14 kushindwa kukamilika kutokana na kuanza kujengwa na wananchi mwaka 2010 kwa nguvu zao wenyewe,ndipo ikaamua kuchukua hatua.

Sera ya Afya ya mwaka 1990 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2007 inasema Serikali itashirikisha wananchi katika kuimarisha huduma za Afya ngazi zote, na kwamba kila Kijiji inapaswa kuwa na Zahanati na Kituo cha Afya kwa Kila Kata.
Awali Zahanati ilivyokuwa.

Sera hiyo inasema, wananchi watashiriki kuanzisha ujenzi wa boma hadi kufika hatua ya Renta, ndipo Serikali itamalizia ujenzi huo, hali ambayo ilikuwa tofauti kwa wananchi wa Kijiji cha Mwamagunguli ndani ya miaka 14 Zahanati yao ilishindwa kukamilishwa na Serikali, lakini sasa imeanza kujengwa na ipo hatua ya mwisho.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwamagunguli Makoye Shindayi, anasema walipokea fedha Sh,Milioni 50 kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Aprili mwaka huu kwa ajili ya kumalizia boma la ujenzi wa Zahanati Kijijini humo na sasa ujenzi unaendelea.

Amesema anaishukuru Serikali kwa kusikia kilio chao cha muda mrefu juu ya kuikamilisha Zahanati hiyo,ambayo ni hitaji kubwa la wananchi kwa kuwasogezea huduma za Matibabu kuwa karibu.

“Kwanza kabisa nakupongeza Mwandishi wa habari kwa kufika hapa Kijijini Mwezi wa tatu na kutuhoji Juu ya Boma hili la Zahanati yetu kuchukua miaka 14 kushindwa kukamilika, bila wewe kuirusha taarifa hii huande hata ujenzi usinge anza, lakini Serikali imesikia kilio chetu kupitia wewe na ikatoa Pesa Milioni 50, na sasa kama unavyoona ujenzi unaendelea,”anasema Shindayi.

Mwananchi Salome Ndaki, anasema kukamilika kwa Zahanati hiyo na kuanza kutoa huduma itawasaidia kupata huduma karibu hasa akina Mama Wajawazito ambao wamekuwa wakipata tabu kutembea umbali mrefu kwenda kujifungua katika Hospitali ya Kanisa la AICT Kolandoto,lakini sasa shida hiyo wataondokana nayo.

Anasema Mfano mtu akiugua ghafla au Mjazito kupata uchungu wakati wa usiku, inakuwa shida kumpeleka hadi Hospitali ya Kolandoto ambayo ipo mbali,lakini Zahanati hiyo ikianza kutoa huduma watakuwa nayo karibu na kupata matibabu haraka na kuokoa Afya zao.

“Tunaishukuru Serikali kwa kuanza kutukamilishia Zahanati yetu hapa kijijini na itakuwa msaada mkubwa kwetu, hasa sisi wanawake ambao ndiyo hua tunauhitaji mkubwa wa huduma za Afya,”anasema Salome.

Mwananchi mwingine Hollo Jidula, anasema kukamilika kwa Zahati hiyo ni faraja kwao sababu watapa huduma mbalimbali za kiafya, ikiwamo elimu ya Afya ya uzazi na uzazi wa Mpango, huduma ambazo walikuwa hawazipati katika Hospitali ya AICT Kolandoto, kutoka na Sera za Kanisa kutotoa huduma hizo tofauti na Hospitali za Serikali.

“Sisi kuwa na Zahanati yetu hapa Kijijini ni faraja kubwa hasa kwa wanawake, sababu tutapata elimu mbalimbali zinazohusu masuala ya afya ya uzazi na uzazi wa mpango, sababu Hospitali ya Kanisa haina huduma hizi,”anasema Hollo.

Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii Kijijini humo Ester Emmanuel, anasema kukamilika kwa Zahanati hiyo ni Mkombozi kwa wajawazito ambao wanaondokana na adha ya kujifungulia njiani na kuhatarisha maisha yao na Mtoto.

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk.Elisha Robert anasema Zahanati hiyo ya Mwamagunguli, itasaidia kuboresha upatikanaji wa huduma za Afya kwa wananchi wa eneo hilo.

Anasema ujenzi wa Zahanati hiyo kwa sasa ipo hatua ya mwisho, na tayari wameshapokea fedha za Vifaa Tiba Sh,Milioni 100 ikiwamo na Zahanati ya Mwagala, na kwamba kati ya Mwezi Julai hadi Agosti inaweza kufunguliwa na kuanza kutoa huduma za matibabu.

“Zahanati hii ikishakamilika kujengwa, ambapo tayari Serikali imeshatupatia Sh.Milioni 100 kwa ajili ya kununua Vifaa Tiba ikiwamo na Zahanati ya Mwagala, tutakacho kifanya ni kuhamisha Watumishi wachache waende kwenye Zahanati hiyo ili huduma zianze kutolewa,”anasema Dk.Elisha.

Diwani wa Kolandoto Mussa Andrew, anaishukuru Serikali kwa kumuunga Mkono kuikamilisha Zahanati hiyo, na kwamba itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa kijiji hicho kupata huduma za matibabu karibu na maeneo yao.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga Alexius Kagunze,anasema kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali kuu imetoa kiasi cha fedha Sh.milioni 50 ili kukamilisha ujenzi wa Zahanati hiyo ya Mwamagunguli,na fedha hizo zilishapelekwa sehemu husika na ujenzi unaendelea hadi sasa.

Post a Comment

0 Comments