Header Ads Widget

MKUU WA WILAYA YA SHINYANGA JULIUS MTATIRO AWAHAKIKISHIA WANANCHI KUPUNGUZIWA BILI ZA MAJI






Na Mapuli Kitina Misalaba

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga Wakili Julius Mtatiro amewahakikishia wakazi wa kata za Tinde, Iselamagazi na Didia wilayani Shinyanga kuwa maombi yao ya kupunguziwa bei za maji yanashughulikiwa na kwamba siku zijazo wataanza kulipia bili za maji kama watumiaji wengine wa Manispaa ya Shinyanga.

Ameyasema hayo jana baada ya kupokea kero na malalamiko mbalimbali kwa wananchi katika mkutano wake wa hadhara ambao umefanyika katika uwanja wa shule ya msingi Tinde, ambapo wananchi wamesema kuwa muda mrefu wamekuwa wakilipia Shilingi 2500 unit tofauti na maeneo mengine ya Manispaa ya Shinyanga.

Amesema suala hilo lipo hatua za mwisho ambapo amewatoa hofu wakazi wa kata za Didia, Iselamagazi pamoja na Didia kuwa siku zijazo wataanza kulipa bei za maji kama watumiaji wa kata zingine za Manispaa ya Shinyanga.

“Suala la maji kwa kifupi limefika hatua za mwisho toka nilipotoa yale maelekezo kwenye mkutano pale Didia kwamba bei za maji kwenye kata za Iselemagazi, Tinde na Didia zishushwe kutoka shilingi 2500 kwa Unit mpaka elfu 1400 na kama ambavyo mjini wanalipa baada ya wananchi kuniambia zaidi ya Miaka miwili wamekuwa wakilipa elfu 2500 huku mjini wakilipa elfu 1400 na kwahiyo tulitoa maelekezo lakini maelekezo yale niliyatoa baada yangu mimi kuwasiliana na Mhe. Mbunge na Mhe. Waziri Awezo tukakubaliana ndiyo maana kwenye ule mkutano niliwaelekeza EWURA wakamilishe huo mchakato ambao kwa Miaka miwili umekuwa haukamiliki lakini baada ya agizo la juzi huo mchakato umeshakamilika”.

“Mara ya mwisho nilipokuwa Dodoma niliwaziliana tena na Mhe. Awezo nikiwa na Mhe. Mbunge na tulipofika pale wizarani Mhe, Awezo akatuonyesha amekwisha pokea barua kutoka EWURA bodi ya EWURA imeidhinisha kushusha bei za maji kwenye kata za Tinde, Didia na Iselemagazi na baada ya hapo wiki iliyoisha SHUWASA wamenifuata ofisini wakiwa wamepokea barua kutoka kwa Mhe. Waziri ya agizo la kushusha hizo bei kwa mujibu wa sheria ile barua inavyotoka kwa waziri kinachofuatia ni kutangaza kwenye gazeti la serikali”.amesema DC Mtatiro

Mkuu wa Wilaya huyo akiwa anaendelea na mkutano wake amempigia simu meneja wa EWURA Kanda ya Magharibi Mhandisi Walter Christopher ambaye pia ametoa ufafanuzi kuhusu suala hilo.

“Ombi tayari nimeshapitishwa na bodi ya EWURA la kufanya bei ziwe sawa katika eneo la Shinyanga sasa hivi tumeshapeleka kwenye gazeti wakishaturudishia ndiyo tunatoa kwa ajili ya utekelezaji kwahiyo tunaimani Mwezi huu wa sita wataanza na hiyo bei ambayo ni sawa na wengine”amesema Mhandisi Christopher

Pamoja na mambo mengina wakazi wa kata ya Tinde wametaja changamoto na kero mbalimbali zilizopo ikiwemo changamoto ya ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji , stendi pamoja na ukosefu wa maji katika mnada wa Tinde. Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Stewart Makali ametolea ufafanuzi kuwa changamoto hizo zinashughulikiwa ili kuwaepusha na usumbufu unaojitokeza.



Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Stewart Makali akitolea ufafanuzi kero za wananchi katika mkutano wa hadhara leo.Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Stewart Makali akitolea ufafanuzi kero za wananchi katika mkutano wa hadhara leo.




Post a Comment

0 Comments