CAMFED IMETOA MAFUNZO YA STADI ZA MAISHA KWA WATENDAJI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA SHINYANGA
Shirika lisilo la Serikali la Campaign for Female Education (CAMFED) limetoa mafunzo ya stadi za maisha kwa Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule Za Sekondari, Walimu wa Unasihi Shuleni na Mratibu wa Mradi ngazi ya Halmashauri.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia Juni 10 hadi Juni 11, 2024 katika ukumbi wa Halmashauri uliopo Iselemagazi na yanalenga kuwajengea uwezo makundi hayo ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea kujifunza kwa umahiri na kukabiliana na changamoto zinazoweza kusababisha wasiendelee na masomo.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Bw. Stewart Makali, Mkuu wa Divisheni ya Elimu Sekondari kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga amesema Halmashauri iko tayari kushirikana na wadau hao katika kuhakikisha ulinzi wa watoto katika jamii.
Naye Mwezeshaji wa Mafunzo hayo, Bw. Filoteus Nombo akiwasilisha kuhusu dhana ya CAMFED amesema, shirika hilo lilianzishwa nchini Tanzania mwaka 2006 likiwa na lengo la kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu ili kutimiza ndoto zake. Kwa sasa CAMFED inafanya kazi na Ofisi ya Rais TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sanyansi na Taknolojia katika mikoa 10. Mikoa hiyo ni Shinyanga, Singida, Mwanza, Tabora, Iringa,Dodoma,Tanga, Morogoro, Pwani na Dar es Salaam.
Kwa upande wake Bw.Patrick Mwalyepelo, mwezeshaji wa mada ya elimu ya stadi ya maisha amesema program ya elimu ya stadi ya maisha inalenga kumjengea mwanafunzi uwezo wa kutambua mahitaji yake ya kisaikolojia na kifizikia ili aweze kufanya vizuri kimasomo na kimaisha. Elimu hiyo imelenga pia kuongeza mahudhurio na ufaulu shuleni.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464