Header Ads Widget

RC MACHA AWASHAURI WANANCHI SHINYANGA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA


RC MACHA AWASHAURI WANANCHI SHINYANGA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA

Na Marco Maduhu,SHINYANGA
MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha,amewashauri wananchi mkoani humo kujenga utamaduni wa kupima Afya zao mara kwa mara, huku akimpongeza Mheshimiwa Rais Dk, Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya nchini.

Macha amebainisha hayo leo Juni 18,2024 wakati alipotembelea kuona Maendeleo ya ujenzi wa uboreshaji wa Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga,pamoja na utoaji huduma za Afya kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Rais Dk. Samia ambao wanaendeleo na utoaji wa matibabu ya kibingwa kwa wananchi wa Mkoa huo.
Amesema wananchi wengi wamekuwa wakisumbuliwa na Magonjwa na kufikia katika hatua mbaya, hali ambayo inasababishwa na kutopima Afya mara kwa mara, ili kupata ushauri wa Daktari kwa kulinda Afya au kuanza Tiba mapema.

“Wananchi nimeona mmejitokeza kwa wingi kuja kupata Matibabu kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Mheshimiwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan, hivyo natoa wito kwa wananchi wa Shinyanga mjenge tabia ya kuchunguza Afya zenu mkiwa bado wazima na siyo kusubili hadi mnakuwa katika hali mbaya,”amesema Macha.
“Mkipima Afya zenu mapema itawasaidia kujua hali zenu, na ukibainika unatatizo unaanaza matibabu mapema na kupona, Mfano Magonjwa haya ya Saratani ya Matiti na Shingo ya kizazi ukiwahi matibabu mapema unaweza kupona kabisa,”ameongeza Macha.

Aidha, amesema katika Mkoa huo watapanga namna ya kuweka utaratibu wa wananchi wawe wanapima afya zao mara kwa mara, huku, akiwataka pia wananchi wakate Kadi za Bima za Afya ambazo zitawasaidia kupata matibabu kwa urahisi bila ya kuingia gharama kubwa na kuokoa Afya zao.
Katika hatua nyingine amempongeza Rais Samia kwa kutoa fedha na kuboresha huduma za Afya nchini, ikiwamo na Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga, ambayo kwa sasa ujenzi wake unakwenda kukamilika kwa Jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD),Majengo ya upasuaji na Wodi.

Naye Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk.Elisha Robert, amesema ujenzi wa uboreshaji wa Hospitali hiyo ya Manispaa ya Shinyanga utakamilika Juni 30 mwaka huu.
Nao baadhi ya wananchi wa Shinyanga, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za Afya, huku wakiwaletea pia Madaktari Bingwa na kuwapatia Matibabu ya Kibingwa na kuimarisha Afya zao.

TAZAMA PICHA UKAGUZI UBORESHAJI UJENZI HOSPITALI YA MANISPAA SHINYANGA👇
Muonekano Jengo la Wagonjwa wa Nje OPD.
Ukaguzi ukiendelea uboreshaji ujenzi Hospitali ya Manispaa ya Shinyanga.

Post a Comment

0 Comments