Wanafunzi wa darasa la Awali katika shule ya msingi Mwenge iliyopo Manispaa ya Shinyanga
Na Kareny Masasy
MSAKO wa kuwapata watoto wenye umri wa miaka mitano walioanzishwa vituo vya kulea watoto mchana (daycare centre) badala ya kuanzishwa darasa la awali limepata mafanikio manispaa ya Shinyanga nakufikia uandikishaji asilimia 100.
Manispaa hiyo mpaka kufikia Mwezi Marchi 2024 uandikishaji ulikuwa umefikia asilimia 85 huku lengo la uandikishaji likiwa asilimia 100.
Kaimu ofisa elimu Manispaa ya Shinyanga Grace Kuzanza anasema uandikishaji mpaka sasa wanafunzi wanaosoma darasa la awali na darasa la kwanza ulienda ukiongezeka baada ya msako kufanyika.
Kuzanza anasema uandikishaji wa darasa la awali kwa mwaka jana ulifikia asilimia 105 na mwaka huu umefikia asilimia 100 ambapo wavulana asilimia 97 na wasichana asilimia 103.
Kuzanza anasema kuanzia mwezi Oktoba 2023 hadi March 2024 wanafunzi walioandikishwa ni 5059 wavulana ni 2457 na wasichana ni 2602 wakiwemo walemavu wasichana watatu na wavulana wanne sawa na asilimia 85 .
“Maoteo ya uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la awali kwa mwaka 2024 ni wanafunzi 5947 wasichana 3000 na wavulana 2,947 na sasa imefikia lengo lililo kusudiwa”anasema Kuzanza.
Mwenyekiti wa vituo vya kulea watoto mchana Manispaa ya Shinyanga Damari Msuya anasema kweli vituo vinasaidia kulea watoto lakini wamiliki waangalie wa umri gani wanaohitajika kwa mujibu wa sheria wasiangalie pesa.
Baadhi ya wazazi watoto wao waliokuwa wamepelekwa kwenye vituo vya kulea watoto Amos Kulwa na Meridan Haule wameridhia waanze darasa la awali kwa mujibu wa sheria ya Elimu na Mafunzo.
Haule anasema wazazi wanatakiwa kupewa elimu kwani wengine sio makusudi ni uelewa tu hivyo msako wa kwenye vituo vya kulea watoto utasaidia kujua umri gani mtoto aanze darasa la awali.
Meneja wa shirika lisilo la kiserikali la Investing Children Societies (ICS) mkoa wa Shinyanga Sabrina Majikata anasema umuhimu wa darasa la awali ni kumuandaa mtoto katika ujifunzaji wa maendeleo katika ukuaji wake na kituo cha kulelea watoto ni kucheza kwa kadri ya umri wa mtoto kuanzia miaka miwili hadi minne.
“Mtoto anapozaliwa tu ubongo wake unakuwa umefikia asilimia 25 katika ukuaji wake na anapofikisha umri wa miaka mitano unakuwa kwa asilimia 92 hivyo darasani anaendelea kujifunza zaidi vitu mbalimbali kupitia nyimbo na michezo”anasema Majikata.
Majikata anasema mtoto anatakiwa kuanzishwa darasa la awali akiwa na umri wa miaka mitano na akifikisha umri wa miaka sita aanze darasa la kwanza lakini mzazi analazimisha huko kwenye vituo aanze pia kufundishwa kusoma na kuandika.
“Mzazi unaposhindwa kumpeleka mtoto shule umri unaotakiwa tayari umeanza kumnyima haki yake ya elimu ambayo anatakiwa kuipata akiwa mdogo”anasema Majikata..
Sera ya elimu ya mwaka 2014 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016 inaeleza darasa la awali kuwa Mwalimu mmoja na wanafunzi 25 tu.
Mwalimu mkuu wa shule ya msingi Mwenge Hemed Hussein anasema Mwitikio wa darasa la awali kwa shule hiyo umekuwa mzuri sababu maoteo kwa mwaka huu yalikuwa wanafunzi 130.
“Wazazi waliendelea kuleta watoto wao kutoka maeneo mbalimbali mpaka wamefika wanafunzi 300 mpaka kufunga shule” anasema Hussein.
Kwa Mujibu wa Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009 na sera ya Maendeleo ya Mtoto ya Mwaka ya Mwaka 2008 ni kuhakikisha mtoto anaandikishwa shule na kufuatilia maendeleo yao kwa kuwapatia mahitaji yote ya shule.
Katika Programu Jumuishi ya Taifa ya Maendeleo ya Awali ya Mtoto PJT-MMMAM inaeleza Tanzania ni nchi ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kwenye elimu ya awali kuifanya kuwa ya lazima.
Katika sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 na maboresho yake ya mwaka 2016 kuwa elimu bila malipo na kujumuisha elimu ya msingi kuzita shule zote kuwa na darasa la elimu ya awali kwa watoto wenye umri wa miaka mitano.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464