Usalama wa watoto barabarani mkoani Geita.
Salum Maige, Geita
Mazingira yasiyo rafiki kwa watembea kwa miguu kwenye baadhi ya barabara mkoni Geita,yamekuwa yanahatarisha ulinzi na usalama wa watoto kwenye baadhi ya maeneo hususani mtaa wa Nyantorotoro A kata ya Nyankumbu halmashauri ya mji wa Geita
Miongoni mwa kundi linaloathirika na matukio hayo ni kundi la watoto wadogo wanaosoma darasa la awali na la kwanza ambao kutokana na umri wao hushindwa kutambua ni wakati gani sahihi wa kuvuka barabara wanapoenda ama kutoka shuleni.
Watoto wanaokabiliwa na ajali hizo ni wale wanaosoma katika shule ya msingi Tumaini ambayo iko ng’ambo ya pili ya barabara kuu inayotoka Geita mjini kuelekea Katoro.
Wananchi wa eneo hilo baada ya kuona ajali zinakuwa nyingi wamelazimika kuishinikiza serikali kuweka tuta na alama za barabarani katika eneo hilo ili kuwanusuru watoto na ajali za barabarani ambazo zimesababisha vifo na wengine kujeruhiwa.
.Mmoja wa wakazi wa Nyantorotoro A anasema, yeye alikuwa na watoto wane lakini mmoja alifariki kwa kugongwa na gari wakati akivuka kutoka shule kuelekea nyumbani ,hivyo alilazimu kuwaachisha shule watoto wengine watatu.
“Mwaka jana mwanangu aligongwa na gari akitoka shule akafariki, na nimebakiza watoto watatu nimekataa sisomeshi wapo tu nyimbani hadi pale serikali itakapoweka utaratibu wa usalama wa watoto wetu”
Musa Edward mkazi wa mtaa huo amesema, wananchi wa eneo hilo wamelazimika kuchangishana fedha kwa ajili ya kujenga shule mpya ili kuwanusuru watoto wao na ajali za barabarani ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Mama mzazi wa miongoni mwa wanafunzi wanasoma katika shule ya msingi Tumaini ambao huvuka barabara hiyo kwenda shule, Semeni Meleka amesema, kilio cha wananchi kimekuwa cha muda mrefu cha kuomba serikali kuweka alama za barabara ikiwa ni pamoja na kuomba askari kusimama kuvusha watoto.
“Kila mara ajali zilikuwa zinatokea hapa ombi letu waweke zebra, kila mwezi watoto wamekuwa wanagongwa ,tulikuwa tunaomba trafiki wawe wanasimama hapa ili kuondoa changamoto hizo” anasema Semeni.
Kwa mujibu wa wananchi hao wamesema machi 25, mwaka huu wa 2024 mtoto wa darasa la kwanza jina linahifadhiwa aligongwa na gari katika eneo hilo na kupelekwa hospitali kutokana na kujeruhiwa, na kwamba katika katika kipindi cha kuanzia januari hadi machi mwaka huu watoto watatu wamefariki kwa ajali za kugongwa katika eneo hilo.
Kufuatia tukio la machi 25,wananchi walishinikiza serikali kuthibiti hali hiyo na hivyo serikali ilifika eneo la tukio na kuchukua hatua za kuweka alama za barabarani.
Wakala wa barabara mkoa wa Geita(TANROAD) Mhandisi Ezra Magogo amesema baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi ya muda mrefu kutokana na ajali hizo wameamua kuweka alama za barabarani yakiwemo matuta.
Mhandisi Magogo amesema, eneo la Nyantorotoro limekuwa na shida ya ajali kila wakati na kwamba limekuwa hatarishi kwa wakazi wa eneo hilo wakiwemo watoto wa shule.
“Sisi kwa upande wetu kama Tanroad tumejitahidi kwamba kipande kile cha barabara kinakuwa salama kwa watumiaji waendesha vyombo vya moto na wapita kwa mguu”, amesema mhandisi Magogo.
Ameongeza kuwa, wakala huyo wameweka alama zote zinazostahiki kuwekwa kwenye maeneo ya barabara ikiwa ni pamoja alama ya mwendo kasi kuzuia mwendo usizidi kilomita 50 kwa saa na alama ya kuzuia gari lililoko nyuma kupita la mbele.
WANANCHI WAISHUKURU SERIKALI.
Baadhi ya wakazi wakazi wa eneo hilo wameishukuru serikali kwa kuchukua hatua hiyo ya kuweka alama za barabarani kwani ilikuwa kero kwa wanafunzi wakati wa kuvuka kwenda na kutoka shuleni.
“Kwa sasa hivi tunaona gari zinapunguza mwendo, kwa kweli uawafadhali upo mkubwa sana, sasa mwendesha vyomvo vya moto akipita kwa kasi eneo hilo basi naye atakuwa ni mtu ambaye hajitambui kuvunja sheria kwenye alama” anasema John Samwel.
Mkazi mwingine Elias Totoo amesema “Tunaishukuru serikali kujenga vizuizi mwendo hii itatusaidia wananchi wakiwemo watoto wanaovuka hii barabara kwenda shule ya msingi Tumaini kuvuka salama bila kutokea ajali”
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Tumaini wamesema, ajali hizo zimepoteza wapendwa wao ambao walikuwa wanasoma nao huku wengine wakipata ulemavu na majeraha kutokana na kugongwa na gari pamoja na pikipiki.
"Tunashukuru sana serikali kusikia kilio chetu, wenzetu wamefaiki eneo hili hili la hii barabara ,waligongwa wakapoteza maisha ,hivyo pengine tuta hili na alama hizi zinaweza kupungua au kumaliza ajali" anasema Catherine Tito ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu.
Mmoja wa walimu wa shule hiyo ambaye alionekana kando ya barabara hiyo ili kuwapa msaada wa kuwavusha katikati ya barabara ili waende nyumba ,kwa shariti la kutotaja jina lake ,amesema licha ya kuwepo kwa alama hizo bado wanawapa msaada hasa watoto wadogo kuvuka barabara hiyo.
"Hawa wanafunzi mfano wa darasa la awali,la kwanza na la pili ,tunawavusha kwa sababu umri wao ni mdogo" anasema mwalimu huyo.
Ikumbukwe kwamba huko katika mji wa Katoro wilaya ya Geita wanafunzi 6 walipoteza maisha katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2022 kutokana na ajali za barabarani baada ya kugongwa na gari pamoja na pikipiki walipokuwa wakivuka barabara hiyo ya kutoka Geita kwenda Bukoba na ile Katoro kwenda Rwamgasa.
Mikasa hiyo iliwalazimu wananchi kuchangishana kuanzisha ujenzi wa shule katika kitongoji cha Afya na nyingine katika eneo la Nyamigota hatua ambayo iliungwa mkono na serikali kuanzishwa kwa shule hizo mbali na kupunguza msongamano darasani kuwaepusha pia watoto na ajali za barabarani.
Kwa mujibu wa ofisi ya Taifa ya Takwimu(NBS) ni kwamba watu 1,031 wamefariki dunia na watu 646 wamejeruhiwa kutokana na matukio 1,933 ya ajali za barabarani katika kipindi cha kuanzia januari hadi disemba 2020 nchini Tanzania.
Matukio hayo ya ajali za barabarani yanatokana na vyombo vya usafiri baiskeli,pikipiki na gari ambapo ajali nyingi zikitokana na sababu za kimazingira(2.7%), ubovu wa vyombo vya moto(5.7%), na sababu za kibinadamu(91.6%).
Katika kipindi hicho cha januari hadi disemba, 2020 kwa mkoa wa Geita matukio ya ajali za barabarani ni 71 yaliyosababisha vifo 54 na majeruhi 12.
Kwa mujibu wa kamanda wa Polisi mkoa wa Geita Safia Jongo katika kudhibiti ajali za barabarani, jeshi limefanikiwa kudhibiti ajali kwa kukamata makosa 8,124 ya usalama barabarani, ambapo baadhi ya madereva walitozwa faini na wane kufikishwa mahakamani.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464