Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Mkoa wa Kigoma, Dkt. Julius Zelothe
Mradi wa Afya Hatua unaotekelezwa na Shirika la Tanzania Health Promotion Support (THPS) kwa ufadhili wa Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR) kupitia Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa cha Marekani (U.S CDC) kwa kushirikiana na Serikali umechangia uimarishaji wa huduma za kinga, matunzo na tiba mkoani Kigoma ili kudhibiti maambukizi ya Virusi vya UKIMWI.
Hayo yamebainika leo Juni 14,2024 wakati wa ziara iliyofanywa na Waandishi wa Habari Mkoani Kigoma kwa ajili ya kufuatilia utekelezaji wa Mradi huo wa Afya Hatua.
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Dkt. Isaya Mapunda amesema hali ya Maambukizi ya VVU kwa mkoa wa Kigoma kwa sasa ni asilimia 1.7 hivyo ameshukuru THPS kwa kushirikiana na Serikali katika kutoa huduma za afya hasa huduma za kinga, matunzo na tiba, ikiwemo afua ya kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
“Kwa mfano, hali ya maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto imepungua kutoka asilimia 1.3 mwaka 2022 na kufikia asilimia 1.0 mwaka 2023 na inatarajiwa kushuka zaidi katika mwaka huu wa 2024.”
“Hali ya maambukizi ya akina mama waliokuwa wanaibuliwa katika hudhurio la kwanza kliniki ilikuwa asilimia 0.16 mwaka 2022 lakini kwa mwaka 2023 imepungua hadi kufikia asilimia 0.13”,amesema Mapunda.
“THPS inatoa mchango mkubwa kwa serikali katika kuhamasisha jamii jinsi ya kujikinga na VVU, Upimaji, huduma za kinga, matunzo na tiba. Tunawashukuru sana THPS wamekuwa wadau wakubwa wanaochangia kuendeleza gurudumu la afya kwenye mkoa wetu”,amesema.
Mapunda amefafanua kuwa kabla ya Mradi wa Afya Hatua idadi ya vituo vya tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya VVU vilikuwa vichache, vilikuwa chini ya 60 lakini hivi sasa vituo vingi vya afya sasa vimeongezewa vituo vya tiba na matunzo kwa WAVIU, idadi ya wapokea huduma imeongezeka na wamerahisishiwa kutembea umbali mrefu kufuata huduma kwenye vituo vya afya.
“Kabla ya Mradi wa Afya Hatua tulikuwa tunapata idadi kubwa ya watoto ambao wanazaliwa wakiwa na maambukizi ya VVU lakini sasa hivi hatupati watoto wanaozaliwa na maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kutokana na huduma kuimarika kwa huduma kuanzia mama anapoanza Kliniki hadi anapojifungua. THPS wanasaidia sana katika ufuatiliaji na utoaji wa huduma hizi”,ameeleza Mapunda.
Naye Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Mkoa wa Kigoma, Dkt. Julius Zelothe amesema THPS inafanya kazi na Timu za Usimamizi wa Afya Mkoa na Halmashauri chini ya Mradi wa Afya hatua katika jitihada za kuboresha utoaji wa huduma za kinga, matunzo na tiba kwa wapokea huduma mkoani Kigoma.
“Tunatekeleza mikakati ya kuhakikisha wapokea huduma wanabaki katika huduma za ART katika vituo 69 vya afya. Ili kufikia wapokea huduma katika maeneo ya pembezoni, mradi huu unawezesha huduma za kupatiwa dawa za ART katika ngazi ya jamii ambapo kuanzia Juni 2023 hadi Juni 2024 mradi wa Afya Hatua umeweza kufanya Kliniki 961 za kutoa ART katika jamii kupitia vijiji 89 mkoani Kigoma”,ameeleza Dkt. Zelothe.
Ameongeza kuwa, Mradi huo kwa kushirikiana na Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Kigoma ulianzisha vikundi 32 vya Kuzuia Maambukizi ya Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT) ili kutoa elimu kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha ambapo kuanzia Juni 2023 hadi Mei 2024 , wanawake 551 waliojiunga na vikundi walijifungua watoto 551 ambao walithibitishwa kutokuwa na maambukizi ya VVU.
“THPS inalenga katika kushughulikia changamoto mbalimbali za afya ya umma ikiwa ni pamoja na VVU na UKIMWI, Kifua kikuu, ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, huduma za afya ya uzazi, uzazi, watoto wachanga, watoto na vijana, maabara na mifumo ya taarifa za usimamizi wa afya, UVIKO 19 na tathmini za afya ya umma”,ameeleza.
Amefafanua kuwa Mradi wa CDC/PEPFAR Afya Hatua (Oktoba 2021- Septemba 2026) unatekelezwa katika mikoa minne (Kigoma, Pwani, Tanga na Shinyanga) kwa lengo la kutoa huduma za hali ya juu za kinga, matunzo na tiba ikijumuisha Tohara Kinga kwa wanaume (Kigoma na Shinyanga) na Mpango wa DREAMS ambao unalenga wasichana rika balehe na kina mama wadogo kwa kuwapa afua za msingi ili kupunguza uwezekano wa kuambukizwa VVU.
“Kwa hiyo mradi huu umejikita zaidi katika kuhakikisha kwamba tunatoa huduma hizi ambazo zinahusisha kuwatambua wale wanaishi na VVU ili tuweze kuwaingiza kwenye tiba na matunzo lakini wale ambao hawana maambukizi basi waweze kuendelea kujikinga na kutopata maambukizi. Pia tunatoa mafunzo kwa watoa huduma za afya kwenye vituo vya afya na jamii na kuchangia katika kuajiri watoa huduma hao. Hadi sasa katika vituo 69 ambavyo vinahudumiwa na mradi wa Afya Hatua, tunatoa mshahala kwa wafanyakazi 257.Hali kadhalika tunakarabati vituo vya afya”,amesema Dkt. Zelothe.
“THPS kwa kushirikiana na Timu za usimamizi wa Afya za mkoa na halmashauri (R/CHMT) tunaendelea kushirikiana vizuri katika kuhakikisha huduma za kinga, matunzo na tiba zinazidi kuimarika katika mkoa wa Kigoma”,ameongeza Dkt. Zelothe.
HUDUMA ZA KINGA, MATUNZO NA TIBA KATIKA ZAHANATI YA RUSIMBI MANISPAA YA KIGOMA
Akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma, Bi. Goleth Ezekiel Mama Kinara (Mama anayejitolea ambaye yuko tayari kusaidia ufuatiliaji wa karibu wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha kuhusu huduma za matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), katika nyumba zao na jamii), anasema kupitia mradi wa Afya Hatua wamewezesha kwa kiasi kikubwa kupunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Mama Kinara Goleth Ezekiel akitoa elimu kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma
“Miongoni mwa majukumu ya Mama Kinara ni kuhakikisha akina mama wajawazito wanajifungua watoto wasio na maambukizi ya VVU na wanaonyonyesha wasiwaambukize watoto, wabaki katika matunzo na matibabu ya VVU, kuhakikisha ufuasi mzuri wa dawa (ARV) na dawa kinga kwa watoto. Ninajitahidi kufuatilia watoro katika huduma na utoaji wa huduma za kisaikolojia, ninahamasisha ufuasi mzuri kwenye matibabu ya ART kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha”,amesema Bi. Goleth.
Bi. Goleth ambaye anaishi na maambuzi ya VVU tangu mwaka 2011 na amefanikiwa kujifungua watoto wawili wakiwa hawana maambukizi ya VVU amesema mpango wa Mama Kinara unatumika kuwafuatilia akina mama wanaoishi na maambukizi ya VVU ili waendelee na huduma za kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto lakini pia kupunguza unyanyapaa.
Naye Muelimishaji Rika, Mwera Baraza amewataka akina mama wajawazito kujua hali zao za afya, kuhudhuria Kliniki na kuhakikisha wanajifungulia kwenye vituo vya afya hali ambayo itapunguza maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto huku akihamasisha wale wanaobainika kuwa na maambukizi ya VVU kujikubali na kuwa wafuasi wazuri wa dawa za ART.
Afisa Tabibu katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma, Joram Mathew amesema tangu mwaka 2023 mpaka sasa kituo cha Tiba na Matunzo katika zahanati hiyo kinahudumia wapokea huduma 305 kati yao wanaume ni 73 na 232 ni wanawake.
“Tumekuwa tukihamasisha wanawake wajawazito kuhudhuria Kliniki mapema, kupima na endapo akibainika ana maambukizi anaanza huduma za matibabu mapema. Wanaonyonesha tunawafundisha jinsi ya kunyonyesha watoto na matumizi sahihi ya dawa ili kuepuka kuambukiza watoto. Kwa kweli mwitikio kwa sasa ni mkubwa licha ya kwamba wapo baadhi hawajajikubali kama wanaishi na maambukizi, hawajiweki wazi na hofu ya unyanyapaa”,amesema Mathew.
Hata hivyo kwa mwaka huu, amesema kati ya akina mama wajawazito 15 wenye maambukizi ya VVU waliojifungua, mmoja pekee alijifungua mtoto mwenye maambukizi ya VVU kutoka kwa mama ambapo sababu kubwa ni mama huyo kutokuwa tayari kuzingatia matumizi sahihi ya dawa hivyo akamwambukiza mtoto wake na sasa amejitambua anaendelea vizuri na matumizi ya dawa na mtoto wake ana afya njema.
Mshauri wa Huduma za Matunzo na Tiba kutoka THPS mkoani Kigoma Dkt. Prisila Boniface amesema THPS kupitia Mradi wa Afya Hatua imekuwa ikiwafundisha wanawake wajawazito na wanaonyosha jinsi gani wanaweza kujitunza katika kipindi cha ujauzito na wanaponyonyesha ili wasiwaambukize watoto wao, na pia namna ya kujikwamua kiuchumi.
Aidha Dkt. Prisilla amewahimiza akina mama wajawazito waone umuhimu wa kuanza kliniki mapema, kupima afya mara kwa mara na kujifungulia kwenye vituo vya afya ili kuhakikisha kila mama mwenye maambukizi ya VVU anajifungua mtoto asiye na maambukizi ya VVU.
Kwa upande wake, Afisa Ufuatiliaji Wapokea Huduma za Kinga, Matunzo na Tiba, Juventus Julius ameeleza kuwa endapo mama mjamzito atahudhuria Kliniki kwa tarehe alizopangiwa inasaidia kupata ushauri kutoka Daktari, kupata dawa kwa wakati hivyo kufubaza Virusi vya UKIMWI kwa kiwango cha juu mwisho wa siku asimwambukize mtoto.
ANGALIA PICHA HAPA CHINI
Kaimu Mganga Mkuu Mkoa wa Kigoma, Isaya Mapunda akizungumza na waandishi wa habari Juni 14,2024 ofisini kwake Mkoani Kigoma
Meneja Mradi wa THPS Afya Hatua Mkoa wa Kigoma, Dkt. Julius Zelothe akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za THPS Mkoani Kigoma
Muonekano wa Sehemu ya moja ya majengo katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma
Afisa Tabibu katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma, Joram Mathew akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Goleth Ezekiel, Mama Kinara (Mama anayejitolea ambaye yuko tayari kusaidia ufuatiliaji wa karibu wa akina mama wajawazito na wanaonyonyesha kuhusu huduma za matumizi ya dawa za kufubaza makali ya VVU (ARVs), katika nyumba zao na jamii), akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Mama Kinara Goleth Ezekiel akitoa elimu kwa mama wajawazito na wanaonyonyesha katika Zahanati ya Rusimbi Manispaa ya Kigoma
Muelimishaji Rika, Mwera Baraza akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Mshauri wa Tiba na Matunzo kwa Wapokea huduma za kinga na Tiba za VVU kutoka THPS Manispaa ya Kigoma Dkt. Prisila Boniface akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Afisa Ufuatiliaji Wapokea Huduma za Tiba na Matunzo ya VVU, Juventus Julius akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Afisa Ufuatiliaji Wapokea Huduma za Tiba na Matunzo ya VVU, Juventus Julius akizungumza na waandishi wa habari katika Zahanati ya Rusimbi
Picha zote na Kadama Malunde - Malunde 1 blog