Mojawapo ya kituo cha kulea watoto mkoani Shinyanga
Na Kareny
Masasy, Shinyanga
VITUO vya kulea watoto mchana ‘daycare center’ vimeanza kuchukua hatua ya matakwa ya sheria,sera na muongozo dhidi ya kumlinda mtoto.
Sheria hizo mojawapo ni sheria ya mtoto namba 21 ya mwaka 2009 iliyofanyiwa maboresho mwaka 2019 na muongozo uliopo juu uendeshaji wa vituo hivyo ili viendane na sifa stahiki za ukuaji timilifu kwa mtoto.
Ofisa ustawi wa jamii mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo anasema vituo vya kulea watoto mchana zaidi ya kumi vilituma maombi ya kusajili na vimepatiwa usajili.
Kwesigabo anasema wanaendelea kutoa elimu katika vituo hivyo ikiwa vituo ambavyo vilibainika kukosa sifa kabisa viliweza kufungiwa na kutoruhusiwa kuendesha Shughuli yoyote.
Mwenyekiti wa vituo vya kulea watoto mchana Damary Mollessi anasema makubaliano yaliyofanyika hakuna kuendesha kituo bila kuwa na usajili na wazazi waendelee kuviamini vituo vilivyosajiliwa ili watoto waendelee kupata elimu changamshi.
“Kwani wazazi wamekuwa wakiamini vituo vya kulelea watoto kwa asilimia 100 na sisi wamiliki tujitahidi kufuata miongozo na sheria zinavyoeleza”anasema Mollessi.
Mollessi anasema sasa hivi changamoto ya uanzishwaji wa vituo vya kulelea watoto mchana kiholela umeanza kutoweka sababu ya kujisimamia wenyewe kwanza bila kuangalia maslahi ya fedha kutoka kwa wazazi.
“Tunachoshauri kwa wazazi wasiwapeleke watoto kwenye vituo ambavyo havijasajili kwani kikipata usajili ina maanisha miongozo inafuatwa na mtoto kuwa katika mazingira salama”anasema Mollessi.
Masunga Joseph Mmiliki wa kituo cha kulea watoto mchana anasema aliamua kusajili kituo chake mwaka huu ambapo ana watoto wenye umri wa kuanzia miaka miwili hadi minne alianza na watoto watatu sasa ana watoto 87.
“Tunapenda wazazi nao waelimishwe kuwa mtoto wa miaka miwli hadi mitano akienda kwenye vituo vya kulelea watoto sio kuandika bali ni kuimba na kucheza ilia pate uchangamfu”anasema Masunga.
Naibu katibu mkuu wizara ya Maendeleo ya jamii ,jinsia,Wanawake na Makundi Maalum Amoni Mpanju anasema vituo vya kulelea watoto mchana vinatakiwa kufuata muongozo ili watoto wapate makuzi na malezi bora katika ukuaji wao.
“Ili kufikia ukuaji wenye utimilifu watoto wawe kwenye mazingira bora ya kupata elimu changamshi kwa wakati na umri walio nao katika mazingira salama”anasema Mpaju.
Kwa mujibu wa kitabu cha Proramu jumuishi ya Taifa cha Makuzi,Malezi na Maendeleo ya Awali ya mtoto PJT-MMMAM 2021/2022-2025/2026 hapa nchini Tanzania watoto wenye umri wa miaka miwili hadi minne hawajafikiwa na malezi na makuzi yanayostahili kupatiwa katika ukuaji wao ili kufikia hali ya utimilifu.
Baadhi ya wazazi wenye watoto wanaolelewa kwenye vituo Amina Shija na Gerald Fabian wanasema wamiliki wanaposajili hata wazazi wanaondoa hofu juu ya mazingira wanayoshinda watoto, upataji wa lishe na ujifunzaji unakuwa mzuri.